Talib Ussi, Zanzibar
RAIA wengi wa Tanzania waliopata nafasi ya kutoa maoni mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba wameomba majengo yote yanayohusu Mungano yajengwe sawa baina ya Tanganyika na Zanzibar.
Hayo waliyasema katika Kijiji cha Kiongwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya kuandaa Katiba Mpya Tanzania.
Ali Haji Pandu (68) akitoa maoni yake alisema majengo ya Muungano yawepo Zanzibar kama ilivyo bara.
“Mimi napendelea mfumo huu wa Serikali mbili uendelee, lakini kama Bunge liko bara basi na jingine lijengwe Zanzibar na bajeti ikisomwa Bara na mwaka mkutano mwingine bajeti hiyo ifanyike Zanzibar”, alisema Pandu.
Pandu alisema si vyema kuona majengo yote ambayo ni ya Muungano yanajengwa upande mmoja huku upande ukiwa hauna jengo lolote.
“Hii si haki bwana ni bora maoni yangu yachukuliwe ili kuondoa kero za Muungano ambazo zimedumu kwa muda mrefu” alisema Pandu.
Nasiri Haji Kibaraka (57) naye alisema sasa ni wakati wa kuwa na usawa wa kila kitu ikiwamo madaraka na majengo yake ya Muungano wa Tanzania.
“Jamani madaraka ndio ambayo yameleta kero nyingi za Muungano, kwa maana hiyo ni vyema sasa jengo liwepo bara na pia hilohilo lijengwe Zanzibar na madaraka sawa kwa sawa”,alisema Kibaraka.
“Nakuhakikishieni kama usawa huu utakuwapo na kwambieni kero zote zitayayuka kama barafu” alifafanua Kibaraka.
Ame Saidi Ali (41) akitoa maoni yake alisema usawa wa madaraka utaweza kuondoa kero zote ambazo zimedumu kwa miaka 50.
Tume hiyo kwa upande wa Kaskazini Unguja ipo chini ya Mwenyekiti Joseph Butiku akisaidina na mjumbe, Suleiman Omar Ali.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment