Tuesday, December 25, 2012

CHEKA AWAAHIDI WATANZANIA USHINDI WA KISHINDO, MKANDA KUBAKI TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARIDESEMBA 25, 2012


Bondia wa kimataifa asiyepigika, Mtanzania Francis mwana wa Cheka kutoka katika jiji lisilo na bahari la Morogoro amewaahidi watanzania ushindi wa kishindo katika mpambano wake na bondia kutoka Malawi Chimwemwe Chiotcha kesho tarehe 26 Desemba 2012 siku ijulikanayo kama “Boxing Day”

Wababe hao walizuiwa na maofisa wa ngumi wa TPBC na wale wa IBF kutozipiga kavukavu wakati walipokuwa wanapima uzito kwenye hoteli ya nyota tane (5) ya Naura Springs ya jijini Arusha leo tarehe 25 Desemba 2012.

Cheka amesema kuwa kazi yake ni moja tu kumpiga Chiotcha kipigo kitakatifu ili akumbuke kuwa yeye ndiye jogoo pekee la IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati.Tayari Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (IBF) lenye makao yake makuu katika jiji la New Jersey kule Marekani limeshatuma barua ya kuliruhusu pambano hilo kuwa la ubingwa wa Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati (IBF AMEGP).

Katika barua yake kwa promota wa pambano hilo bwana Andrew George wa kampuni ya Green Hills (T) Limited, Mwenyekiti wa Kamati ya Ubingwa wa IBF Lindsey Tucker alimtakia bwana George mafaniko katika mpambano huo na kuwataja maaofisa wa ulingo kutoka Tanzania kuwa wasimamizi wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, Mtanzania Onesmo Ngowi.

Hii itakuwa mara ya tatu mwaka huu wa 2012 kwa mkanda wa IBF kushindaniwa hapa Tanzania. Mara ya kwanza ilikuwa mwezi wa Aprili mwaka huu wakati Francis Cheka alipopambana na Mtanzania mwenzake Mada Maugo kugombea mkanda wa IBF katika bara la Afrika uzito wa Super Middle.

Mwezi wa August 2012 Ramadhani Shauri alikutana na Sunday Kizito kutoka nchini Uganda kugombea mkanda wa IBF katika bara la Afrika uzito wa unyoya (Featherweight). Mapambano hayo mawili yaliandaliwa na bwana Lucas Rutainurwa wa Kitwe General Traders ya jijini Dar-Es-Salaam.

Mpambano wa mwezi huu wa Desemba ni wa kufunga mwaka huu wa 2012 na utamkutanisha Francis Cheka na Luteni usu wajeshi la Malawi Chimwemwe Chiotcha kugombea mkanda wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati uzito wa Super Middleweight.

Mungu ambariki Francis mwana wa Cheka, Mungu aijalie Tanzania, Amina!

Imetumwa na:

Utawala
Kamieheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC)

No comments: