ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 18, 2012

KAMA TUNATAKA MAENDELEO BASI VIWANDA VILIVYOKUFA VIFUFULIWE


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda.

MUNGU ni mwema ni usemi unaosemwa na wacha Mungu wengi na huo ndiyo ukweli. Kama hivyo ndivyo basi tumshukuru kwa kutuwezesha kuwa na afya njema leo.
Naomba nianze makala yangu kwa kusema kwamba Tanzania iliwahi kuwa na viwanda vingi vya uzalishaji mali enzi ya utawala wa serikali ya awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere naye akawa anaamini kuwa vinaweza kuinua uchumi wa taifa na kuondoka katika daraja la nchi maskini duniani.
Wazo hilo hata mimi ninalo na naungana na Mwalimu Nyerere kwa kusisitiza kuwa tunaweza kupiga hatua za kimaendeleo kama serikali na sekta binafsi zitaanzisha mpango kabambe wa kufufua baadhi ya viwanda vilivyouawa na baadhi ya viongozi wetu.
Nasema hivyo kwa sababu Tanzania kuna malighafi za kutosha ambazo zinaweza kutumika kutengeneza bidhaa viwandani na kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Hivi sasa malighafi hizo zinapotea bure kwa kuwa Tanzania hatuna viwanda vya kutosha vya kusindika na kutengeneza bidhaaa mbalimbali.
Ukweli ni kwamba kuna viwanda vingi ambavyo havifanyi kazi kutokana na ukosefu wa mitambo imara na hivyo kusababisha uzalishaji wa bidhaa kuwa chini.
Kwa ushauri wangu, kwa kuwa wote tunajua kwamba tuna ardhi yenye rutuba ya kutosha, tunaweza kuitumia kwa ajili ya kuzalisha mazao ambayo kama yakisindikwa na kuuzwa, yatasaidia kuinua pato la taifa.
Watanzania wengi, hasa wenye umri mkubwa wanajua kuwa baadhi ya viwanda vilivyokuwa vikifanya kazi miaka ya nyuma hasa katika serikali ya awamu ya kwanza na ya pili, sasa havipo tena baada ya watu waliokabidhiwa kuviongoza kushindwa kuviendeleza.
Baadhi ya viwanda hivyo ni kama Kiwanda cha Nguo cha Urafiki Garments kilichopo Ubungo, Kiwanda cha Maziwa cha Tanzania Dairies Limited, Ubungo Spining Mill, pamoja na cha Zana za Kilimo (UFI) ambacho kilikuwa maalum kwa ajili ya kutengeneza zana za kilimo. Vingine ni Tanzania Sewing Thread na Poly Sacks. Viwanda hivyo hivi sasa havifanyi kazi.
Vipo vya nguo vilivyokufa au kusuasua kama vile Sunguratex, Kiltex, Tabora Textile, Mwanzatex, Mbeya Textile na kadhalika.
Nakumbuka sana kiwanda cha kusindika nyama cha Tanganyika Packers ambacho kilikuwa kikizalisha nyama za kopo zilizokuwa zikiitwa Frey & Bentos na zilikuwa zikiuzwa ndani na nje ya nchi.
Kulikuwa na viwanda vya magunia Moshi na Morogoro, Kiwanda cha Ngozi Morogoro na kadhalika, hakika tulikuwa tunaelekea kupaa kimaendeleo naamini ni watu wachache wametuangusha. 
Hakuna ubishi kwamba katika sekta ya viwanda tuko nyuma mno ukilinganisha na nchi jirani na walioviua kwa kujineemesha wanaonekana mashujaa.
Sasa serikali ni lazima ijipange na kuangalia jinsi ya kutatua matatizo yaliyopo kwenye sekta hiyo ili kufufua viwanda hivyo na kuleta maendeleo nchini.
Ihakikishe inaweka mazingira bora kwa ajili ya kuvutia wawekezaji, kuviboresha na naamini kwa kufanya hivyo sekta ya viwanda itainuka upya na kuleta matumaini ya maisha bora kwa Watanzania kwani watapata ajira licha ya nchi kuingiza kipato.
Aidha, naishauri serikali na sekta binafsi kuungana ili kufufua uchumi kupitia viwanda na siyo kutegemea kilimo tu kwamba ni uti wa mgongo wa taifa kama propaganda za kisiasa zinavyosema.
Hakika mageuzi ya fikra zetu yanahitajika kuitazama upya sekta ya viwanda kwani hata nchi zilizoendelea zinavithamini.
Ukweli ni kwamba vitendo vinahitajika zaidi katika kufufua sekta ya viwanda kuliko maneno ya kisiasa, tuondokane na nadharia na kujikita kwenye vitendo ili wizara inayohusika na viwanda na biashara ipanue soko la ndani na nje, lakini hili litafanikiwa baada serikali na sekta binafsi kuungana.
Kutokana na viwanda vingi kufilisika ni wazi kwamba sasa tatizo kubwa linaloikumba sekta ya viwanda nchini ni ukosefu wa mitaji na tatizo la kupatikana kwa soko la uhakika la kuuza bidhaa za viwandani.
Hakuna atakayepinga nikisema kuwa matatizo hayo yanasababisha kudorora kwa biashara katika nchi zaAfrika.
Ni jambo lililowazi kwamba viwanda nchini havijatengeneza ajira kwa Watanzania hasa vijana kwa sababu hakuna viwanda vikubwa vinavyotumia mitambo ya kisasa kwa ajili ya kugeuza malighafi kuwa bidhaa.
Hii maana yake tunahitaji kuwa na viwanda vikubwa vyenye mitambo ya kisasa na visambae nchi nzima kwa sababu viwanda vingi vipo Dar es Salaam na vichache Arusha ambavyo vipo nyuma kimaendeleo.
Ndani ya nchi yetu kuna tatizo la baadhi ya watu kukwamisha vitu ambavyo ni vya faida kwa taifa kwa sababu zao binafsi. 
Safari hii hilo tusilikubali, ule ujinga wa kuwasifu wezi wa mali za umma kisha kuwaita eti wana akili kwa kuwa wametajirika baada ya kufanya kazi kwa muda mfupi katika mashirika ya umma au serikalini ufe.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments: