Monday, December 24, 2012

Katongo, Sunzu washangaa Ngassa kucheza Bongo

Mrisho Ngasa
Nahodha wa timu ya taifa ya Zambia (Chipolopolo) ambaye pia ni mshindi wa Tuzo ya BBC ya Mwanasoka Bora wa Afrika, Christopher Katongo na beki wa kikosi cha wachezaji 11 wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Stopilla Sunzu walishangaa kusikia kuwa winga Mrisho Ngassa wa timu ya taifa (Taifa Stars) akiendelea kucheza soka la ridhaa ndani ya Tanzania licha ya kuonyesha kiwango cha juu na kufunga goli pekee lililowazamisha katika mechi yao ya kimataifa ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, nyota hao walioshindwa kuisadia Zambia isilale kwa goli 1-0 juzi, walisema kuwa Ngassa anastahili kucheza nje ya Tanzania kutokana na uwezo alio nao.

“Yule mchezaji mwenye jezi namba nane (Ngassa) ni hatari sana. Anazijua njia za mpira na ana kasi sana,” alisema Sunzu, ambaye kaka yake Felix Sunzu anaichezea Simba ya Tanzania.Sunzu aliongeza kuwa Ngassa aiwapa tabu katika eneo la safu ya ulinzi katika kipindi cha kwanza cha mechi hiyo kutokana na uwezo wake wa kukimbia kwa kasi huku pia akiwa mzuri kwa chenga; na anaamini kwamba akipata nafasi anaweza kufanya makubwa akiwa nje ya Tanzania.

Katongo pia alimsifu Ngassa na kusema kuwa awali, alidhani ni miongoni mwa nyota wachache wa Tanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi.

“Yule (Ngassa) ni mchezaji mzuri sana. Nimeshangaa nilipoambiwa kwamba anacheza hapa hapa Tanzania na nilifikiri anacheza nje ya hapa,” alisema Katongo.

Ngassa ‘aliwaua’ Zambia kwa kufunga goli pekee katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza.

MRISHO NGASSA
Baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, Ngassa aliiambia nipashe kwamba hivi sasa amekuwa akimtanguliza zaidi Mungu katika shughuli zake za soka na kuwa, anaamini hata goli alilofunga lilitokana na jitihada za pamoja na dua zake nyingi kwa Muumba.

“Nafurahi kuifungia goli la ushindi timu yangu, hasa ukizingatia tulikuwa tukicheza dhidi ya mabingwa wa Afrika,” alisema Ngassa.

“Kwakweli jamaa (Zambia) ni wazuri sana,” alisema Ngassa, ambaye hivi karibuni alikataa kwenda kucheza soka la kulipwa katika klabu ya El Merreikh ya Sudan kutokana na kile alichodai mwenyewe kuwa ni kutokuwa tayari kuizwa kama ‘mzigo’ kwa kutoshirikishwa na klabu anayoichezea kwa mkopo ya Simba wala klabu yake ya Azam.

Ngassa aliongeza kuwa katika mechi hiyo, yeye alivutiwa zaidi na kiwango kilichoonyeshwa na kiungo Felix Katongo.
“Kwa wachezaji wa Zambia waliocheza leo (juzi), mchezaji aliyevaa jezi nambari 10 (Felix Katongo) ndiye amenikosha zaidi,” alisema Ngassa, kumuelezea Felix anayeichezea klabu ya Green Buffaloes ya Zambia.
CHANZO:NIPASHE

No comments: