ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 24, 2012

TPBC KUMALIZA MWAKA 2012 NA MAFANIKIO LUKUKI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
DESEMBA 24, 2012

Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC) inamaliza mwaka 2012 na mafanikio lukuki ikiwa imeweza kuiletea nchi ya Tanzania mapambano makubwa ya kimataifa zaidi ya matano.

Haya ni mafanikio ambayo yanapaswa kusifiwa na watanzania wote wapenda maendeleo kwani kutokana na mapambano hayo nchi imeweza kujulikana kimataifa, vivutio vyake vya utalii vimeweza kujulikana, nchi imeweza kuwatengenezea vijana ajira, na kuweza kupunguza uhalifu kwa kuweza kuwapa vijana kazi kwani kukaa kwao bure ni kishawishi tosha cha kutumia nguvu zao kwa shughuli ambazo sio za maendeleo.

Katika mwaka unaoishia Desemba 31, 2012, TPBC imeweza pia kuwapeleka nje mabondia zaidi ya 15 wakiiwakilisha nchi ya Tanzania ambako waliweza kuitangaza nchi ya Tanzania vizuri na kuwavutia wageni wakitalii na kuwekeza katika nchi hii inayojulikana kama kisiwa cha amani katika bara la Afrika.

Aidha, TPBC imeweza kuhudhuria mikutano mitatu mikubwa ikiwa ni pamoja na mkutano wa Bodi ya Wakurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) katika jiji la London, Uingereza na ule wa mwaka wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola uliofanyika nchini Bahamas.Kadhalika TPBC iliwakilishwa kwenye mkutano wa 30 wa Shirikisho la Ngumi la Kimataifa na Chana cha Ngumi Cha Marekani (IBF/USBA) uliofanyika katika jiji la Honolulu, jimbo la Hawaii nchini Marekani pamoja na ule wa Baraza la Ngumi la Dunia (WBC) uliofanyika pia katika mjiji la Las Vegas, nchini Marekani.

Hapa nyumbani , TPBC iliweza kutoa vibali na kusimamia mapambano mengi yaliyofanyika katika miji ya Tanga, Dar-Es-Salaam, Morogoro, Songea, Mbeya, Morogoro na Arusha na kuweza kuwapatia mabondia wengi wa kitanzania mikanda ya Kanda, Taifa na Afrika ya Mashariki, Kati na bara la Afrika.

TPBC inawashukuru na kuenzi michango ya mapromota wote waliochangia kuandaa mapambano haya wakiwa ni pamoja na:

Kitwe General Traders, Kaike Siraju Boxing Promotions, Kyando Boxing Promotions, Mwanzoa Boxing Promotions, International Boxing Promotions, Selemani Siminyu, Green Hills (T) Limited na wengine wengi.

Aidha TPBC inapenda kuishukuru TPBO chini ya Abdalla Mwaipaya Ustaadh kwa ushirikiano wake katika kuendeleza ngumi za kulipwa Tanzania.

Tunapenda pia kuwashukuru wadau wote waliochangia kwa njia moja au nyingine kama vile vyombo vya habari, mamlaka za miji na miji na majiji, jeshi la polisi, kumbi zote za burudani zilizotumika kuandaa mapambano haya na wadau wengine wengi.

Pia tunaishukuru serikali kupitia Msajili wa Vyama (Mambo ya Ndani), Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa ushirikiano wao katika kusaidia kuendeleza ngumi za kulipwa nchini.

Imetolewa na:

Onesmo Ngowi
Rais, TPBC
Dar-Es-Salaam,Tanzania

No comments: