Monday, December 24, 2012

Lema kuzoa Sh85 Milioni


Mb. Godbless Lema,

*NI MALIMBIKIZO YA MSHAHARA NA MAFAO KWA KIPINDI ALICHOKUWA NJE YA BUNGE

MBUNGE wa Arusha Mjini (Chadema)  Godbless Lema, akazo kitita cha Sh85 milioni ambazo ni malimbikizo ya mishahara na posho mbalimbali ambazo hakulipwa wakati alipokuwa nje ya Bunge.

Lema amekuwa nje ya Bunge kwa miezi minane, kuanzia Aprili 5 mwaka huu wakati alipovuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, hadi aliporejeshewa ubunge wake Ijumaa wiki iliyopita na Mahakama ya Rufani ambayo ilikubali rufaa yake iliyopinga uamuzi huo.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah jana alisema baada ya kurejea bungeni, Lema atalipwa stahili zake zote anazostahili kwa muda wote wa siku 260 ambao alikwa nje ya Bunge.

Ingawa ofisi hiyo ya bunge haikusema atalipwa shilingi ngapi, uchambuzi wa malipo na stahili za wabunge umebaini kuwa mbunge huyo kupitia Chadema, atalipwa kitita cha Sh85 milioni ikiwa ni mshahara wake na posho kwa kipindi cha miezi nane alichokuwa nje ya Bunge.
Hata hivyo, Lema mwenyewe aliliambia gazeti hili jana kuwa, malipo yake yanaweza kufikia Sh60 milioni.

Lema aliyeibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, alivuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, April 5, 2012, kufuatia kesi iliyofunguliwa na makanda watatu wa CCM; Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agness Mollel, wakipinga ushindi wake. Hata hivyo, Desemba 21,2012, Mahakama ya Rufani ilimrejesha bungeni, baada ya kushinda rufaa yake aliyokata mahakamani hapo kupinga hukumu na tuzo ya Mahakama Kuu Arusha iliyomvua wadhifa huo.

Tangu alipovuliwa ubunge hadi Mahakama ya Rufani ilipomrejesha tena bungeni, Lema alikuwa amekosa mikutano mitatu ya Bunge yenye jumla ya vikao 84.

Mikutano hiyo ni ule wa mwezi Aprili, mkutano wa Bunge la Bajeti Juni hadi Agosti na mkutano wa Novemba.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya Bunge na wakiwamo wabunge wa upinzani na wale wa CCM vilisema kwamba malipo ya mbunge kwa mwezi ni Sh10.7 milioni, yakijumuisha Sh2.3 milioni za mshahara, Sh2.5 milioni za mafuta, posho ya jimbo inayokaribia Sh5 milioni na malipo mengineyo.

Kwa muda wa miezi zaidi ya minane ambao amekuwa nje ya Bunge, malimbikizo ya mshahara wake yanafikia Sh18.4 milioni, posho ya jimbo Sh40 milioni, mafuta Sh20 milioni na posho nyingine Sh6.6 milioni.

Kauli ya Lema
Hata hivyo akizungumza na Mwananchi jana, Lema alisema kuwa ingawa hajui kwa hakika kuwa malipo yake ni kiasi gani, lakini kwa hesabu za haraka, yanafikia Sh60 milioni.
Alisema wakati wa kesi hiyo ikiendelea hakuwahi kuwaza kwamba angerejeshwa bungeni, hivyo hakuwahi atalipwa kiasi gani na Bunge.

“Sijui kwanza nitalipwa nini kwani sikuwahi kukaa na kupiga hesabu za malipo haya, maana najua ubunge siyo faraja bali ni kuongoza harakati za kuwasaidia wananchi kutetea haki zao mbalimbali,” alisema Lema.

Alisema alichokuwa akijua ni kwamba kama akishinda basi, atarejeshewa gharama za kesi yake na makada wa CCM ambao walimfungulia kesi kwani ni malipo yanayotambulika kisheria.
“Najua lazima hawa makada wa CCM, walipe gharama zangu za kesi.Baada ya wao kushinda kesi Mahakama Kuu, Arusha, waliniletea madai ya kuwalipa Sh139 milioni na sasa mimi nawadai zaidi ya milioni 250,” alisema Lema na kuongeza:

Chanzo:Mwananchi

No comments: