ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 24, 2012

Afisa Mtendaji na wengine watano kortini kwa mauaji ya polisi Ngara

Na Daniel Limbe.
Watu sita wakazi wa kijiji na kata ya Mugoma akiwamo mtendaji wa kijiji hicho wilayani humu, wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya mauaji ya askari polisi wawili na kuchoma kituo cha polisi.

Waliofikishwa mahakamani hapo wiki iliyopita ni Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mugoma, Method John, Suleiman Zuberi, Rashid Ally, Issa Athuman, Simon Chuma na Aman Maulid.

Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Tumaini Membi, alidai kuwa washtakiwa hao waliwaua polisi wawili kwa kutumia silaha za jadi na kuchoma kituo kidogo cha polisi Desemba 15, mwaka huu saa 8:15 mchana.

Aliwataja polisi waliopoteza maisha kuwa ni E 5792 Koplo Paschal na H 429 Konstebo Alexander.

Katika shitaka la pili, alidai kuwa washatakiwa hao walichoma kituo kidogo cha polisi Mugoma na kusababisha kuungua nyaraka za polisi zenye hamani ya zaidi ya Sh. milioni 68.

Vile vile, Mwendesha Mashitaka huyo alizitaja mali za jeshi hilo zilizoteketea kwa moto kuwa ni pikipiki tatu zenye namba za usajili PT 1348,PT 1341 aina ya Yamaha ambazo ni mali ya jeshi hilo pamoja na T.767 AXH Sanlg iliyokuwa kielelezo cha baadhi ya wasitakiwa na baiskel moja.Mbele ya Hakimu Msaidizi wa Mahakama ya Wilaya ya Ngara, Andrew Kabuka, washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.

Wasshtakiwa walirudishwa rumande mpaka hapo kesi yao itakapotajwa tena Januari, mwakani.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro, aliyeko wilayani Ngara kikazi, amejikuta katika wakati mgumu baada ya mwananchi mmoja mkazi wa kijiji cha Mugoma kuibuka na kuelezea wazi mkasa wa mauaji ya polisi wawili na raia mmoja.

Kijana huyo, Said Rugwiza, aliyejitokeza kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na Kamanda Sirro, alieleza kuwa yeye akiwa eneo la tukio, alishuhudia unyama uliofanywa na polisi hao kwa kumuua Said Mkonikoni, kwa risasi na kudai kuwa aliyehusika kumuua raia huyo ni askari anayejulikana kwa jina la Hamis kutoka kituo cha Polisi Mugoma.

Alidai kuwa polisi huyo alimpiga risasi mguuni kabla ya mwenzake Konstebo Alexander, kumpa bunduki Koplo Paschal, ambaye alimmalizia kwa risasi kifuani.

"Wakati fundi wangu Mkonikoni akiburutwa kutoka kwenye gereji yake kuelekea kituo cha polisi, kwanza alipigwa ngumi na askari Alex...na ndipo katika hali ya kujitetea na yeye alirudisha ngumi kwa kumpiga askari huyo na baadaye walimpiga ngwala akaanguka chini...na ndipo akapigwa risasi mguuni...mimi nikishuhudia kwa macho yangu," alisema Rugwiza.

"Kutokana na kuvuja damu nyingi kwenye mguu huku akilia...askari Alex alishikwa na kiwewe na kutaka kukimbia, lakini mwenzake Paschal alichukua bunduki na muda mfupi nikiwa nimemshikilia fundi wangu mkono, nilishtukia imepigwa risasi nyingine na damu nyingi kuanza kufoka ikitokea mgongoni na ndipo alinizidi uzito nikashindwa kumnyanyua akawa amekufa," aliongeza.

Baada ya mauaji hayo kutokea polisi hao watatu walitimua mbio sehemu tofauti na ndipo wawili waliingia kwenye kituo cha polisi baada ya kuona wananchi wanawafuatilia kabla ya kuanza kukichoma kituo hicho kwa moto.

Kufuatia hali hiyo, Kamanda Sirro aliwataka wananchi kutulia na kuliamini Jeshi la Polisi na kuwaahidi ukweli wa tukio hilo kuwa utajulikana na wote waliohusika lazima watafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili haki itendeke.

“Ndugu wananchi, kwa sasa suala la mauaji ya raia na askari wetu wawili, liko kwenye utaratibu wa ufuatiliaji wa kisheria tuwe na subira ili matokeo ya uchunguzi na haki iweze kupatikana muhimu tujihusishe na mambo ya kuleta maendeleo,” alisema Kamanda Sirro.

“Pamoja na mauaji hayo kutokea Jeshi la Polisi litaendelea kufanya kazi ya kulinda usalama na amani na zoezi la kukamata vyombo vya usafiri na kuwakamata wanaohatarisha usalama...hakuna mtu atakayeonewa kwa madai ya kulipiza kisasi,” alisisitiza.

No comments: