NI mada ambayo inajenga zaidi kujiamini kwa kila mtu kwa mwenzi wake. Kutanguliza nafsi yakoni kitu muhimu mno. Tupo katika sehemu ya tatu ya mada yetu, tuendelee kuwa pamoja...
Kama mwenzi wako hafai au anafaa, jibu lipo ndani ya kuta za moyo wako. Ndiyo maana linapokuja suala la kupokea ushauri wa kimapenzi, unatakiwa umuone mtu ambaye ana sifa ya kutoa ushauri. Tafuta washauri na siyo wapondaji.
Unaweza kuwaazima masikio marafiki zako, wakampaka mwenzi wako badala ya kukupa ufumbuzi wa kile kinachokusumbua. Mwisho ukaona yao ni mazuri halafu kwa hasira ukafikia uamuzi wa kuachana naye, utajuta baadaye. Itakutesa zaidi baada ya kubaini kuwa mmoja wa waliokuwa wanamponda ndiye kamchukua.
MJALI MWENZI WAKO KULIKO CHOCHOTE
Hiyo ni nidhamu kuu. Hapo unashauriwa kitaalamu kuwa mwenzi wako kama mtu ‘spesho’ zaidi wa maisha yako, unapaswa kwenda naye kwa maelewano. Kusikilizana na kupeana muongozo wa kila siku katika maisha.
Fikiria kuwa una marafiki wengi, ndugu na jamaa mlioshibana lakini mwishoni unapotaka kulala, hurejea nyumbani na kujifunika shuka moja na mwenzi wako. Bila shaka unaona ni kwa namna gani huyo anashikilia kipengele nyeti cha maisha yako.
Dunia katika pointi ya maradhi, hususan Ukimwi na magonjwa mengine ya ngono, ni yeye ndiye anayeweza kukuweka huru. Damu yako ikawa salama, kwani kinyume chake asipokuwa makini, anaweza kuchetuka, akachetukia maradhi, mwisho akakuletea gonjwa uhangaike nalo.
Kwa maana hiyo ni mlinzi wa maisha yako. Unalala fofofo karibu yake na mpo wawili tu chumbani, ukiamka hujikuti na jeraha lolote. Usipomjali mtu wa namna hiyo unataka thamani yake ukampe nani?
Kuna kundi la watu huwatanguliza marafiki kuliko wenzi wao. Yaani katika pande mbili, mwenzi wako anasema hili, halafu wewe unasikiliza neno la rafiki kwanza. Hilo ni kosa kubwa ambalo ni rahisi kuyeyusha upendo.
Ni bora unapoona mwenzi wako anaongea kitu ambacho unaona hakifai, utumie muda wako kumuweka sawa na akuelewe. Usithubutu kufanya kinyume chake kama hakuelewi. Mwisho kabisa, ukiona mwenzio ana wasiwasi, jiepushe na hicho anachokihofia au mfanye aondoe mashaka.
Mwenzi wako anahisi kuna mtu unatoka naye kimapenzi. Fahamu kuwa hilo linamtesa moyoni, huwezi kujua kaambiwa na wangapi mpaka akaja kukuuliza. Zifanye fikra zake ziwe huru kwa kumuelewesha mpaka aelewe au jiepushe na huyo mtu.
Naamini katika ‘Kitchen Party’ lakini sikubaliani na dhana kuwa ili mwanamke awe bora kwenye mapenzi au ndoa yake ni vema apitie katika mafundisho ya namna hiyo.
Inahitaji busara za kufikiria na kuamua. Kutambua wewe mwenyewe unahitaji nini kisha upime na kile ambacho unaambiwa. Hata kumhudumia mwenzi wako chumbani ufundishwe?
Mapenzi si taaluma kwamba kuna tabaka la watu fulani ambalo limefuzu. Kila mtu anaweza, kwa hiyo unaweza pia. Muhimu ni kujitambua, kung’amua maeneo yako hatarishi na kujiweka wazi.
Kuna ugumu gani kumueleza mwenzi wako kuwa eneo hili na lile ndiyo muafaka? Unadhani anaweza kuja malaika kutoka mbinguni wa kutii kiu yako? Ni wewe na yeye, ndiyo maana mpo ‘spesho’.
Mwanaume kwenda ‘Bag Party’, sipingi lakini ni utamaduni ambao hauna matunda mema. Kinachoweza kukupa uhakika wa kumudu penzi lako ni kuamini katika kile kinachokuunganisha na mwenzi wako.
Unatakiwa ujue sababu ya wewe kuwa na mwenzako kabla ya mwingine yeyote. Faida zake zifike kwake.
Itaendelea wiki ijayo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment