Monday, December 24, 2012

LINDA PENZI LAKO ILA MWENZI WAKO AKING’ANG’ANIA MUACHANE, USIMLAZIMISHE-4


TUNAENDELEA na mada yetu tuliyoianza wiki kadhaa zilizopita. Tunajadili juu ya umuhimu wa kulinda penzi lako. Tunaendelea kuanzia pale tulipoishia.
Kasoro mnarekebishana wawili, tena katika eneo ambalo hukutani na mtu mwingine yeyote. Mapenzi yana maana kubwa!
Ni katika hilo, ndiyo maana ya kutoa pointi kwamba hupaswi kuamini katika maneno ya watu ili kuchukua uamuzi hasi au chanya kuhusu mwandani wako. Kila kitu kipo ndani yako, hakuna mtu wa nje anayejua zaidi.
Inaposemwa sikitiko la mahaba linashinda msiba, maana yake ni kuwa ukifiwa utalia na wengi lakini maumivu ya moyo yanayotokana na mapenzi, yatakuuma peke yako. Hayupo atakayelia kilio cha kweli pamoja na wewe.
Hatatokea mtu ambaye anaweza kuhisi kile ambacho kinakutoa machozi. Tunakataa utengano lakini hoja ya msingi hapa ni kuwa tafsiri ya mapenzi ni kitu chenye ubaguzi, kwamba “ni sisi wawili tu, kwa ajili yetu, furaha yetu na kila kinachotuhusu!”

MWENZI WAKO NI NAMBA MOJA
Haihitaji kufuzu elimu ya chuo kikuu kujua hili. Hata yule ambaye hajapita kabisa shule anafahamu kwamba binadamu anavyoishi, kila kipindi anajikuta anapoteza marafiki na kupata wengine.
Inalazimishwa na hali halisi ya maisha. Unaposoma makala haya, mwisho wa aya hii fumba macho ukumbuke ni marafiki wangapi ambao ulikuwa nao, ukashibana nao mpaka ukadhani wao ni sehemu ya maisha yako?
Bila shaka ni wengi, baada ya hapo jiulize swali lingine, wote hao wapo wapi? Unakuja kugundua kwamba kuna baadhi hata hujui walipo katika huu mgongo wa ardhi.Mmekwishapotezana, kila mtu anaangalia ustaarabu wake.
Kwa mwenzi wa maisha yako, mtaishi mpaka kufa. Mtaambatana kila mahali kwa sababu maisha yako hayakamilishi tafsiri yake bila uwepo wake, kwa maana hiyo hupaswi kudanganyika kwa hoja dhaifu za kukuchonganisha naye.

USIACHE MBACHAO KWA MSALA UPITAO
Hutakiwi kuwadharau marafiki lakini usiwape nafasi kuzidi hata ile ambayo wewe humpa mwandani wako.
Nina mfano wa mtu aliyekuwa anateswa mno na marafiki wa mke wake. Jamaa kila siku anaonya kuhusu aina fulani ya watu lakini mke hasikii. Ndiyo kwanza maneno yanaingia sikio la kulia kabla hayajafika sikio la kushoto yanapotea.
Mume akawa analalamika kuwa anazidiwa nguvu na marafiki wa mwenzi wake, kwamba hana kitu chochote cha kuamua endapo marafiki wa mke wake watasema chochote. Sikitiko la mume mwisho likampa shinikizo la damu! Mapenzi yanatesa!
Mume akalalamika kuwa akimkataza mke wake kutoka, wakija marafiki wataondoka naye hata kama itakuwa ni usiku. Wakati mwingine wanatoa maneno ya kuudhi, “achana naye, kwani mwanaume peke yake!”
Ni kosa kubwa kwa sababu wanaopotosha ni watu wa kupita. Mume au mke ndani ya nyumba upo naye leo na kwa uweza wa Mungu, ni kifo ndicho kitakachowatenganisha. Huyo mpiga debe hajui kinachokutuliza kwake.
Hii ni kwa mume na mke, kwani wapo wanaume wengi hawajui kutunza hisia za wenzi wao. Wamelemaa kwa hulka za mfumo dume, matokeo yake wanaharibu. Usisikilize ya watu, mwache akushauri lakini si kukupangia maisha.
Tafuta watu wanaojua kutoa ushauri wa kitaalamu na si kudandia kila mtu. Wengine hawajui tafsiri ya kuumizwa na mapenzi, kwa hiyo si ajabu akakwambia umuache! Kumbuka kwamba utakapokuwa unalia, moyo unauma, machozi yanatoka, unakosa usingizi, yeye hatakuwepo. Ni maisha yako!

www.globalpublishers.info

No comments: