ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 18, 2012

MAISHA NDIVYO YALIVYO: Ukitaka kujua mwanamke ni jasiri, hali ya nyumbani kiuchumi iende vibaya

NA FLORA WINGIAMpenzi msomaji, hebu leo tuzungumzie kidogo kuhusu vijana wetu wanaojitosa kwenye ndoa kama kweli wanakuwa na maadalizi ya kutosha.

Wapo wanaoingia kwenye kundi hilo kiushabiki eti naye ajulikane kuwa amefunga ndoa, wengine kutafuta umaarufu, wengine kuonja yaliyomo kisha kuchomoka.

Hivi majuzi (Jumatatu iliyopita),nilikutana na marafiki zangu tukawa tunapata soda.

Kidogo akafika kijana mmoja mkazi wa mtaani kwetu ambaye alikuwa amefunga ndoa Jumamosi Desemba mosi, mwaka huu.

Kwenye kikao kile ambapo tulikuwa wanne, wote tukaanza kumshambulia kwanini yuko pale wakati ule, tena peke yake wakati ni takriban siku moja tu tangu afunge ndoa kanisani.

Kijana huyu akajitetea kwa nguvu kwamba kwanza ni jirani na nyumbani na eti aliomba ruhusa kwa mwenza wake aende dukani kununua vocha.
Lakini alipokuta wazee wamekaa naye akasalimia kijanja lakini lengo likiwa kupata bia moja.

Utetezi huo haukutosheleza na ndipo wazee walipoanza kumfunda kuhusu ndoa na kashkash zake, huku tukimwambia kwamba asidhani ni lelemama. Mwenyewe akawa anajipa moyo kwamba hapana shaka atamudu kwani mke alimchagua mwenyewe.

Yafuatayo ni baadhi ya mawaidha aliyopewa kijana yule kwamba;-

Mmoja akamshauri kwa kusema; “Unapooa usidhani kuwa umemaliza kila kitu. Hiyo ni changamoto ambayo inasubiri utekelezaji. Na utekelezaji wenyewe na ule mpangilio wa maisha utakavyokuwa baada ya ndoa.

Mwanamke au mwanaume wanaotaka kuingia katika mkataba wa ndoa, bado hawajawekana sawa kwamba nini mmoja anataka kutoka kwa mwenzake.

“Kwa mfano mwanamke yawezekana hakumtaka yule bwana bali watoto atakaozaa naye. Yaani hakuhitaji sana wewe mwanaume, lakini kwa sababu tu umeunganishwa naye kwa ndoa “.

Mwingine ambaye ni mwanaume akadakiza; “Mwanamke akikuheshimu sana, ile mimba ya kwanza haina uzito.
Itakapotokea mimba ya pili kama mkeo hajakuambia kitu utakuwa na bahati.

Yaani kipindi hicho atakuwa yapo mengi ameyavumilia na sasa anakuwa na nguvu ya kuyatoa moyoni. Kama ni uvumilivu anakwambia basi.

“Kwa wanawake wana haki ya kufanya hivyo hata kama mwanaume atabisha lakini wanakuwa wamesimamia ukweli fulani. Wanaume siku zote, kitu ambacho hawataki kukubali ni kuambiwa ukweli.

Wanaume hujaribu kuwakandamiza au tuseme kuwapelekesha wanawake kwa sababu ya ujeuri wao na hasa kwa kuambiwa kuwa wao(wanaume) ni kichwa’.

Mwingine pia mwanaume akasema, “Lakini ukitaka kujua mwanamke ni jasiri, hali ya nyumbani kiuchumi iende vibaya, utasikia mwanaume anasema ‘nifanyeje’.

Lakini mwanamke atapiga ubongo kuangalia kazi itakayoleta kipato.

Anaweza kuanzisha biashara inayoingiza sh.1000 kwa siku, japo mume ataipuuza lakini ni kipato muhimu kikisimamiwa vema”.

Wakati bwana mdogo huyu aking’ang’ana kuwa yote atayamudu kwa uwezo wa Mungu, simu yake ya mkononi ikaita, “ ndiyo ma darling, nakuja usihofu, mpenzi wangu…niko karibu, nisubiri….Aaaah ma love wewe ni mke wangu niliyekuchagua, sina mwingine, nakuja sasa hivi…”

Wakati akiwa bado anazungumza ambapo ilibidi anyanyuke na kwenda kando, pale tukacheka wote.

Tukawa tunasema si ndiyo tulikuwa tunamwambia kwamba ndoa siyo lelemama. Ndoa yataka kutulizana na kutafakari kule uendako.

Siyo wakati wa kahanjahanja tena na kuvinjari ovyo kwenye vijiwe vya burudani, ni kipindi cha mabadiliko kutoka usela na kujiandaa kuwa baba wa familia.

Hili vijana wengi hawalijui, wanadhani kuingia kwenye ndoa ni fasheni, kumbe ni kuleta matatizo nyumbani kama hutakuwa makini.

Kijana yule aliporejea, akawa amebadilika. Wanajopo wakaendelea kumfunda huku wakimhimiza kuwa ni muhimu asikilize wito wa mkewe kwani anammisi hasa ikizingatiwa kuwa ni siku moja tu tangu wafunge ndoa.

Na kusema ukweli mwanaume kiruka utamjua tu. Yaani siku moja tu baada ya ndoa tayari utatafuta vijiwe vile vile ulivyozoea kupiga soga na kumwacha mke roho ikimwenda mbio kwamba mume yu wapi?

Vijana yafaa wabadilike na wajiandae vema katika kutoka maisha ya ujana na kuingia katika maisha ya ndoa. Kama kweli wanataka maisha bora na tulivu, ni lazima watulizane na waweke wazi nyendo zao iwe ni mke au mume.

Ukweli na uwazi na uvumilivu ni miongoni mwa misingi mizuri katika maisha ya ndoa.

No comments: