ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 1, 2012

MAKOSA KULIGEUZA PENZI KAMA ZAWADI

NAMSHUKURU Mungu kutukutanisha tena ili tuendelee kufundishana kwa wasiojua na kukumbushana kwa waliosahau. 
Wengi wameniona kama nabii au mnajimu kwa kuingia ndani ya mioyo yao na kuyasema yanayowasibu, ukweli ni kuwa sina sifa hizo bali Mungu kanipa jicho la tatu kuyafahamu matatizo katika maisha yetu ambayo yapo wazi, hayajifichi ila ni wachache wenye kugundua haraka dosali katika mapenzi.
Wapo ambao hupoteza dira wasijue wafanye nini kutokana na kutatizwa na mapenzi hadi kufikia hatua ya kujiona wana bahati mbaya au mikosi.

Unapokuwa unaangalia tatizo bila kujua chanzo, utakuwa mtu wa kurudia makosa na mwisho utajiona una bahati mbaya au nuksi.
Kumekuwa na tabia za watu fulani kuamini wao katika mapenzi ni kila kitu na kitendo cha kuwapa wenzao penzi ni kama zawadi. Tatizo hili limekuwa kwenye uhusiano mwingi, inawezekana kabisa nawe ni muathirika wa tatizo hili.
Unajikuta upo kwenye mapenzi, lakini mpenzi wako amekuwa na kauli hii ambayo hupenda kuirudia:
Una bahati sana, hata sielewi kitu gani kimefanya tuwe pamoja, kuna watu kibao wamenitaka lakini hakuna hata mmoja aliyebahatika ila wewe ndiye una bahati. 
Maneno haya ukifikiria kwa juujuu unaweza kuamini kweli una bahati kupewa penzi na mtu fulani mwenye kiwango. Lakini ukiyaangalia kwa upande wa pili, inaonyesha kabisa haukuwa na hadhi ya kuwa mpenzi wake bali alichokupa ni zawadi. Nina imani nimesomeka vizuri!
Penzi la aina hii mwenye uamuzi huwa mmoja kwa vile ndiye anaamini kabisa penzi alilokupa ni zawadi, huna kauli kwa vile anaweza akakunyang’anya wakati wowote. 
Watu wa aina hii huwa hawaombi msamaha wanapokosea kwa vile huamini hata ukikasirika huwezi kumfanya chochote! Wanapenda kusikilizwa wao kila wakati hata kama jambo linakuwa halina umuhimu na huyaona mambo ya wenzao hayana maana.
Hufanya mambo kwa kulazimisha kwa kujua huwezi kukataa kwa vile zawadi ya penzi lake bado unaihitaji. Ni wepesi kutishia kuvunja penzi kwa kuamini huna shukurani kwa penzi analokupa.
Huamini wao ndiyo wanaopoteza muda kuliko wengine. Hata kama amekuweka sehemu kuanzia asubuhi hadi jioni, dakika tano zao huzithamini kuliko muda wako.
Watu hawa hawana tofauti sana na wabinafsi kwenye mapenzi. Wao huamini ndiyo walioshikilia ufunguo wa penzi lenu kwa kuamini ndiyo wenye uwezo wa kuliendeleza au kulivunja.
Huamini upande wa pili hauna jeuri kwa vile wao wapo juu kwa kila kitu na walichokupa si haki yako bali ni msaada ambao kikomo chake wanakijua wao. Inawezekana wewe ni mmoja wa watu wenye tabia hii ambayo mwisho wake huwa na maumivu makali. 
Nataka kuwaeleza kitu kimoja, hakuna penzi  la mmoja kuburuzwa. Wanaofanyiwa hivi wengi wao huwa wavumilivu huku wakijitahidi kuwaeleza wenzao baadhi ya vitu ambavyo havitakiwi kuwa katika mapenzi. 
Mara nyingi watu wa aina hii wanapochoka upendo huondoka moyoni na kuamua kulivunja penzi. Hapo ndipo unakuja kushtuka baada ya makosa yako kugeuka sumu iliyoua penzi lenu. 
Hapo utajitahidi kumrudisha, anaweza kurudi lakini hatakuwa na mapenzi tena na wewe na penzi lenu linakuwa halina nguvu kwa vile hana imani na wewe tena. 
Ili kulirudisha penzi la awali, lazima uwe mtumwa wa mapenzi.
Mapenzi si zawadi bali makubaliano ya watu wawili walioridhiana, ni makosa upendo kugeuka zawadi. Kumpenda mpenzi wako ni haki yake kwa vile hukulazimishwa kupenda au kupendwa.
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.

www.globalpublishers.nfo

No comments: