ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 7, 2012

Mke wa Mandela aeleza mwarobaini ndoa za utotoni

Asasi za kiraia nchini zinazojishughulisha na utetezi wa wanawake na kutokomeza ndoa za utotoni, zimepewa changamoto ya kutafiti kwa kina chanzo cha unyanyasaji wa kijinsia, ili kazi ya kupambana nayo iwe rahisi.

Akizungumza na wanaharakati mbalimbali wanaounda mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni nchini (TECMN), Mwanaharakati mashuhuri barani Afrika, Mama Graça Machel, alisema asasi za kiraia zinapaswa kubaini chanzo cha ndoa za utotoni na ukatili mwingine kwa kila kabila.



Alisema chanzo cha kuozesha wasichana wadogo kinatofautiana kutoka kabila moja na lingine akieleza kuwa wengine wanaozeshwa kwa sababu ya mila potofu na wengine ni umasikini.

“Ni vizuri mkajua nini kinachosababisha wasichana kuozeshwa wakiwa na miaka tisa, kama wanaharakati mnapaswa kujua nini kinafanya unyanyasaji huu uzoeleke,” alisema.

Mama Machel alisema inasikitisha kuona familia na jamii nzima inachukulia ndoa za utotoni kama suala la kawaida na kwamba ni vyema wadau wote ikiwemo serikali kushirikiana kulitokomeza.

Alisema wakati umefika sasa kwa serikali kutekeleza kwa vitendo mikataba mbalimbali ya kimataifa iliyoridhiwa na nchi pamoja na kuzifanyia marekebisho sheria zote zinazohalalisha ndoa za utotoni.

Mama Machel mbali ya kwamba ni mwanaharakati mashuhuri, pia ni mwanzilishi wa asasi za kiraia katika nchi mbalimbali ikiwemo ya kwake inayojulikana kama Graça Machel Trust (GMT), inayojishughulisha na harakati za kumkomboa mwanamke kwa kutoa elimu ya haki za wanawake na watoto barani Afrika.
CHANZO: NIPASHE

No comments: