ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 13, 2012

Mkurugenzi h’shauri adaiwa kumtwanga vibao mtumishi

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Robert Kitimbo anadaiwa kumtandika vibao ofini kwake, mtumishi wa Idara ya Afya ya Manispaa hiyo, Mwendwa Mhembano alipokwenda kudai fedha za kununulia sare.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilidai kuwa katika tukio hilo ambalo limeripotiwa polisi, mbali na kumpiga, mkurugenzi huyo alimsukuma na kumwangusha mtumishi huyo na kumsababishia maumivu.

Imedaiwa kuwa siku ya tukio hilo, Mhembano ambaye ni muuguzi katika Hospitali ya Makole iliyopo katika Manispaa ya Dodoma, alifika katika Ofisi ya Mkurugenzi huyo akitaka kupewa ufafanuzi kuhusu Sh150,000 alizostahili kulipwa kwa ajili ya kununua sare kwa mwaka.
Baada ya kuingia ofisini kwa mkurugenzi huyo, ilidaiwa kuwa muuguzi huyo alieleza matatizo wanayopata, ikiwamo ukosefu wa vifaa na sare za kufanyia kazi, lakini maelezo hayo yalimkera kiongozi huyo na kuanza kumchapa vibao sambamba na kumkaba shingo na kumsukuma.

Akizungumza jana mjini hapa, Mhembano alidai kwamba alipigwa na mkurugenzi huyo na kueleza kuwa tayari suala hilo alishalifikisha polisi na kufunguliwa jalada DOM/RB/12805/2012.
“Nilikwenda Polisi kutoa taarifa waliniandikia barua ya matibabu (PF3), kimsingi niliumia goti la kulia kwa sababu alinisukuma na nilianguka sakafuni,” alisema Mhembano.

Hata hivyo, Mhembano alisema hajui kinachoendelea baada ya kutoa taarifa hiyo polisi kwani hadi sasa hajaona mkurugenzi huyo akikamatwa wala kuhojiwa na polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alithibitisha kupokea malalamiko hayo ya Mhembano na kusema kuwa bado anayafuatilia.

“Taarifa hizo tunazo lakini bado tunazifanyia kazi. Tutakuwa na majibu ya kutosha baada ya kumaliza uchunguzi wetu,” alisema kamanda huyo jana.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alikanusha kumpiga mtumishi huyo lakini akakiri kusikia kile alichokiita uvumi huo, kwa watu.

Alisema Mhembano alifika ofisi kwake Novemba 24, mwaka huu saa za jioni akiwa amelewa na kuanza kumtukana, akidai sare kwa nguvu... “Niliamua kuondoka ofisini na kumwacha,” alisema na kuongeza: “Mimi ni mtu mzima, siwezi kumpiga mtu kama yule na hakuna mtu anayeruhusiwa kumpiga mwenzake. Yeye alikuja ofisini kwangu akiwa amelewa chakari na kuanza kunitukana, akidai sare. mimi nikaamua kumkimbia lakini nashangaa anazusha kuwa nilimpiga,” alisema Kitimbo.

Mkurugenzi huyo alisema baada ya tukio hilo, Mhembano alielekezwa na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS), kuandika barua ya maelezo, lakini hajafanya hivyo hadi sasa.
Alipotakiwa kuzungumzia madai ya mkurugenzi huyo kwamba alikwenda ofisini kwake akiwa amelewa, mama huyo alijibu: “Siyo tu siku hiyo, mimi sijawahi kuonja wala kunywa pombe hata siku moja katika maisha yangu.”

MWANANCHI

No comments: