Najua wapo ambao mapenzi yamewaliza sana ndani ya mwaka huu kutokana na kutendewa na wapenzi wao yale ambayo hawakuyatarajia. Hilo halina ubishi na niseme tu kwamba, kama wewe ni mmoja wa wale ambao mapenzi yamewaweka kwenye wakati mgumu sana basi ifike mahali uone kwamba inatosha!
Sema basi kwa mpenzi laghai. Usiwe king’ang’anizi kwa mtu asiyelithamini penzi lako wakati yawezekana yupo mwingine ambaye anatamani kukuona ukiwa singo ili awasilishe hisia zake za kweli kwako.
Lakini zaidi ya yote nataka kusema kwamba, katika maisha yako usiendeshe mambo kibubusabubusa na kwa maana hiyo basi, kabla ya kuingia 2013 lifanyie tathmini penzi lako. Hii ni muhimu sana kwa wale ambao bado hawajaingia kwenye ndoa.
Unataka kujua namna unavyoweza kulitathmini penzi lako? Ni rahisi sana kwani unachotakiwa kufanya ni kujiuliza haya yafuatayo;
Umefaidika na nini mpaka sasa?
Wakati uko singo na baada ya kuanzisha uhusiano naye ni kipi ambacho unaweza kujivunia kwa kuwa naye? Je, umeona faida yoyote? Je, umejikuta ukiwa na amani ndani ya moyo wako na ukanenepa?
Ametimiza ndoto zako?
Huenda ulikuwa ukiota kuwa na mpenzi wa aina flani, je ndiyo huyo uliyenaye? Amekupa ile furaha uliyotarajia? Je, amekudhihirishia kwamba kwenye moyo wake uko wewe peke yako?
Usaliti je?
Kasi ya wapenzi kusalitiana ni kubwa sana. Vipi kwa upande wako? Ulishawahi kumfuma akikusaliti? Je, ulishawahi kupewa hata umbeya tu kwamba mpenzi wako ana mwingine au ulishawahi kujiwa na hisia hizo?
Mna ‘future’?
Huenda mmekuwa kwenye uhusiano wa kawaida kwa muda mrefu sana, je unavyomuangali huyo mpenzi wako ana malengo ya baadaye na wewe? Je, ni mtu anayeonesha kuwa na dhamira ya kuingia kwenye ndoa na wewe?
Hili ni la kuangalia sana, kama unamuona hana ‘future’ na wewe, hata kama anakupa penzi tamu kiasi gani, mruhusu aende wala usikubali kuingia mwaka ujao ukiwa naye. Usiwe mtu wa kukubali penzi la muda ‘temporary love’ eti kwa sababu tu umetokea kumpenda.
Penzi la kweli lipo?
Hapa nazungumzia mambo mengi. Unapoingia kwenye uhusiano na mtu kuna mambo yanayoweza kukufanya ukaamini kuwa mtu huyo ana mapenzi ya kweli na wewe.
Kwa kipindi chote ambacho umekuwa na naye, je umebaini kuwa anakuheshimu, anakupenda, anakujali kwa shida na raha, anakuthamini wewe na ndugu zako?
Hizo ni nguzo muhimu sana kwenye uhusiano kwa hiyo kama umeyabaini hayo, unaweza kujiaminisha kuwa umepata mtu sahihi na unaweza kujivunia kwa kujaaliwa kuwa naye.
Hayo ni baadhi ya mambo ambayo unatakiwa kujiuliza ili uweze kujua kama umeingia kwenye penzi na mtu sahihi au umeingia ‘choo cha kike’.
Ni hayo tu kwa leo, niwatakie kheri ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Chanzo:Global Publishers
No comments:
Post a Comment