Wachimbaji watatu wa madini wamefariki dunia na wengine wawili wamejeruhiwa kwenye machimbo ya madini ya dhahabu baada ya kuangukiwa na udondo kisha kufunikwa mgodini katika kijiji cha Tsawa, Kata ya Gehandu, Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa, alisema watu hao walifariki dunia juzi kwenye eneo la machimbo hayo.
Mpwapwa alisema watu hao walifariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa mchanga wa mgodi huo uliomeguka na kuwafunika wakati wakiwa kwenye shughuli za uchimbaji.
“Wachimbaji wa madini ya dhahabu yaliyogunduliwa mwezi Oktoba mwaka huu walikuwa wanafanya shughuli hizo na wakapata ajali hiyo wakati mvua ilipokuwa inanyesha,” alisema Kamanda Mpwapwa.Alisema wakati mvua ilipokuwa inanyesha, wachimbaji hao walikuwa kwenye machimbo yao na walipoona inazidi kunyesha wakajibanza katika pembe ya kuta za udongo ndipo ghafla udongo huo ukawafunika.
Aliwataka waliofariki dunia kuwa ni Samwel Mpanda (29), mkazi wa Shaurimoyo Babati; Juma Said (34), mkazi wa Rotia katika wilaya ya Karatu mkoani Arusha na John Kiwanko (32), mkazi wa Rotia wilayani Karatu.
Kamanda Mpwapwa aliwataja wachimbaji waliojeruhiwa kuwa ni Paul Marcel (32) na Cosmas Kahindi (30) wanaopatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mbulu ambao hali zao hivi sasa zinaendelea vizuri.
Alisema polisi walifika kwenye eneo la tukio hilo na kufanya uchunguzi. Aliongeza kuwa miili ya marehemu hao imehifadhiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mbulu.
Aidha kufuatia hali tukio hilo, Kamanda Mpwapwa alitoa wito kwa wachimbaji kuhakikisha wanachukua tahadhari pindi wanapokuwa wanafanya shughuli za uchimbaji ili kuepuka ajali zisizo za lazima zinazoweza kutokea.
CHANZO:NIPASHE
No comments:
Post a Comment