Saturday, December 8, 2012

Muhimbili hali ni tete mashine za kufua



Wagonjwa  katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wapo katika hatari ya kuambukizwa magonjwa kutokana na kukosekana  mashine za kisasa za  kufulia na za kukaushia nguo zinazotumika kwenye chumba cha upasuaji pamoja na nguo za wagonjwa walioko mawodini.

Changamoto hiyo ni miongoni mwa zile zilizotajwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji  wa hospitali hiyo, Dk Marina Njelekela mbele ya mke wa Rais Mama  Salma Kikwete,  ambaye ameahidi kuzitafutia ufumbuzi.



Jana Mama Kikwete kupitia Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alitoa msaada wa vitanda 80 katika jitihada za kuboresha huduma hospitalini hapo.

Akizungumzia  changamoto hizo   Dk. Njelekela alisema kukosekana mashine bora ni hali  tete na wakati mwingine husababisha kusimama kwa huduma hizo za ufuaji na ukaushaji nguo za hospitali.

“Kuwepo kwa mashine moja tu ya kuua wadudu kwenye vifaa tiba (sterilizer) kunasababisha kupungua kwa mwendo kasi wa kutoa huduma hapa hospitalini,” alisema.

Akibainisha changamoto nyingine,  hospitali inakabiliwa na tatizo la maji na kulazika kuchimba visima mara kwa mara na kuongeza kuwa kuna baadhi ya maeneo muhimu hayajaunganishwa umeme wa jenereta kwa sababu ya uhaba wa fedha za kununua kifaa hicho.

Alitaja uhaba wa madaktari bingwa, ukosefu kifedha na  msongamano wa wagonjwa .

“Fedha zinazotolewa  kwa ajili ya matumizi ya hospitali zimekuwa zikipunguzwa  kila mwaka kuanzia 2008, wakati mahitaji ya huduma zitolewazo yanaongezeka kila mwaka,” alisema.

Alisema kwa  sasa hospitali  hiyo ina  vitanda 1, 259, wafanyakazi 2,770 na uwezo wa kulaza ni kati ya wagonjwa  1, 000  na  1, 200.

Akizungumzia mafanikio alisema  Muhimbili inatoa huduma bora za kibingwa ambapo takriban wagonjwa 1,200 wa nje hutibiwa kila siku  na kufikia lengo la asilimia 70.
CHANZO: NIPASHE


No comments: