ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 28, 2012

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Ndugu Khatib Mwinchande akabidhi ripoti na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi atembelea makazi ya padri Ambrose kenda

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Ndugu Khatib Mwinchandeakimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ripoti ya Utumishi wa miaka Mitano wa tume hiyo inayomaliza muda wake tarehe 1/1/2013.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wajumbe na Makamishna wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar wanao maliza muda wake tarehe 1/1/2013 wakiongozwa na mwenyekiti wao Nd. Khatib Mwinchande.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akipata maelezo kutoka kwa Uongozi wa Skuli ya Francis Maria Tomondo ambapo Padre Ambrose Mkenda wa Paroko ya Parokia ya Mpendae alijeruhiwa kwa risasi hivi karibuni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia gari ya Paroko wa Parokia ya Mpendae Padre Ambrose Mkenda ambayo alikuwa akiendesha na kuvamiwa kwa risasi ya watu wasiojuilikana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifuatana na Father Shayo wa Kanisa la Roman Katholic liliopo minara miwili baada kuwafariji na kutoa mkono wa pole kwa uongozi wa huo kufuatia kujeruhiwa kwa Paroko wa Parokia ya Mpendae Padre Ambrose Mkenda.


Joto la Uchaguzi miongoni mwa Viongozi wa vyama vya siasa sambamba na wanachama pamoja na wapenzi wa vyama vya siasa litapungua au kuondoka kabisa endapo Tume ya Uchaguzi itaendelea kuwa karibu na washirika wake.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar { ZEC } Ndugu Khatibu Mwinchande alisema hayo wakati yeye na wajumbe wa Tume hiyo walipokuwa wakimuaga rasmi  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakikaribia kumaliza muda wao wa utumishi wa miaka mitano unaomalizika  Januari Mosi 2013.

Ndugu Khatib Mwinchande ambae katika mazungumzo hayo akimkabidhi Balozi Seif  Ripoti kamili ya Utumishi wao wa Miaka Mitano alisema ukaribu wa Tume ya Uchaguzi kwa washirika wake ndio njia pekee ya kuondosha malalamiko au dhana potovu ya wadau hao dhidi ya Tume hiyo.

“ Ni mara ya kwanza katika Historia ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutoa fursa kwa Vyama vya Siasa kupatiwa fursa ya kulikaguwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hii ni ishara kwa Tume hii kuwa karibu na wadau wake ili kupunguza  joto la Uchaguzi”. Alifafanua Ndugu Khatib Mwinchande.

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Nd. Mwinchande alifahamisha kwamba daftari  la wapiga kura litaendelea kuwa la kudumu katika dhana ya kuimarisha Demokrasia licha ya changamoto zilizopo za ukosefu wa fedha kwa ajili ya kuendeleza zoezi hilo.

Alisema harakati za kimaisha zinazoendelea kukuwa kila siku zinachangia kulifanya daftari hilo kuwa la kudumu kutokana na ongezeko la idadi ya watu sambamba na baadhi ya wananchi kuhama sehemu moja kwenda nyengine.

Akizungumzia uhusiano wa Kitaifa na Kimataifa Ndugu Mwinchande alisema Tume ya Uchaguzi Zanzibar imefanikiwa kuoneza ushirikiano wa karibu kati yake na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania { NEC } sambamba na Tume za Kimataifa za Nchi za Sadc na zile za Umoja wa Afrika { AU }.

Alisema hatua hiyo imeijengea uwezo zaidi Tume ya Uchaguzi Zanzibar na kufikia kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Nchi za Kusini na Mashariki mwa Bara la Afrika { Sadc }.

“ Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC } imefikia daraja ya kuwa sehemu ya Tume ya Uchaguzi ya Umoja wa Afrika { AU }”. Alifafanua Mwenyekiti huto wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Nd. Mwinchande.

Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuijengea uwezo Tume hiyo uliosaidia kufanikisha majukumu waliyopangiwa baada ya kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa watendaji wa wizara tofauti  za Serikalini.

Akitoa pongezi zake kwa kazi kubwa iliyotekelezwa na Wajumbe wa Tume hiyo ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC } Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar  imefanya  kura ya maoni iliyopelekea  uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010  kuingia katika  historia mpya ya amani na utulivu.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Uongozi makini wa Tume hiyo kwa kiasi kikubwa  umesaidia kusimamia kupunguza joto la kisiasa ndani ya visiwa vya Zanzibar lililodumu kwa kipindi kirefu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia wajumbe wa Tume hiyo inayomaliza muda wake kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kuona Tume mpya itakayochaguliwa itapatiwa  vitendea kazi pamoja na fedha kwa lengo la kufanikisha kazi za zake.

“  Tutahakikisha changamoto zilizojichomoza ndani ya kipindi cha  utumishi wenu wa miaka mitano, Serikali inazipatia ufumbuzi wa kudumu”. Alisisitiza Balozi Seif.

Wakati huo huo  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika katika makazi ya padri Ambrose Mkenda  wa Paroko wa parokia ya kanisa katoliki la Mpendae Zanzibar kuupa pole uongozi wa Kanisa hilo pamoja na Familia yake kufuatia ajali ya  kupigwa risasi hivi karibuni na watu wasioujulikana.

Tukio hilo la kusikitisha lililofanywa na watu wawili waliopakiana kwenye Vespa lilitokea  langoni mwa Skuli ya Francis Maria iliyopo Tomondo Wilaya ya Magharibi ambapo ndio makaazi ya Padri Ambrose.

 Balozi Seif akiufariji Uongozi huo alisema ni jambo baya na la kusikitisha lililofanywa na watu hao ambalo limetoa sura mbaya  kwa Taifa na Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi itaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo na haitasita kuwachukuliwa hatua za kisheria watu watakaobainika kufanya  uhalifu huo.

Alisema Serikali imesikitishwa na kulaani kitendo cha watu hao ambacho kinaashiria uvunjifu wa amani pamoja na kuwaweka wananachi katika hali ya wasi wasi usio wa lazima ndani ya harakati zao za kimaisha.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi na Familia ya Padre Ambrose Mkenda Kiongozi kutoka  Kanisa la Roman Katholic Father Shayo aliiomba Serikali kuendelea kuimarisha ulinzi wa raia wema ili kupunguza hofu iliyotanda mioyoni mwao kutokana na matukio ya uvamizi.

Father Shayo alitahadharisha kwamba hulka mbaya  iliyoanzishwa na baadhi ya watu kuwafundisha watoto wadogo tabia ya kukashifu watu wazima kwa sababu ya utofauti wa Kidini inawajengea maisha mabovu watoto hao.

“ Watoto wadogo kufundishwa tabia ya kukashifu watu wengine tuelewe kwamba Taifa halitakuwa na muelekeo mwema wa jamii yake ya baadaye”. Alitahadharisha Father Shayo.


Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

27/12/2012.

No comments: