ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 13, 2012

POLISI UINGEREZA WATAFUTA NDUGU WA MWAFRIKA ALIYEANGUKA KUTOKA KWENYE NDEGE LONDON

Picha ya mtu aliyeanguka kutoka kwenye ndege wakati inatua jijini London.

POLISI wa Jiji la London, Uingereza, bado wanahangaika kujua uraia wa mtu mmoja wanayeamini alitoka Afrika na ambaye alianguka na kukutwa amekufa baada ya ndege moja kufungua milango ya magurudumu yake wakati inataka kutua uwanja wa Heathrow mwezi Septemba mwaka huu.
Polisi hao wana picha ya mtu huyo iliyotayarishwa kwa kompyuta.
Vilevile, wachunguzi wanaamini mtu huyo anaweza kuwa alikufa muda mfupi tu baada ya ndege kuondoka ardhini ilikotokea, kutokana na kukosa hewa na kupigwa na ubaridi mkali wakati ndege ikiwa juu, hususani kwa vile alikuwa amejichimbia sehemu yanakoingia magurudumu ya ndege.
Mwanzoni, polisi walifikiri mtu huyo alikuwa ameuawa na watu lakini baadaye walifikia uamuzi kwamba alianguka kutoka kwenye ndege iliyotoka Angola kwani walimkuta na pesa za nchi hiyo ya Afrika na kwamba muda mfupi baadaye walipata habari kuna ndege ilikuwa inatua uwanjani Heathrow.
Tatizo kuu la polisi ni kutaka kufahamu ndugu wa mtu huyo mwanamme ili wawape mwili wake iwapo watamfahamu na kuwa tayari kumchukua. Mtu huyo aliyekutwa na polisi hapo Septemba 9 ni mwenye mwili wa kadiri anaaminika kuwa na umri wa miaka kati ya 20 na 30 na alikuwa amevaa suruali ya ‘jeans’, raba nyeupe na sweta ya kijivu.
Wakazi wa eneo aliloangukia walitoa ushahidi wa kuiona ndege ya Angola ikipita juu ya anga lao na polisi wanaamini alikuwa mmoja wa wazamiaji wa Afrika wenye kutafuta maisha Ulaya.
(CHANZO: NDTV)

No comments: