ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 13, 2012

Wabunge Chadema kukamatwa


  *Ni maamuzi ya Kamati ya Ulinzi
 *Mmoja asema anasubiri kwa hamu
    Highness Kiwia   na  Ezekiah Wenje
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, imeliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata wabunge wa Nyamagana na Ilemela wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Baraka Konisaga, alitoa amri hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Konisaga alisema kamati yake imemuagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ilemela (OCD) kuhakikisha anawakamata wabunge hao wa Ilemela, Highness Kiwia na wa Nyamagana, Ezekiah Wenje na kuwahoji kwa tuhuma za kutamka maneno yenye lengo la uvunjifu wa amani, fujo na athari zingine  jijini Mwanza.
Alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nyamagana ilifikia uamzi huo jana baada  ya kukutana, kujadili na kubaini kwamba kauli  zilizotolewa na wabunge hao kwa nyakati tofauti, Novemba na Desemba mwaka huu zinalenga  kuvunja amani.

“Tumemwagiza OCD awapate na kuwahoji wabunge hao kuhusu matamshi yao,” alisema Konisaga baada ya kuulizwa na NIPASHE juu ya hatua  zinazochukuliwa na ofisi yake dhidi ya wabunge hao.

“Baada ya kupata taarifa ya kina, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya  ya Nyamagana kupitia kikao chake cha tarehe 12/12/2012, imejiridhisha maneno  yaliyosemwa na waheshimiwa Wabunge, Wenje na Highness Kiwia ni ya upotoshaji na yanalenga  kusababisha uvunjifu wa amani, fujo na athari  kubwa katika jamii ya Jiji letu la Mwanza,”  aliongeza.

Hatua hiyo ya kamati hiyo imechukuliwa zikiwa zimepita takribani siku tatu tangu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe,  kufanya mkutano na waandishi wa habari  na kudai  kuwa tuhuma zinazotolewa na wabunge hao hazina  ukweli wowote na zinalenga kumchafulia jina ndani ya jamii.

Hata hivyo, Konisaga, aliwataka wakazi wa Jiji la Mwanza  kupuuza maneno ya uchochezi   yanayodaiwa kutolewa na  wabunge hao kwa lengo la kushinikiza Kabwe aondolewe jijini hapo.

Pamoja na mambo mengine, alisema kikao cha kamati hiyo kilibaini kuwa Mkurugenzi huyo hajafanya kosa na kwamba ametekeleza na  anaendelea kutekeleza sheria, taratibu, miongozo  ya serikali, na maazimio ya vikao halali  vya Halmashauri ya Jiji la Mwanza  hususani kikao cha Septemba 27, mwaka huu.

Alisema wajumbe wa kikao hicho ambacho Wenje  na  Kiwia walihudhuria, waliamua juu ya mgawanyo  wa mali kati ya Halmashauri hiyo na Manispaa  ya Ilemela kabla hazijagawanya rasmi.

Alisema Kabwe bado anatekeleza mambo ambayo  yaliamuriwa kwenye kikao hicho ambacho  aliyekuwa Naibu Meya  wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza  (kabla ya kugawanywa  kwa Halmashauri hizo), Charles Chinchibela (Chadema) ndiye  aliyekuwa mwenyekiti  wake.

Alisema zabuni  na miradi yote ya maendeleo  iliyomo eneo la Manispaa  ya Ilemela itaendelea  kutekelezwa chini ya ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji hilo kwa sababu ndiye alifunga mikataba kabla  Manispaa  hiyo haijaanza  kujitegemea.

“Sasa sijui ni kwa nini  wabunge hawa wanaeneza maneno ya uongo mbele ya jamii huku wakijua kwamba yanayofanywa na Kabwe yanatokana na  maamuzi yao. Halafu ni kwa nini wasimsakame hata  aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao hicho (Chinchibela)  ambaye  ni mwana-Chadema mwezao?”  alihoji  Konisaga.

Alisema Serikali ya Wilaya ya Nyamagana haiko  tayari  kuruhusu  maandamano ambayo  yanachochewa na kauli  zilizotolewa  na wabunge hao (Wenje katika viwanja  Sahara Septemba 28 mwaka huu  na Kiwia Desemba 5 mwaka huu katika  uwanja wa Furahisha ).

Kwa upande wake, Kiwia  alisema  yuko tayari  kujipeleka  kituo chochote cha Polisi iwapo  atahitajika.

“Mimi nipo jijini Dar es  Salaam. Lakini kwa kifupi ni kwamba  hata saa nane nikihitajika nitakuwa tayari kujipeleka Polisi kusisitiza kwamba sikubaliani na  maneno ya Kabwe wala Mkuu  huyo  wa Wilaya  ya Nyamagana,”  alisema  kwa njia ya simu, jana.

Alikiri kwamba alihudhuria  Baraza la Madiwani   Septemba 27, mwaka huu  na kwamba hakuunga mkono maamuzi yaliyofikiwa na wajumbe   wenzake juu ya mgawanyo wa mali baina ya Halmashauri hizo mbili.

Alisema baada ya kikao hicho alitoa malalamiko yake kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati  wa wiki ya mwisho  ya  mkutano wa Bunge uliopita na kwamba hadi sasa hakuna majibu yoyote yaliyotolewa na Pinda.

Hata hivyo, Wenje hakupatikana ofisini kwake wala  kwa njia ya simu yake ya mkononi ili aweze  kuzungumzia   suala  hilo.

Simu yake iliita bila  kupokelewa na hakujibu ujumbe mfupi (sms).

Desemba 10, mwaka huu, Kabwe, aliwaambia waandishi wa habari kwamba madai ya wabunge hao hayana ukweli wowote huku akiviomba vyombo vya dola vichukue hatua dhidi yao kwa madai kuwa wanamchafua.

Wakati huo huo, Mahakama ya Rufani jana ilitupilia mbali rufani ya kupinga kubatilisha matokeo ya ubunge wa Jimbo la Ilemela, baada ya kutamka kuwa waliofungua rufani hiyo dhidi ya Kiwia hoja zao hazikuwa na mashiko ya kisheria.

Baada ya uamuzi huo, Kiwia alisema kuwa anaishukuru mahakama kwa kumtendea haki, lakini alisema kuwa waliofungua rufani hiyo walimpotezea muda wake wa kuwatumikia wananchi badala yake kuhudhuria mahakamani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: