ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 28, 2012

Polisi waendelea kuua raia


Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma ,linawashikilia askari wawili wa kituo chake cha Wilaya ya Kasulu kwa tuhuma za kumtesa ,kumpiga kipigo na kumuua raia, Gaspa Musa, kwa tuhuma za kumdai deni la Sh. 50,000 za mbao 20 alizokopa.

Askari hao wanadaiwa kumpiga kichwani, tumboni na kwenye kifua kwa kutumia mateke na mti wa mwanzi akiwa uchi wa nyama.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo katika Kijiji cha Heru Ushingo Wilaya ya Kasulu Desemba 25, mwaka huu saa tano usiku.

“Askari wote wawili tunawashikiria na tunafanya uchunguzi juu yao waliyohusika na tuhuma za mauaji, ikibainika watafukuzwa kazi na kupelekwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake,”alisisitiza kamanda Kashai.

Askari hao ni D.8622 CPL Peter Mrimba na G. 1236 PC Sande Simon.
Kaka wa marehemu, Yohana Musa (55), alisema:

“Mimi nilikuwa nyumbani watu wakaja wakaniambia kuwa mdogo wako Gaspa Musa anapigwa na askari polisi Peter na Sande katika baa ya Peter hadi amezimia na amepelekwa mahabusu. Nilipofika katika kituo kidogo cha polisi nilikuta polisi wameshapeleka mwili wa mdogo wangu katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu.”
Aliongeza: “Ninavyojua mdogo wangu alikuwa anamdai askari Peter Shilingi 50,000 za mbao 20 alizokuwa amekopa, nashangaa kuona askari huyo anadaiwa tena anaanza kumpiga mdogo wangu hadi kufa.”

Daktari aliyechunguza mwili wa marehemu, Dk. Jonathani Bujiji, alisema Gaspa alifariki kutokana na kipigo kilichosababisha kupasuka kwa bandama, michubuko usoni iliyosababisha kuvuja damu nyingi na jeraha kubwa sehemu ya kichwa.

Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agripina Buyogera alisema alipigiwa simu na wapiga kura wake kuwa kuna askari polisi wa kituo kidogo cha kiijiji cha Heru Ushingo wamempiga Gaspa na kumuua, na kwamba baadaye alikwenda katika kituo hicho.

Alisema aliingia mahabusu ya kituo hicho na kukuta damu na kinyesi na baada ya kuona hivyo alikwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu na kukuta mwili wa marehemu umetapakaa kinyesi pamoja na jeraha kichwani.

Shuhuda wa tukio hilo, Idd Juma, alisema siku ya Krismas marehemu alikwenda katika baa ya mtuhumiwa Peter kudai fedha zake naalipofika aliagiza pombe za Sh. 5,000 na baada ya kumaliza kunywa akamwambia Peter fedha za bia zikatwe katika deni ndipo askari huyo aliamua kumpa kichapo.

CHANZO: NIPASHE

No comments: