Kamanda Mangu amesema kuwa hana taarifa zozote kama Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nyamagana mkoani hapa imeliagiza Jeshi la Polisi kumkamata mbunge huyo na kuongeza kwamba ofisi yake haiwezi kufanyia kazi maagizo yanayotolewa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Kamanda Mangu alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na NIPASHE kwa njia ya simu. NIPASHE lilitaka ufafanuzi kutoka kwa Kamanda Mangu kama Wenje ameshakamatwa au la ukiwa ni utekelezaji wa agizo lililotolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga.
“Sina taarifa, hata hivyo, mimi sifanyii kazi kwa maelekezo ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya; isipokuwa ninafanya kazi kwa maelekezo ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa,” alisema Kamanda Mangu.
Hata hivyo, Kamanda Mangu hakusema iwapo alimeshapokea taarifa zozote juu ya agizo hilo kutoka kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Nyamagana, Ally Kitumbu, ambaye kwa mujibu wa Konisaga, aliagizwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama kwamba anatakiwa amtie nguvuni na kumhoji Wenje.
Juzi Konisaga alisema Wenje anapaswa kukamatwa kwa kuwa amekuwa wakitoa kauli za uchochezi na upotoshaji kuhusiana na mgawanyo wa vyanzo vya Halmashauri za Manispaa za Nyamagana na Manispaa ya Ilemela, ambazo zilimegwa kutoka katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Aidha, Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia anatuhumiwa kwa kutoa kauli hizo, lakini Konisaga hana mamlaka ya kuamuru akamatwe kwa kuwa DC Konisaga siyo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela.
Jana Wenje hakupatikana ofisini kwake kuzungumzia agizo la Konisaga na hata alipitafutwa kwa simu iliita bila majibu.
Katibu Muhtasi wake aliliambia NIPASHE ofisini kwake jana mchana kwamba mbunge huyo yuko jijini Dae es Salaam kikazi.
Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Tito Mahinya, alikataa kutoa ufafanuzi kuhusu ni kiasi gani cha fedha (asilimia 40) ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kabla ya kuanzishwa kwa Manispaa ya Ilemela.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe, aliwaambia waandishi wa habari kuwa fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti ya Manispaa ya Ilemela, Desemba 10, mwaka huu.
Mahinya alidai kuwa hawezi kutoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari kwa sababu hiyo ni siri ya ofisi.
Hata hivyo, alitupilia mbali ombi la NIPASHE la kutaka kuonyeshwa maazimio ya kikao cha Baraza la Madiwani na wabunge wa Ilemela na Nyamagana wakiwamo.
Hata hivyo, Kabwe aaliwaambia wandishi wa habari kuwa Baraza liliketi Septemba 27, mwaka huu na kuridhia utaratibu utakaotumika kuhusu mgawanyo wa mali mara baada ya kuanzishwa kwa Manispaa ya Ilemela.
Aliendelea kusisitiza kuwa wabunge wote wawili, Kiwia na Wenje walikuwapo katika Baraza hilo na kuongeza kuwa yaraka hizo ni taarifa za ndani za Halmashauuri ya Jiji la Mwanza ambazo hazitakiwi kuitolewa kwa vyombo vya habari.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Ilemela, Matata, alisema mgawanyo wa asilimia 40 ya fedha zinazotakiwa kutumwa kwenye akaunti ya Manispaa ya Ilemela ni kutokana na fedha zilizokuwamo kwenye akaunti ya Jiji la Mwanza wakati Manispaa hiyo inaanza kujitegemea.
“Sina hakika kama Halmashauri ya Jiji la Mwanza imeshatuma fedha katika akaunti ya Manispaa ya Ilemela. Lakini pia siyo kweli kwamba Ilemela itaendelea kupokea asilimia 40 kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza eti kutokana na vyanzo vya mapato,” alisema Matata wakati akizungumza na gazeti hili.
Alisema baada ya kufunguliwa rasmi kwa kupata mgawo wa watendaji pamoja na uongozi wa madiwani, Manispaa ya Ilemela inatakiwa ianze kukusanya mapato kutokana na vyanzo vilivyomo ndani ya wilaya hiyo, na siyo vinginevyo.
“Hatuwezi kuendelea kupokea asilimia 40. Kwa sababu mikataba iliyofungwa wakati wa nyuma inaweza kuhamishwa kisheria na sisi kama Manispaa tukakusanya mapato katika vyanzo vya mapato vilivyomo kwenye ardhi yetu kama kawaida.” alisema.
Alisema hata miradi ya maendeleo iliyomo kwenye ardhi ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela inatakiwa ikabidhiwe katika Manispaa ya Ilemela.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment