Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa (wa pili kushoto) akijumuika pamoja na Baadhi ya Wabunge wanaounda timu ya Bunge Sports inayoundwa na wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi na Bunge la Jamhuri,wakati wa Chakula cha Mchana alichowaandalia Nyumbani kwake,Ngarashi Wilayani Monduli jana.Wengine pichani kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Habari,Vijana Utamaduni na Michezo,Mh. Amos Makalla,Mbunge wa Jimbo la Kinondoni,Mh. Iddi Azzan pamoja na Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Monduli, Reuben ole Kunai.
Wabunge wanaounda timu ya Bunge Sports inayoundwa na wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi na Bunge la Jamhuri wakipata Chakula cha Mchana kilichoandaliwa na Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa Nyumbani kwake,Ngarashi Wilayani Monduli jana.Mh. Lowassa alikutana na Wabunge hao ili kujadili maswala mbali mbali yahusuyo Michezo hapa nchin,wakati timu hiyo ikiwa Kambini jijini Arusha,kujiandaa kwenye Jijini Nairobi kwenye Mashindano ya Afrika Mashariki.
WAZIRI Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Monduli Mh. Edward Lowassa amewashauri wabunge wa timu ya Bunge Sports kufikiri juu ya kutunga sera ya michezo itakayoruhusu kuanzishwa kwa Shule za Michezo (Sports Academy) hapa nchini.
Lowassa ameyasema hayo jana,baada ya kuialika nyumbani kwake timu hiyo iliyopiga kambi ya jijini Arusha tayari kwa mashindano ya Mabunge ya Afrika Mashariki jijini Nairobi.
“Nilisikitika kweli Timu ya Taifa ya Kilimanjaro Stars ilipofungwa na Burundi kwenye mchezo wa pili wa Mashindano ya CECAFA huni Uganda, pamoja na juhudi za Rais Jakaya Kikwete kuleta makocha bado tumefungwa na Burundi iliyotoka kwenye vita juzi!.
“Nyinyi ni watunga Sera, ni wachezaji mnajua changamoto zinazofanya tusifike juu, umefika wakati wa kuwa na Shule za Michezo zinazotambuliwa na Sera zetu.
“Mpira ni chakula cha Watanzania, wanapenda mpira sana. Napendekeza baada ya kurejea anzeni kufikiria juu ya kutunga Sera ya kuwa na Shule za Michezo. Kipingu amejitahidi kuwa na kitu kama hiki lakini amebakia peke yake hakuna anayemuunga mkono,” alisema Lowassa.
Alisema kuwapo kwa Timu ya Bunge Sports kutasaidia kufikiria juu ya mafanikio ya mchezo wa mpira wa miguu, pete na michezo mingine.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo,Mh. Amos Makalla aliyeongozana na timu hiyo alimwambia Mh. Lowassa kwamba serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Sera za michezo.
“Sera na sheria za sasa za michezo kweli haziendani kabisa na wakat,zote ni za zamani. Serikali imejipanga kuzifanyia kazi.
“Changamoto uliyoitoa ya kuanzisha Shule za Michezo na kuendeleza michezo nchini tunaipokea na tutaifanyia kazi.
“Nilipoteuliwa kuwa Naibu Waziri kwenye Wizara hii niliwaambia watu na binafsi namshukuru Rais Kikwete, kwamba upele ulipata mkunaji kwani mimi ni mwanamichezo na uwanjani ni kiungo mchezeshaji,” alisema Makala.
Naye Mwenyekiti wa Timu hiyo ya Bunge Sports inayoundwa na wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi na Bunge la Jamhuri, Iddi Azan alimshukuru Mh. Lowassa kwa mawazo yake na kuahidi kuyafanyia kazi.
“Kwanza tunaahidi ushindi kwa nchi, Bunge letu na haya uliyoyasema tunaahidi kuendelea kuyafanyia kazi kwani tunatambua sheria na Sera za michezo zimepitwa na wakati,” alisema Azan.
Timu hiyo ya Bunge Sports ilikuwa na wachezaji wake wote waliopo kwenye kambi jijini Arusha wanaounda timu ya Mpira wa miguu na Pete.
No comments:
Post a Comment