Magila kuna mlima ulio katika safu za milima ya Usambara ukipakana na mlima wa Magoroto ambao ndio chanzo cha maji ya mto Mkurumuzi unaoelekea Muheza.
Historia inaonyesha eneo la mlima Magila wenye miamba na mawe mengi, zamani kabla ya kuja wageni lilitumika kuwatenga wagonjwa wa ukoma na magonjwa mengine yasiyotibika, kwa lengo la kuwazuia wasiwaambukize wengine.
Dk Krapf alipofika na kuwaona wagonjwa hao waliokuwa wakiishi kwa madhila makubwa, alichonga msalaba katika mti wa mkuyu kwa imani kuwa Mwenyezi Mungu angewaponya wagonjwa hao.
Eneo hilo ndilo lililokuja kujengwa shule ya kwanza na Waingereza mwaka 1886. Alama ya msalaba huo ipo hadi na sasa na ndipo ilipo Shule ya Sekondari Hegongo.
Hadi leo mahali hapo panaitwa Magila Msalabani. Kwa sasa Magila ni kata yenye vijiji vya vya Magila, Mikwamba, Misongeni na Mafleta.
Nilifika katika eneo hilo nilipokuwa wilayani Muheza hivi karibuni ili kuchunguza historia ya eneo hilo.
Hapo nikutana na Luteni Kanali mstaafu John Mhina ambaye amekamilisha kuandika kitabu kuhusu historia ya Magila Msalabani, kinachoeleza historia ya kijiji hicho na ujio wa wazungu walioanzisha shule ya kwanza Tanganyika na kanisa.
Luteni Kanali Mhina aliyelitumikia Taifa kwa muda mrefu kama mwanajeshi , na baadaye kuwa Mbunge wa Muheza kutoka mwaka 1990 hadi 1995, anasema harakati za kuanzisha shule katika kijiji hicho zilitokana na Wamishenari waliokuja Afrika Mashariki kutoka Ulaya kwaajili ya kueneza dini ya kikristo tangu miaka ya 1770.
Anawataja baadhi ya Wamishenari hao kuwa ni pamoja na David Livingstone, Charles Mackenzie, William Tozer na Edward Steer.
Anasema harakati hizo zilianzia tangu visiwa vya Zanzibar mwaka 1863 ambako pia walikomesha biashara ya utumwa na kuanza ujenzi wa kanisa la Anglikana la Mkunazini Zanzibar kwa miaka 10 tangu mwaka 1873.
Anasema wakati huo kulikuwa na shule iliyoanzishwa Zanzibar maeneo ya Kiungani na Kiinua mguu na Askofu William Tozer mwaka 1869. Hata hivyo, anasema shule hiyo haikuwa rasmi na ilikuwa ikifundisha elimu ya dini kwa watumwa waliokombolewa.
Uamuzi wa kujenga shule Bara
“Mnamo Agosti 13, 1967 Askofu Tozer alimtuma Padri CA Alington aende Vuga (Lushoto) kwa Chifu Kimweri ili apate kibali cha kujenga kituo cha misheni kwenye maeneo ya Bara,’’anasimulia Luteni Kanali Mhina na kuongeza:
“ Padri Alington alimchukua Vincent Mkono aliyekuwa mwanafunzi wake wa Kiungani na mwingine Mwinyi Khatib aliyekuwa mkalimali. Msafara huo ulipata baraka za Sultan Majid aliyekuwa akitawala Zanzibar.”
Anaeleza kuwa baada ya msafara wao kufika Vuga, Chifu Kimweri aliwasikiliza, lakini akaomba apewe muda wa kutafakari kwanza.
Baadaye Januari 20, 1868, Padri Alington alirudi Vuga na kuruhusiwa na Chifu Kimweri kujenga sehemu yoyote katika maeneo ya Pwani.
Anasema Padri Alington aliamua kuchagua eneo la Magila ambalo lilikwishajulikana kutokana na alama ya msalaba uliowekwa na Dk Krapf.
“ Jumbe Kifungiwe aliyekuwa akiongoza Magila wakati huo chini ya baraza la ‘wamaka’ (Baraza la Wazee wa Kibondei), walimpa mlima wote wa Magila wakidhani kuwa atashindwa kujenga kwa sababu ya kuwa na mawe mengi….kwa mshangao aliporudi aliyatumia mawe hayo kujengea.” anaeleza.
Anasema pamoja na kazi ya kueneza dini Wamishenari hao walijipa jukumu la kuwatunza wagonjwa wa ukoma na kuanzisha shule.
“Shule ya sokoni ilikuwa kwanza kujengwa maeneo hayo mwezi Aprili 1869 chini ya Padri Fraser na wanafunzi wake walikuwa ni pamoja na Jumbe Kifungiwe na ndugu yake Sagosago na vijana wengine. Palikuwa na soko dogo na mti mkubwa wa Mzindanguuwe, watu wazima walipenda kukaa hapo ili walione jambo hilo geni,” anaongeza kusema.
Sekondari ya Hegongo
Hivi sasa eneo hilo kuna shule iitwayo Hegongo. Mkuu wa shule hiyo, Wilfred Mdimu anasisitiza kuwa eneo hilo ndipo palipojengwa shule ya kwanza Tanzania ambapo mpaka sasa kuna mabaki ya darasa la kwanza lililojengwa na Wamisheni.
Hivi sasa anasema darasa hilo linatumiwa kama ofisi ya walimu wa shule ya sekondari ya kata Magila.
“Hili ndilo darasa la kwanza lililojengwa mwaka 1869 na Waingereza. Awali lilikuwa ghorofa lakini likabadilishwa. Inasemekana shule nyingine ilijengwa Bagamoyo na baadaye Minaki,” anasema Mdimu na kuongeza,
“Walijenga pia kanisa baada ya lile la Mkunazini Zanzibar. Lakini lilipochakaa ndipo wakajenga kanisa jingine mwaka 1886 kama lile la Mkunazini na ndiyo linatumika hadi sasa.”
Akizungumzia uchaguzi wa eneo hilo, Mdimu anasema awali wazungu walitaka kujenga shule maeneo ya Muhenza Mkumbi na Mkanyageni, lakini wakaathiriwa na malaria, ndipo wakahamia katika mlima wa Magila.
Kuhusu shule hiyo, Mdimu anasema kuwa awali ililenga kuwaandaa Waafrika ili wawasaidie wamisheni katika kazi zao. Waliwafundisha kusoma, kuandika na kuhesabu.
Baadaye elimu ikapanuka baada ya shule za St. Marys na St Martin kujengwa zikiongeza masomo na wanafunzi.
Anaongeza kuwa shule hizo hazikudumu muda mrefu, bali zilibadilishwa na kuwa Sekondari ya wasichana ambayo nayo ilikuja kuhamishiwa wilayani Korogwe ilipo shule ya wasichana maarufu kwa jina la Korogwe girls.
Baada ya kuhamisha shule hiyo, matumizi yakabadilishwa na kikaanzisha chuo cha ualimu kwa wanawake tu. Hata hivyo, anasema chuo hicho nacho kilihamishiwa tena Korogwe kilipo chuo cha ualimu hadi leo.
“ Mwaka 1974 hadi 75, majengo hayo yakafanywa kuwa mahali pa kujifungulia wanawake na ndipo ilipoanzia hospitali teule ya Muheza. Lakini ikahamishiwa eneo ilipo sasa na majengo haya yakabaki matupu,” anasema Mdimu.
Kuanzishwa kwa Hegongo sekondari
Mwalimu Mdimu anasema baada ya majengo kubaki matupu, mwaka 1976 wenyeji wa Magila walimwomba Askofu wa kanisa hilo dayosisi ya kaskazini John Ramadhani, ili waanzishe shule ya sekondari hasa kwenye majengo ulipo msalaba wa Dk Krapf, naye akawakubalia.
“Februari 24, 1977 shule ya Hegongo ilianzishwa ikiwa chini ya wenyeji wa Magila ili kuwapa elimu watoto wa wilaya hiyo,” anasema.
Hata hivyo anasema shule hiyo haikuwa na maendeleo mazuri kwa muda mrefu. Isitoshe, wasimamizi wa shule hiyo walishindwa kuiendesha kutokana na madeni makubwa ya umeme, mishahara ya watumishi na mafao yao.
Hegongo ya sasa
Anasema hadi mwaka 2000 wasimamizi wa shule hii walishindwa kabisa kuiendesha wakairudisha kwa kanisa.
“Tangu wakati huo uongozi wa kanisa umeamua kuiendesha kwa kwa kulipa madeni makubwa yaliyokuwepo na kuimarisha hali ya elimu,” anasema na kuongeza:
“Kwa sasa tunaboresha majengo, tumejenga maabara, maktaba ya kisasa na tutaongeza nyingine. Askofu wa sasa ameamua kuwachukua mapadri 10 waliomaliza kidato cha sita na kuwapeleka vyuo vikuu ili wasomee ualimu kwa ajili ya shule hii.’’
Kwa upande mwingine, majengo ya zilizokuwa shule za St. Mary’s na St. Martin sasa zimechukuliwa na Serikali, huku mojawapo ikitumika kama shule ya sekondari ya kata ya Magila na nyingine kama shule ya msingi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment