ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 28, 2012

TAARIFA KUTOKA KWA MBUNGE WA JIMBO LA UBUNGO, JOHN MNYIKA

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika (Mb)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nakusudia kutumia kifungu cha 10 cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kutaka nakala ya mkataba wa mkopo wa masharti kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.225 (shilingi trilioni 1.86) kutoka China.

Nitataka pia nakala za mikataba wa mradi wa miundombinu ya gesi asilia ambayo itahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ujenzi wa bomba kuu la kusafirishia gesi asilia la inchi 36 kutoka Mtwara kupitia Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam lenye umbali wa kilometa 532.

Hii ni kwa sababu mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini haijatekeleza pendekezo nililowasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwamba kutokana na unyeti wa mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha ya wananchi wa sasa na baadaye Serikali ilipaswa kuwasilisha bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika.

Pendekezo hilo lingeliwezesha Bunge kuishauri na kuisimamia serikali kuanzia katika hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya taifa yanalindwa katika hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za uwekezaji huo mkubwa.
Kutokana na Serikali kutokuzingatia pendekezo hilo na badala yake Rais Jakaya Kikwete kufanya uzinduzi wa mradi huo tarehe 8 Novemba 2012 Mkoani Dar es salaam huku usiri ukiendelezwa malalamiko yameanza kujitokeza katika maeneo ya mradi husika hususan katika Mkoa wa Mtwara.

Aidha, Serikali irejee katika mapendekezo niliyotoa bungeni na kutoa maelezo kwa umma ya sababu za bomba hilo kujengwa kutoka Mtwara mpaka Dar es salaam na kueleza kwa uwazi manufaa ya mradi huo na miradi mingine inayopaswa kutekelezwa katika mikoa ya Kusini kwa maendeleo ya wananchi husika.

Tarehe 27 Julai 2012 nilieleza bungeni kuwa pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi huo; Serikali inapaswa kueleza ni miradi ipi inayoambatana na mradi huo ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwemo kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa MW 300 Mtwara na MW 230 wa Somanga Fungu (Kilwa).

Kwa upande mwingine, utekelezaji wa mradi huo unaendelea bila kuwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ingepaswa kuishauri na kuisimamia Serikali hivyo ni muhimu Spika wa Bunge akachukua hatua kutokana na barua niliyomwandikia mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2012 ambayo mpaka sasa haijajibiwa.

Ikumbukwe kwamba katika barua hiyo nilitoa mwito kwa Spika atumie madaraka na mamlaka yake kutangaza kwa umma kamati nyingine ya kudumu ya Bunge itayoshughulikia nishati na madini ikiwemo masuala ya gesi asili kwa sasa kufuatia hali tete na tata kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.

Pamoja na mambo mengine nilipendekeza Spika aelekeze kamati hiyo kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu Sekta Ndogo ya Gesi Asili ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika kushughulikia tuhuma za ufisadi, madai ya mapunjo ya fedha za mauzo ya Gesi asili na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango mkakati na sheria ya gesi asili.

Hatua hii ni muhimu kwa sasa kwa kuwa hata baada ya uamuzi wake kuhusu tuhuma za rushwa kwa wajumbe wa Kamati husika, Spika hakueleza hatma ya Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa hali ambayo imeacha ombwe la uongozi na usimamizi wa kibunge (Parliamentary Oversight) kwenye sekta hizi nyeti kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
26/12/2012

No comments: