ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 26, 2012

Tanesco yatangaza suluhisho kukatika umeme

MAKAO MAKUU YA SHIRIKA LA UMEME LILILOPO MAENEO YA UBUNGO

Kufuatia adha ya kukatikakatika kwa umeme inayoendelea hivi sasa katika maeneo mengi nchini, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza mikakati kabambe ya kukabiliana na adha hiyo kuanzia Januari, mwaka ujao.

Mikakati hiyo iliwekwa bayana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Fulchesm Mramba, wakati akizungumza na waandishi wa habari juzi, jijini Dar es Salaam.“Kwanza nianze kwa kusema kwamba, hali ya umeme nchini imeimarika sana kulinganisha na siku za nyuma. Bado yapo matatizo ya hapa na pale ya kukatika umeme katika baadhi ya maeneo nchini na shirika linachukua hatua mwafaka kukabiliana na hali hiyo,” alisema Mramba.

Alisema matatizo ya kukatikakatika kwa umeme yanayoendelea hivi sasa nchini si mgawo wa umeme wa kimyakimya kama inavyodaiwa na baadhi ya Watanzania bali ni kutokana na matatizo ya kiufundi.

Aliyataja baadhi ya matatzio hayo kuwa ni pamoja na mifumo ya umeme kuzidiwa nguvu, hujuma, uharibifu wa miundombinu, urefu wa laini ya umeme, huku ikisambaza nishati hiyo katika eneo kubwa pamoja na lile la kuchoka kwa nguzo za umeme.

Baadhi ya mikakati iliyowekwa na Tanesco katika kukabiliana na matatizo hayo ni pamoja na kuanzishwa kwa miradi mikubwa ya TEDAP, ambao utahusisha kufanya matengenezo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro, huku ule wa MCC ukihusisha mikoa ya Tanga, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Iringa.

Miradi mingine ni ule wa Ecectricity utakaohusika na mikoa ya Shinyanga (Maswa Bariadi), Mwanza, Geita, Dar es Salaam (Jangwani, Vingunguti, Gongo la Mboto, Pugu na Kisarawe, Kurasini, Mbagala, Kigamboni Mkuranga), Arusha na ule wa DSM City Center Substation.

Aliitaja mingine kuwa ni mradi maalum wa Kusini, ambao unahusisha mikoa ya Lindi katika vijiji zaidi ya 24 na Mtwara vijiji 28 na ule wa SCADA.

CHANZO: NIPASHE

No comments: