Saturday, December 8, 2012

TFF:Ngassa mali ya Azam kisheria

Shirikisho la soka, TFF , limesema winga Mrisho Ngassa ambaye mauzo yake kwa klabu ya El Mereikh ya Sudan yamezua mvutano wa timu mbili nchini ni mali ya Azam na si Simba ambayo alikuwa akiichezea kwa mkopo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, katibu mkuu wa TFF Angetile Osiah alisema shirikisho hilo limepokea barua nne ndani ya siku mbili kutoka kwa Simba na Azam kila moja ikidai Ngassa ni mchezaji wake halali.


Lakini, nyaraka za usajili zilizopo TFF, alisema Osiah, zinaelezea kuwa Ngasa ni mchezaji halali wa Azam aliyesajiliwa mwaka 2010 na amekwenda Simba kwa mkataba wa mkopo kwa makubaliano ya malipo ya sh. milioni 25.

Alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni za usajili wa mkopo, mchezaji anapotolewa kwa mkopo kwenda timu nyingine, klabu yenye haki na mchezaji huyo ni ile aliyoingia nayo mkataba na sio aliyokwenda kuichezea kwa mkopo huo.

"Mchezaji aliyetolewa mkopo timu (mama) yake inaweza kumrudisha siku yoyote baada ya kupita siku 28," alisema Osiah na kueleza zaidi, "hiyo yote ni kwa sababu wao ndio wenye haki na mchezaji huyo."

Simba na Azam FC zimeingia kwenye mvutano baada ya klabu ya wauza nafaka hao wa jijini kumuuza Ngasa El Merreikh kwa dau la dola za Marekani 75,000 (sh.milioni 120).

Simba inapinga hatua hiyo ya Azam kwa madai kuwa mchezaji huyo ni mali yake baada ya kumnunua kwa mkopo na kisha kumpa mkataba wa miaka miwili juu ya makubaliano ya mkopo hayo.
"Barua zimekuja hapa juzi na jana (Desemba 5 na Desemba 6) kila upande ukielezea yake juu ya mchezaji huyu," alisema Osiah.

Aidha, pamoja na Simba kuomba TFF kuzuia kutoa ITC ya mchezaji huyo, Osiah alisema kuwa suala la kutoa ITC si la shirikisho lake bali mchakato ambao hufanywa na kwa njia ya mtandano kwa kushirikisha klabu mbili husika huku zikifuatiliwa na shirikisho la soka barani Afrika, CAF.

"TFF haihusiki kutoa ITC," alisema Osiah.

"Hayo mambo yanafanywa na klabu inayotaka kumuuza mchezaji na ile inayotaka kumnunua na wanafanya kwa njia ya mtandao na wanapaokubaliana na mashirikisho ya soka ya nchi mbili ndipo timu hizo zinaombana ITC.
"Hivyo hili suala si la TFF."
SOURCE: NIPASHE

No comments: