Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Sylvester Mhoja Kasulumbayi (62), akitoa maoni yake juu ya uundwaji wa katiba mpya katika mkutano uliofanyika kwenye kata ya Ipililo iliyopo wilayani Maswa jana. Picha na Fredy Azzah
MKAZI wa Kata ya Nkoma, Lazaro Daudi, amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uendelee kwani ukivunjika Zanzibar itaweza kuishambulia Tanganyika.
Alisema kuwa, kuungana kwa nchi mbili hizi kunasaidia kudumisha amani na utulivu hivyo suala hilo lidumishwe.
“Tukijitenga na Zanzibar tutaisha, watakuwa wanaingia kwenye maji na kutokea bandarini hatimaye warushwe mabomu,” alisema.
Alisema ili kuipunguzia Serikali gharama endapo rais, mbunge au diwani akifariki, mtu aliyeshika nafasi ya pili kwenye uchaguzi wa ndani achukue nafasi yake.
Naye Kato Kiumbani (70), mkazi wa eneo hilo alitaka waruhusiwe kuachana na zao la pamba kwa kuwa Serikali hailijali.
Wakulima wa pamba tumekuwa tukipata hasara kila mwaka, ni bora turuhusiwe kuachana na ukulima wa zao hili,”alisema Kiumbani:
“Kwa upande mwingine tangu nakua naona Serikali haitaki wafugaji, kule porini wameleta ndege wanawafukuza ng’ombe wetu wanavunjika miguu na wanakuwa wanazaa bila mpangilio, hili suala liangaliwe.”
Alisema pia kuwa, madaktari wasiruhusiwe kumiliki maduka ya dawa kwani wanatumia nafasi hiyo kuiba dawa za hospitali za umma.
“Unaenda hospitalini unaambiwa dawa hakuna halafu daktari anakuelekeza duka la kwenda kununua dawa, hii siyo sawa haya maduka yatakuwa ni yao na wanapeleka huko dawa za hospitali zetu,” alisema.
Kwa upande wake Masanja Kurwa, alitaka Katiba ijayo iwatambue wanaume waliofiwa na wake zao na kuwapa fursa ya kupata misaada mbalimbali.
“Mbona wanawake wajane wanapewa misaada lakini wanaume wakifiwa na waume zao hawapewi msaada, wanaume tuliofiwa na wake zetu na sisi tutambuliwe,” alieleza.
No comments:
Post a Comment