BADO miezi michache kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya tayari mashirika mbalimbali ya utafiti yameshaanza kubashiri washindi wa uchaguzi huo utakaofanyika mwezi Machi mwakani watakuwa kina nani.
Ni Kawaida kwa mashirika ya utafiti ulimwenguni kote kufanya utafiti hususan kipindi cha karibia na uchaguzi wa nchi husika.
Nchini Kenya Utafiti uliofanywa na Kampuni ya Synovate umebaini kwamba muungano wa Coalition for Reform and Democracy (CORD) unaoshirikisha vyama vya ODM, Wiper Democratic Movement na Ford – Kenya ungeibuka na ushindi endapo uchaguzi mkuu ungefanyika mwezi huu wa Desemba.
Hata hivyo, kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo uliofanywa kati ya tarehe 6 na 11, ushindi huo haungetambulika kikatiba kwani mgombea urais wa CORD angepata asilimia 47 dhidi ya asilimia 41 ya washindani wakuu, Muungano wa Jubilee. Hii ni endapo Waziri Mkuu Raila Odinga na Naibu wake Uhuru Kenyatta watatawazwa wagombea urais wa miungano hii huku Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka na Mbunge wa Eldoret Kaskazini William Ruto wakiwa wagombeaji wenza.
Hata hivyo, utafiti huo, uliofanywa na kudhaminiwa na Kampuni ya Ipsos Synovate, CORD ilipata asilimia 48 dhidi ya asilimia 38 ya Jubilee iwapo Naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi atateuliwa kupeperusha bendera ya muungano huo. Watu 1,625 wenye umri wa miaka 18 na zaidi walihojiwa kwa njia ya simu ya mkononi.
Mtafiti Mkuu wa kampuni hiyo Dk Tom Wolf, hata hivyo alisema kuwa bado kuna maswala mengi ambayo yanaweza kubadili matokeo hayo, ikizingatiwa kuwa miungano hiyo na vyama tanzu vina muda wa hadi Februari 11, 2013 kabla ya kuwasilisha orodha kamili ya watakaogombea nyadhifa mbali mbali kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Vilevile, uteuzi wa mgombea urais wa muungano wa Jubilee, unaoshirikisha vyama vya TNA, URP na UDF Jumanne ijayo, na makubaliano ya mwisho kuhusu suala hilo katika CORD jana alisema, huenda yakabadili mambo.
“Matokeo hayo yanaweza kubadilika baada ya miungano mikuu kufanya teuzi zao za wagombea urais na pale teuzi za wagombezi wa nyadhifa nyingine zitakapokamilika kabla ya Februari 11 mwaka ujao, “ akaeleza Dk Wolf.
Kumekuwa na hali ya vuta nikuvute katika muungano huo kuhusu mbinu na utaratibu wa kumteua mgombea urais kati ya Uhuru Kenyatta na Musalia Mudavadi. Wafuasi wa Uhuru wanapendelea mfumo wa wajumbe huku wenzao wa UDF wakionekana kuegemea ule mfumo wa mwafaka.
Kulingana na umaarufu wa wawaniaji urais kibinafsi, Raila anaongoza kwa umaarufu wa asilimia 34 huku akifutwa na Uhuru kwa asilimia 27, ishara kwamba umaarufu wao umepanda kwa alama moja tangu mwezi uliopita.
Hata hivyo, kutokana na dhana iliyokolea wengi kwamba Makamu wa Rais na kiongozi wa URP, William Ruto watakuwa wagombezi wenza, umaarufu wao ulishuka kwa asilimia 5 na 7 huku ule wa Mudavadi ukishuka kwa asilimia 1. Kalonzo ana asilimia 3 kutoka 8 alioandikisha mwezi wa Novemba. Naye Ruto akiwa na umaarufu wa asilimia 2 kutoka 9 mwezi uliopita.
Utafiti huo pia ulionyesha kuwa asilimia 85 ya waliohojiwa wanafahamu kuhusu muungano wa CORD.
No comments:
Post a Comment