Saturday, December 22, 2012

Viongozi waaswa kuacha kutumia yahoo.com

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Victor Nkya wakati akitoa mada katika ya kazi na majukumu ya ya TCRA kwa waandishi wa habari huko Hoteli ya Zanzibar Ocean View leo.

MAMKALA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezishauri taasisi za serikali na viongozi wake kutumia mitandao inayotambulika badala ya kutumia mitandao ambayo haina uhakika kiusalama nchini.

Ushauri huyo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Victor Nkya wakati akitoa mada katika ya kazi na majukumu ya ya TCRA kwa waandishi wa habari huko Hoteli ya Zanzibar Ocean View jana.Alisema baadhi ya viongozi wa serikali na taasisi zake wamekuwa wakitumia mitandao kama yahoo.com ambayo haina uhakika kiusalama imekuwa ikivamiwa mara kwa mara na wajanja wenye kuingilia mawasiliano duniani.

“Ningewashauri viongozi wa serikali wakawa wanatumia mitandao yetu ya tz.com badala ya kutumia mitandao kama yahoo kwa sababu hata katika usalama wa kuingiliwa mitandao hiyo ni rahisi na kazi hii ndio tumeianza kuwashawishi na nyinyi wanadishi wa habari tusaidieni” alisisitiza Nkya.

Nkya alisema katika kuhakikisha hilo linafanyiwa kazi mamlaka yake imeanza kuwashawishi maafisa wa mamlaka hiyo kutumia mitandao hiyo ya tz.com na kuwataka waachane na mitandao mengine ambayo imekuwa ikitumiwa na watu wengi.

Akizungumzia suala la kuwa na kazi ndogo ‘slow’ mitandao yao amesema sio kweli kama haina kazi lakini wenye kuongelea hilo hawajui faida na matumizi ya mitandao ambapo kasi yake ni kubwa na upatikanaji wa huduma zake ni wa urahisi zaidi kuliko mitandao mengine.

Aidha aliwaomba waandishi wa habari kuwaelimisha wananchi juu ya uvumi wa athari za minara ya mawasiliano inayowekwa katika maeneo mbali mbali kuwa haina athari zozote za kiafya na kuwataka wananchi waondokane na dhana hiyo kwani tayari utafiti uliofanywa na mamlaka yake kwa kushirikiana na idaraza mionzi na kugundua hakuna madhara yoyote juu ya minara hiyo ya simu.

“Tumefanya utafiti kwa kushirikiana na mamlaka nyengine na tulichogundua kwamba hakuna athari zozote za kiafya lakini bado wananchi wana khofu juu ya suala hili ambalo linawatia shaka, hivyo basi waandishi wa habari mnapaswa kutoa elimu kwa umma juu ya suala hili” alisema Nkya.

Akitoa historia ya kazi za mawasiliano na majukumu yake Meneja Mawasiliano, Innocent Mungy alisema dunia imetokea mbali katika teknolojia hadi kufikia leo ambapo teknolojia imekuwa kwa kiwango kikubwa ambapo dunia imekuwa zaidi ya kijiji.

Alisema pamoja na ukuaji wa teknolojia hiyo kumekuwepo na changamoto nyingi katika mamlaka ya mawasiliano lakini mamlaka hiyo imekuwa ikizifanyia kazi ili kuona watanzania wananufaika na makampuni ya mawasiliano nchini na kupata huduma zilizo bora.

Alisema makampuni yenye kutoa huduma za yamekuwa yakilalamikiwa lakini kwa kuwa kumekuwepo na ushindani wananchi wamekuwa wakichagua makampuni ya kuyatumia na wanapokuwa hawaridhishwi na huduma zinazotolewa na kampuni moja huwa wanahama na kuingia kampuni nyengine.

“Huku kuwepo kwa makampuni nyingi za mawasiliano mfano mitandao ya simu kunafanya mwananchi mwenyewe achague huduma anayotaka kwa sababu kungekuwa na kampuni moja tu kama vile zamani ingekuwa shida lakini sasa teknolojia imekuwa na mtu ana uhuru wa kuchagua huduma bora” alisema Mughy.

Mughy alisema mamlaka ya mawasiliano kazi yake ni kusimamia sheria na kanuni na kuwataka makampuni ya mawasiliano ya simu kufuata sheria za mamlaka hiyo ili lengo la mamlaka hiyo liweze kufanikiwa katika kuwarahisishia wananchi huduma ya mawasiliano nchini.

No comments: