Wakuu hao wa wilaya waliopata vyeti hivyo ni wa Meatu mkoani Simiyu Rosemary Kirigini na Monduli, Jowika Kasunga
Jukwaa Katiba Tanzania limetoa hati chafu kwa wakuu wa wilaya wawili wanatuhumiwa kudhoofisha jitihada za uhamasishaji wananchi kuhusu mchakato wa katiba mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa jukwa hilo, Deus Kibamba, alisema wakuu hao wa wilaya wamekuwa mwiba kwenye kampeni za kuhamasisha wananchi umuhimu wa kutoa maoni yao kwenye Tume ya Katiba inapofika katika meneo ya wilaya hizo.
“Jukwaa la Katiba Tanzania, leo (jana) tunatoa hati maalumu kwa viongozi hao kama ishara ya kuwatangaza kuwa maadui wa katiba mpya. Utaratibu huu utaendelea katika muda wote wa uundaji wa katiba mpya hadi kukamilika,” alisema.
Katika hati hizo, kichwa cha habari kilieleza ‘hati ya uadui wa mchakato wa katiba mpya’.
Akifafanua zaidi, Kibamba alisema mkuu wa wilaya ya Meatu alizuia mkutano ulioandaliwa na mtandao wa asasi za kiraia wilayani humo ya Mengonet akitaka wasijadili masuala ya katiba bali mambo mengine.
Alisema jambo kama hilo lilijitokeza wilayani Monduli ambako mkuu wa wilaya hiyo alizuia uhamasishaji uliokuwa ukifanywa na taasisi ya Pingos Forum akidai kuwa anahitaji taarifa zaidi za taasisi hiyo kabla ya kuiruhusu kufanya kazi katika wilaya yake.
“Ni imani yetu kuwa waliopata hati hizi, ambazo nakala yake tutazipeleka kwa mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, watabadilika na kuheshimu zaidi mchakato wa Katiba Mpya na katiba iliyopo ya Tanzania, ambapo kwayo, ndiyo waliapa kuwa wataitetea na kuilinda,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment