*Yadaiwa kujaa mamluki
*Kisa, kupinga Muungano
*Kisa, kupinga Muungano
Vurugu hizo zilitokea kwa mara ya kwanza katika uwanja wa Mzalendo, Jimbo Magomeni juzi na Uwanja wa Mpendae mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na kujirudia jana.
Akizungumza na NIPASHE jana, Kamishina wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Prof. Mwesiga Baregu, alithibitisha kuvunjika kwa mkutano huo kwa mara ya pili baada ya kutokea vurugu na mabishano makali baina ya wananchi kabla ya Tume kuanza kazi ya kukusanya maoni.
Alisema kwamba, juzi katika uwanja Mzalendo Magomeni watu wasiokuwa wakazi wa eneo hilo walikwenda wakiwa wamepakiwa katika magari wakitaka kutoa maoni, lakini walizuiwa na wananchi wenzao wa maeneo hayo kwa madai hawakuwa wakazi halali wa maeneo hayo.
Alieleza kwamba baada ya watu hao kufika katika uwanja huo, wananchi wakazi wa shehia ya Meya na Mpendae walipinga watu hao kutoa maoni wakati siyo wakazi wa shehia hizo.
Prof. Baregu alisema kwamba Tume baada ya kuona hali imechafuka iliamua kusitisha kazi ya kukusanya maoni kwa sababu za kiusalama hasa kwa kuzingatia kuwa haipendi kuona wananchi wakitoa maoni yao wakiwa katika ulinzi mkali wa askari wenye silaha.
Profesa Baregu alisema kwamba Tume ilikuwa na uwezo wa kuimarisha ulinzi wa polisi na kuendelea kukusanya maoni, lakini inataka wananchi watoe maoni yao wakiwa katika mazingira huru bila ya kuwapo askari wenye sare na silaha za moto.
Alisema kwamba tangu tume hiyo ilipoanza kazi ya kukusanya maoni katika wilaya ya Mjini kumejitokeza vitendo vya baadhi ya wananchi kutoa maoni kwa mvutano kati ya wanaotaka mfumo wa Muungano wa mkataba na wale wa mfumo wa Muungano wa serikali mbili, huku watu wasiokuwa wakazi wa maeneo husika wakitumika kutoa maoni.
Alisema kwamba watu hao wamekuwa wakiwahi mapema na kujipanga mwanzo kutoa maoni, kitendo ambacho huwanyima nafasi wakazi halali na kuibua vurugu katika viwanja vya kutoa maoni.
Aidha, alisema kwamba watu hao ambao siyo wakazi wa maeneo husika wamekuwa wakitaka mfumo wa Muungano wa serikali tatu ikiwamo ya Muungano wa mkataba, lakini wamekuwa wakifanya vitendo vya vurugu kama kushangilia na kuzomea kwa watu wanaotoa maoni tofauti na mtazamo wao jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu wa ukusanyaji wa maoni.
Kamishina huyo alisema hafahamu kama wananchi wanaopelekwa kwa magari kutoa maoni kama hawana nauli au katika maeneo wanayoishi hakuna huduma za kawaida za usafiri kama daladala, lakini alisema ni kosa kwa mwananchi kutoa maoni zaidi ya mara moja kwa mujibu wa sheria.
“Kwa sababu za kiusalama tukaamua kusitisha zoezi la kukusanya maoni baada ya kutokea mabishano na vurugu jambo la msingi tunaomba wananchi wazingatie sheria,’ alisema.
Prof. Baregu alisema kwamba kitendo hicho kimekuwa kikisababisha wananchi kupinga mikutano yao kuvamiwa na watu kutoa maoni wakati siyo wakazi wa meneneo hayo.
Hata hivyo, Prof. Baregu alisema kwamba Tume itaendelea na ratiba yake kama ilivyopagwa na sehemu ambayo wananchi wamekwama kutoa maoni itamua baadaye.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, Azizi Juma Mohamed, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na pia kuvunjwa kwa mikutano hiyo, lakini hakuwa na taarifa za kina kwa kuwa jana alikuwa ametingwa na shughuli za kukaguliwa kwa mkoa wake, ukaguzi unaofanywa na Kamishna wa Polisi Zanzibar. Aliahidi kutoa taarifa zaidi leo.
Hata hivyo, mashuhuda waliozungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti walisema kuwa wanahisi aliyejeruhiwa amekatwa na kisu.
NIPASHE ilifika Hospitali ya Mnazi Mmoja kutaka kujua kama wamepokea majeruhi huyo, lakini ilielezwa kwamba hakuna mtu kama huyo aliyepokewa jana hospitalini hapo.
Hata hivyo taarifa kutoka katika eneo la tukio huko Mpendae zinasema kwamba mtu mmoja alijeruhiwa kufutia vurugu hizo.
CUF WAZUNGUMZA
Akizungumza juu ya vurugu hizo kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari na Uenezi wa Chama cha Wananchi (Cuf), Salum Bimani Abdalla, alidai Kamishina wa Tume hiyo Fatma Said Ali na Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Salmin Awadhi ndiyo chimbuko la vurugu hizo.
“Mwakilishi Salmin Awadh Salmin, pamoja na Waziri Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Fatma Said Ali, ambaye pia ni Kamishna wa Tume wamevuruga zoezi na hatimaye wananchi kushindwa kabisa kutoa maoni yao,” alidai Bimani katika taarifa hiyo.
Alisema Cuf imeshtushwa na hali hiyo ambayo imelenga kuchafua zoezi hilo halali na pia kuinyima Tume nafasi yake ya kuendesha shughuli zake.
Alisema kwamba tokea Tume lilipoanza kazi yake mkoa wa Kusini Unguja Julai mwaka huu hadi Disemba 5 mwaka huu ilipomaliza katika wilaya ya Magharibi Unguja, haijawahi kutokea hali kama hiyo.
“CUF kinatoa wito kwa Tume kuchukua hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria ili kuondoa jeuri na kiburi kwa viongozi wanaotaka kuvuruga kazi ya kukusanya maoni ya wananchi” ilisema taarifa hiyo.
Bimani alisema kitendo kilichofanyika ni uvunjifu wa amani, kinyume na Sheria na pia kukiuka kifungu cha 21 (a) (i)(ii) cha Sheria ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Muungano.
CCM YAITAHADHARISHA TUME
Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeitahadharisha Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba kuwa macho na njama zinazofanywa na baadhi ya vyama vya siasa za kuandaa makundi ya vijana ambao siyo wakazi wa vituo husika vya kutoa maoni na kusababisha vurugu kutokea.
Tahadhari hiyi ilitolewa na Katibu Msaidizi Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi Makao Makuu ya CCM Kisiwanduwi Zanzibar, Ali Mwinyi Msuko, katika taarifa yake baada ya vurugu zilizotokea katika Jimbo la Magomeni na Mpendae wilaya ya Mjini Zanzibar.
Alisema kwamba vitendo vya kupandikiza watoa maoni mamluki vimesababisha vurugu na kuwanyima haki ya kutoa maoni wakazi halali, kitendo ambacho ni kinyume cha Sheria ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Vurugu hizo zimesababisha wananchi wa Shehia ya Mzalendo/Magomeni na Mpendae kushindwa kutoa maoni yao kitendo ambacho ni kuwanyima haki yao ya kikatiba,” alisema Msuko.
Alisema CCM imesikitishwa na kitendo cha watu kupakiwa katika magari na kwenda kutoa maoni katika maeneo ambayo hawaishi na kusababisha vurugu.
Aidha, alisema kwamba kitendo cha kutoa maoni zaidi ya mara moja kwa mujibu wa sheria ni kosa na wakati umefika kwa Tume kuchukua hatua kali dhidi ya watoa maoni mamluki.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment