ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 10, 2012

Waliofariki ajali ya Iringa watambuliwa

Miili ya watu tisa waliokufa katika ajali ya basi la Usokami Tours, mali ya kampuni ya Msanya iliyotokea juzi katika Kijiji cha Kituyu mkoani Iringa, wametambuliwa na baadhi kuchukuliwa na ndugu zao.

Basi hilo lenye namba za usajili T 803 AJV aina ya NISSAN UD linalofanya kazi zake kati ya Iringa mjini na mji mdogo wa Usokami Wilaya ya Mufindi, liliacha njia na kutumbukia katika korongo baada ya kupata hitilafu katika breki na kisha kumshinda dereva wa basi hilo, Rashid Msangi (34).

Abiria 61 wa basi hilo walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Kati yao watu 28 walijeruhiwa vibaya.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa, Dk. Faustine Gwanchelle aliwataja maiti waliotambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao ni pamoja na Kurwa Hendry (28) mkazi wa Mwatasi, Elias Kigodi (52) mkazi wa Mawambala, wote kutoka Wilaya ya Kilolo.

Wengine ni Mwajuma Galasinde (70) mkazi wa Ikomongo, Fausta Kitove (21) mkazi wa Kitwila, Maria Mgata mkazi wa Mkimbizi, Manispaa ya Iringa, Schola Benard (42) mkazi wa Ugele, Mapreti Mgogosi (56), Lubeda Mgogosi (23) wote wakazi wa Igumutwa Wilaya ya Mufindi.

Kuhusu hali ya majeruhi waliolazwa hospitalini hapo akiwamo Msangi ambaye alikuwa dereva wa basi hilo, mkazi wa Mlandege katika Manispaa ya Iringa ambaye ameungua mkono baada ya kubanwa kifuani na usukani zinaendelea vizuri.

CHANZO:NIPASHE

No comments: