MVUTANO wa kisiasa baina ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani umevuka mipaka na sasa unatishia kukigawa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Kagera.
Kagasheni ni Mbunge wa Bukoba Mjini wakati Amani mbali na kuwa Meya pia ni Diwani wa Kata ya Kagondo na wote wamekuwa katika mvutano ambao umekuwa ukihusishwa na vita ya ubunge katika Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015.
Kadhalika, mgogoro kati ya viongozi hao unahusishwa na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa Soko Kuu la Bukoba na upimaji wa viwanja 5,000, miradi ambayo Kagasheki anadai ni ya kifisadi kwa madai kwamba mikataba yake haiko wazi na mmojawapo haujafanyiwa upembuzi yakinifu.
Juzi, mgogoro huo ulichukua sura mpya baada ya halmashauri ya chama hicho Wilaya ya Bukoba Mjini kupiga kura ya kutokuwa na imani na Meya Amani, hatua mbayo ni kujenga hoja ya kuwashawishi madiwani wa chama hicho kumng’oa katika nafasi yake.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Costansia Buhiye alisema jana kwamba hajapata taarifa kuhusu uamuzi huo, lakini akasema halmashauri hiyo haina uwezo wa kumwondoa Amani katika nafasi yake.
“Kwanza lazima tufahamu kwamba chombo chenye uwezo wa kumwondoa meya katika nafasi yake ni Baraza la Madiwani la Manispaa. Kama huyo meya ni mwanachama wa CCM, chama chetu kina taratibu zake ambazo ziko wazi na zinafahamika,” alisema Buhiye.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho cha juzi kilichofanya uamuzi huo zinasema zaidi ya asilimia 80 ya wajumbe walipiga kura za kunyoosha mikono kuonyesha kutokuwa na imani na Amani.
Baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba Mjini, Yusuph Ngaiza na Katibu wake Janath Kayanda, waligoma kuzungumza na waandishi wa habari, huku kila mmoja akimrushia mpira mwenzake kutaja idadi ya kura zilizopendekeza kung’olewa kwa Amani.
Ndani ya Kikao
Kikao hicho kilitawaliwa na vituko kadhaa ambavyo ni pamoja na Kagasheki kutaka Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera, Aveline Mushi na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Zipora Pangani watolewe nje kwa madai kwamba hakuwa na imani nao.
Anadaiwa kutoa hoja hiyo muda mfupi baada ya Mushi kuzungumza, huku akiwaasa madiwani wa CCM ambao wote ni wajumbe wa mkutano huo, wasiyumbe kwenye uamuzi kwani kwa kufanya hivyo wangekuwa wanapingana na uamuzi walioutoa awali.
Mushi alikuwa akifanya marejeo ya ajenda zilizotangazwa na Kayanda ambazo ni hali ya kisiasa, miradi inayotekelezwa na halmashauri katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2015 na tathmini ya chaguzi za jumuiya ngazi ya wilaya.
Baada ya hoja ya Kagasheki, Mushi na Pangani walitoka nje ya Ukumbi wa mikutano wa Mtakatifu Francis unaomilikiwa na Kanisa Katoliki lakini baada ya muda mfupi, walirejea ndani ya ukumbi na kuendelea na mkutano huo. Hata hivyo, alipoulizwa jana kuhusu sakata hilo, Mushi aling’aka akisema: “Huo ni umbea tu, mimi ni mjumbe halali na nilishiriki mkutano.”
Kadhalika, kabla ya kikao kuanza, wajumbe wote walinyang’anywa simu za mkononi kutokana na kile Mwenyekiti Ngaiza alichosema wasingependa watu kurekodi mazungumzo au kutuma ujumbe mfupi wa maneno maana kilikuwa ni cha siri na kwamba maazimio yake yangetangazwa baadaye.
Kagasheki na Amani
Katika kikao cha juzi, mvutano baina ya Amani na Balozi Kagasheki ulikuwa ni dhahiri kwani suala la madaraka kuwa chanzo cha mvutano uliopo lilizungumzwa.
Kagasheki alisema hawezi kumchukia Amani kwa sababu za kugombea ubunge katika jimbo hilo kwani hamtishi na kwamba hata Amani akigombea, hawezi kumshinda.
Kagasheki alisema kutokana na matatizo yaliyojitokeza na kusababisha mgogoro kati yao, hayuko tayari kufanya naye kazi.
Kwa upande wake, Amani alisema ugomvi baina yake na Kagasheki unatokana na watu wachache wasiopenda maendeleo, ambao alidai wamekuwa wakimpelekea maneno kuwa anataka kumnyang’anya jimbo lake.
“Kuna watu ni ndumila kuwili walimwambia Mbunge (Balozi Kagasheki) kuwa nataka kumnyang’anya jimbo baada ya kuona kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, lengo lao tusitekeleze miradi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi,” alisema Amani katika kikao hicho.
Aliwasuta wajumbe wa halmashauri ya CCM wilaya ambao walidai kwamba chama hakina taarifa ya miradi inayotekelezwa. akisema wamekuwa wakihudhuria vikao vya uamuzi na saini zao zipo kwenye nyaraka husika.
Matukio ya Karibuni
Katika mkutano wa hadhara wa hivi karibuni, Balozi Kagasheki aliwatangazia wapigakura wake wa Bukoba Mjini kwamba hatakubali Soko Kuu la Bukoba livunjwe kwa maelezo kwamba utaratibu unaotumika hauwatendei haki.
Pia aliuponda mradi wa upimaji viwanja akisema umesababisha malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi waliodai kwamba mashamba waliyokuwa wakimiliki kihalali yalichukuliwa bila kulipwa au kwa malipo kidogo, huku akitahadharisha kwamba mchezo wanaoanza ndani ya CCM utapoteza jimbo hilo 2015.
Hata hivyo, Amani alijibu madai hayo akisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo, ukiwamo wa kuvunja soko utaendelea kwa kuwa hatekelezi maagizo ya Mbunge, bali maazimio ya vikao.
Katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi hivi karibuni, ilikubaliwa kuwa soko hilo lianze kuvunjwa katikati ya mwezi ujao na litajengwa kwa miezi 18 kwa gharama ya Sh12 bilioni.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment