ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 5, 2013

Abiria 12 wahofiwa kufa ajali ya kuzama boti Kigoma


Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya
 Udhibiti wa
Usafiri wa Majini na Nchi kavu
(Sumatra), David Mziray
Abiria 12 wanahofiwa kufa maji baada ya boti  waliyokuwa wanasafiria ndani ya Ziwa Tanganyika kupinduka na kuzama.
Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana  katika Kijiji cha Herembe kilichoko Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Habari zilizopatikana kutoka kwa wanavijiji walioko eneo la tukio zilieleza kuwa abiria zaidi ya 60 waliokolewa wakati wengine zaidi ya 25 hawajulikani walipo na 12 wakihofiwa kufa maji.
 
Kufuatia tukio wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kigoma ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni Kanali mstaafu Issa Machibya wamekwenda kwenye eneo la ajali  hiyo.
 
Hata hivyo kutokana na kukosa mawasiliano na pia Herembe kukabiliwa na changamoto za kimiundo mbinu  ilishindikana kupata taarifa za safari ya boti hiyo iwapo ilikuwa ni ya ndani ama ilikuwa inafanya safari ya  nchi jirani.
 
Baadhi ya wanavijiji walidai kuwa boti hiyo ilikuwa inasafiri kati kijiji cha mwambao cha Kalya  kwenda bandari ya Kigoma wakati wengine walidai ilikuwa njiani kuelekea  Burundi.
 
Mashuhuda walisema boti hiyo ilikuwa na shehena ya dagaa na abiria zaidi ya 100 na ilipinduka kufuatia dhoruba iliyosababisha kuyumba na kugonga mwamba ,
 
Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma kupitia simu yake ya mkononi hazikufanikiwa.
Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi kavu (Sumatra), David Mziray alisema mamlaka hiyo   ilikuwa haijapata  taarifa kuhusiana na  kuzama kwa boti hiyo.
 
Aliahidi kufuatilia kupitia kikosi cha  uokoaji ili kubainisha kile kilichojiri. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: