ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 5, 2013

Atakachotupa Obama katika muhula wake wa pili

Ahmed Rajab
BARACK Hussein Obama alipochaguliwa mara ya kwanza kuwa Rais wa Marekani 2008 dunia nzima ilisisimkwa. Sisi wazawa wa Afrika pamoja na wenzetu waliozaliwa ughaibuni lakini wenye asili zitokazo bara hili tulisisimkwa zaidi ya wote. Kuna waliolia na kuna waliotokwa tu na machozi.
Sote tulifurahi kumuona mtu anayefanana nasi kachaguliwa kuliongoza taifa lililo na nguvu kushinda yote duniani. Hilo lilikuwa tukio kubwa. Kwa mara ya mwanzo Marekani ilimchagua rais na amiri jeshi asiye mzungu kuliongoza taifa ambalo kwa karne kadhaa limekuwa likimuona mtu mweusi kuwa si kitu.

Sisi wa Afrika ya Mashariki tulizidi kushangilia kwa vile baba wa Rais mpya wa Marekani alikuwa Mkenya. Ni baba yake wala si babu wa babu wa babu yake. Zaidi ya Uafrika wake Rais huyo wa Marekani alizaliwa na baba aliyekuwa Mwislamu na babu aliyekuwa mswalihina.
Kuchaguliwa kwa Obama kuliwakashifu wengi Tanzania ambao bado hawako tayari kumkubali Mtanzania mwenzao awaongoze ikiwa ana hata tone la damu ya kigeni.
Ugonjwa huu uko Bara na Visiwani ambako karibuni tuliwasikia viongozi wa CCM wakieneza siasa za chuki za kikabila. Walitamka waziwazi kwamba wenzao waliochanganya damu hawafai kuaminiwa.
Kilichoshtusha ni kukiona chama chao kikikaa kimya bila ya hata kuwakemea.
Katika kampeni zake za kuugombea urais mara ya mwanzo Obama aliahidi mengi kwa masikini wa Marekani ambao wengi wao ni wenye asili ya Afrika.
Baada ya Obama kuupata urais tabaka hilo la Wamarekani halikupata afuweni yoyote. Hali za masikini wa rangi zote zilizidi kudidimia kama zilivyodidimia hali za Wamarekani wengine, isipokuwa labda za wale walio miongoni mwa asilimia moja ya Wamarekani ambao ni matajiri kupita kiasi.
Kuhusu Afrika muhula wa kwanza wa Obama ulituvunja moyo. Obama alionyesha kama halijali bara la asili yake. Mbali na kuitembelea Misri ambako alizungumzia zaidi masuala ya Mashariki ya Kati,
Obama aliizuru Ghana Julai 2009. Alitoa hotuba iliyojaa ahadi tele. Kwa ufupi, aliahidi kuwa Marekani italisaidia bara la Afrika lijipatie ufanisi kwa kuondosha utawala mbovu.
Ahadi hiyo hakuitimiza. Badala yake Obama amekuwa akishikiriana zaidi na wenye kuongoza tawala mbovu — mbovu ama kwa sababu zinaikiuka miiko ya kidemokrasia au kwa sababu zinavumilia ufisadi.
Tarehe 14 Juni 2012 Obama alitia saini waraka uitwao “Mkakati wa Marekani Kuhusu Afrika Kusini Mwa Sahara.” Hakuna lililo jipya katika ‘mkakati’ huo. Ni yayo kwa yayo maji ya futi kwa nyayo. Mambo manne yalitiliwa mkazo: kuimarisha demokrasia Afrika; kulikuza kiuchumi bara la Afrika kwa biashara na uwekezaji; amani na usalama; na fursa na maendeleo.
Hakuna lililo jipya katika hayo kwa sababu Marekani imekuwa ikiyapigia ngoma miaka na miaka. Na hakuna hata moja kati ya hayo lililoinufaisha Afrika kiasi cha mtu kusema: “Ama kwa hili Marekani imeifanyia jambo Afrika.” Tunaweza kusema hivyo kuhusu China lakini si kuhusu Marekani ya Obama.
Kuna wasemao kwamba Obama kwa makusudi alilipuuza bara la Afrika katika muhula wake wa kwanza asije akalaumiwa kwamba amelishughulikia bara la babake badala ya kuwashughulikia masikini wa Marekani.
Wenye kuamini hivyo wanahoji kwamba kwa vile huu muhula wake wa sasa ndio wa mwisho basi labda atakuwa na ujasiri wa kuyashughulikia masuala yote hayo.
Tunaloweza kulisema kwa uhakika ni kwamba katika muhula wake wa pili utaoanza rasmi atapoapishwa tarehe 20 mwezi huu Obama atazidi kulitumbukiza bara la Afrika katika vita. Hilo ndilo suala kuu litaloongoza sera yake kuhusu Afrika.
Usalama na vita dhidi ya ugaidi wa kimataifa umempa Obama kisingizio cha kupeleka majeshi katika nchi mbalimbali za Kiafrika. Wakati huohuo Wizara yake ya Ulinzi (Pentagon) imekuwa ikiunda mtandao wa kijasusi unaozilenga nchi za Kiafrika na za Mashariki ya Kati. Inasemekana mtandao huo utakuwa mkubwa kushinda ule wa Idara ya Ujasusi ya Marekani (CIA).
Kuna wanaoshukuru kwamba Balozi Susan Rice hatokuwa tena waziri wa mambo ya nje. Ingawa angetaka Afrika ishughulikiwe zaidi hata hivyo misimamo yake kuhusu nchi kadhaa za Kiafrika, kwa mfano Sudan, ingetatiza mambo. Inavyoelekea ni kwamba seneta John Kerry ndiye atayekuwa waziri mpya wa mambo ya nje akimrithi Hillary Clinton.
Kerry hana uzoefu mkubwa kuhusu Afrika ingawa mkewe amezaliwa Msumbiji. Hata hivyo, pengine yeye atakuwa na msimamo mzuri kushinda Rice. Huenda waziri wake msaidizi kuhusu Afrika akawa Michele Gavin, Balozi wa Marekani nchini Botswana. Zamani akifanya kazi katika Senate alikokuwa msaidizi wa Seneta Russ Feingold.
Mtu aliye karibu zaidi na Obama kuhusu Afrika ni Johnnie Carson, waziri mdogo wa Afrika. Lakini sidhani kama Carson ataweza kumsaidia Obama kwa vile nafikiri huenda akastaafu karibuni.
Wengine wanaoweza kuwa na ushawishi kwa Obama kuhusu Afrika ni watumishi wa zamani katika utawala wa Rais Bill Clinton kama vile Gayle Smith mkurugenzi mkuu katika Baraza la Usalama wa Kitaifa na John Prendergast maarufu kwa kampeni zake kuhusu Sudan, magaidi wa Lord’s Resistance Army na Congo-Kinshasa.
Nje ya serikali kuna watu kadhaa wataoendelea kuwa na ushawishi juu ya sera ya Afrika. Miongoni mwao ni John Peter Pham mwenye siasa za mrengo wa chama cha Republican. Pham anaongoza kitengo cha Afrika katika taasisi ya Atlantic Council na huenda akawa miongoni mwa wataomshadidia Obama azidi kuingilia kijeshi Afrika.
Kwenye taasisi nyingine zisizo za kiserikali kuna Jennifer Cooke mkurugenzi wa Afrika katika Center for Strategic and International Studies (CSIS) na Balozi John Campbell wa Council on Foreign Relations.
Katika taasisi ya Brookings Institution kuna wataalamu wawili wa masuala ya Afrika: Dakta Mwangi Kimenya (aliyezaliwa Kenya) na Witney Schneidman waziri mdogo wa zamani wa Afrika. Wote hao watasikilizwa na wapangaji wa sera ya Afrika ya Obama katika muhula wake wa pili.

8 comments:

Anonymous said...

Ni wazi kuwa hufahamu siasa za Marekani... Kwa Obama kuwa Rais wa Marekani siyo mwisho wa matatizo ya Africa au mwafrica anaishi hapa US!! 2008 Obama alirithi nchi iliyovurugika ktk kila upande.. Uchumi, siasa za ndani na nje, ..Kwa wamerekani weusi na masikini weupe wanalitambua hilo na ndiyo maana bado wako nyuma ya Obama wakiamini kuwa ndiyo mtu pekee anaeweza kuleta tena zama za Clinton zilizojaa kazi tele na maisha bora kwa kila mmarekani.. Africa!! Tufahamu kuwa Rais wa Marekani hatembei kuja Africa kama wafanyavyo marais wa Africa.. ni gharama kubwa sana kwa Rais wa hapa kutembelea nchi ambazo hazina miundo mbinu isiyoeleweka.. si uamuzi wake peke yake, kuna CIA, FBI na Secret service ambao wanawajibika kwa usalama wa Rais. Tusisahau marekani bado iko vitani ktk ulimwengu huu uliojaa magaidi kila kona.. Obama anakazi kubwa ya kurekebisha America kabla hajapoteza muda kutalii Africa.. Africa kwa nini hatutaki kujikomboa kutoka umasikini unaosababishwa na tawala mbovu? Obama anatuhusia kujenga tawala za kisheria.. Ghana ni mfano wa kuigwa ndiyo maana alizuru huko.. Kenya? Ndiyo babake Obama ni mKenya lakini tumesahau Walichokifanya waKenya miaka michache iliyopita? Tanzania? ..miaka 51 ya uhuru bado hatujaweza kuwa na bajeti inayojitegemea: ( wizi kila sekta ,hata kidogo tunachovuna kinaishia mikononi mwa mafisadi ya CCM.. tuache dhana ya kutegemea misaada Mungu ametubariki na kila kitu.. Tuwasakame viongozi wetu? Rais wetu siyo Obama.. tunahitaji Katiba mpya yenye kuweka misingi ya utawala bora siyo hii ya sasa yenye kumpa Rais nguvu za kifalme, Mungu ibariki Africa Mungu ibariki Tanzania.

Anonymous said...

Mdau mada yako ni nzuri. Sawa Obama anayo mapungufu katika kusaidia Africa. Lakini lazima Waafrika tukubali kuwa viongozi wetu wana mawazo finyu katika kuliletea bara letu maendeleo. Mwaka 1960, maendeleo kati ya nchi nyingi za Afrika yalikuwa sawa na yale ya Malaysia na Singerpore. Leo hii Afrika ni malofa wakati Mlaysia na Singerpore wako juu sana kimaendeleo japokuwa hawana mlima Kilimanjaro, natural gas, madini, mbuga za wanyama wala mazao ya biashara kama Afrika. Hakuna rais wa Marekani mwemye asili ya Malaysia au Singerpore aliyewasaidia. Lazima tubadili mfumo wa elimu yetu ili tujikomboe wenyewe kisayansi na teknolojia kuliko kumlaumu Obama ambaye hawezi ku-override American check -an-balance eti kwa sababu ya kusaidia Afrika. Kabla ya kumlaumu Obama, tujilaumu sisi kwa kujenga shule za kata zisokuwa na walimu na kuruhusu wahitimu darasa la saba kujiunga na sekondari wakati hawajui kusoma na kuandika. Obama ni rais wa Marekani, na siyo Afrika. Wamarekani inasaidia nchi ambazo kuna interest zao. Tunajivunia Obama kutokana na asili ya Kiafrika, lakini it is not fair kumlaumu wala kubebesha umasikini wetu. Tanzania, kwa mfano, ndiyo nchi pekee duniani yenye viongozi wengi wenye shahada za udaktari (PhD) lakini tuna umasikini uliokithiri. sasa Obama na marais wote wa G8 (ambao hawa PhD's)waamekosa nini? Kujivunia misaada ni aibu. Nafikiri mtoa mada umenielewa, ningependa mjadala huu undelee (with civility) Asante.

Anonymous said...

Mdau mtoa mada kichwa chako cha habari kinatudhalilisha Waafrika. Mtu anayetegemea kupewa ni mtoto, mzee na yule asiyejiweza. Unamaana kuwa Afrika kuna watoto, wazee, na wasiojiweza?

Anonymous said...

Nivizuri saana kusikia Tanzania inaongoza kwa kuwa na wasomi wengi....Wasiokuwa na manufaa yoyote kwenye nchi yao. Kiongozi wetu kaja Marekani zaidi ya viongozi wote Duniani ikiwemo Marekani yenyewe. Wakati huohuo tunadaiwa kihasi cha Dolla billion 2.5 Tshs tillion 22... Ehe mungu tumekukosea nini Africa. Mnangojea Obama aje kuikoa Africa wakati nyinyi wenyewe mnawapigia debe viongozi wabovu.

Anonymous said...

Waliitangulia wamezungumzia na kugusa pande zone, mfano tuu kwenye michuzu jana nyumba inauzwa Arusha $ 2 million na inatangazwa! Yani inatia aibu kumba msaada kwa kina nani watakuuliza, miundo mbinu mibovu lakini kila mtu ana gari, simu za mikononi waeekezaji wanawachuna walala hoi na serikali ndio inapaswa kusimamia, kupoga simu kutoka nje kwenda TZ unaweza ukafilisika, wakati India mtu unapiga simu kwa sent, marekani wamiliki wa simu za mikononi wanadhibitiwa kwa bei, privacy na vyote ili wasieahujumu rais, kuna contract za kueleweka sio ukipokea simu unalipa, ukituma msg shughuli, Angelia walipaji wakubwa - walala hoi, maana wakubwa serikali inawalipia simu zao, na makampuni yanadhitikiana na mitandao wana discount! Bado tunauliza USA itaisaidia nini tz, kwanini tusiulize kikwete keshamaliza kuinua ndugu, watoto marafiki na wote aliopita njiani kuwaona afanye la maana kutokomeza ufisadi, marekani wanaangalia raisi kalifanyia nini taifa lake, sio taifa lake limemfaidisha nini, na wanaweza vile mtu yeyote kwenye siasa hajaenda na njaa zake anaingia vile anataka kuchangia, tukiweza Hilo basi tutaweza kuanza, sikatazi rais kuwa analjichanganya misibani, lakini kama angewajibisha kila fisadi kama anavyofanya misibani mbona tungeghinda! Bado hajachelewa.

Anonymous said...

Rais aendae misibani kila uchao hatifai Tanzania..hivi tunafahamu gharama za msafara wa Rais? Ni mzigo mkubwa kwa Taifa.. kama ameishiwa kazi ikulu ni kwanini asitembelee wizara na idara za Serikali kwa kushtukiza? Ni maovu mangapi yanatendeka kila dakika pasipo yeye kujua? Hivi kweli Rais hana hata Waziri mmoja wa kumtuma msibani? Chukueni hii basi Obama hakukanyaga msiba wa Michael Jackson... Huyu Kikwete hakufaa urais hata kidogo..anafikiri ikulu ni sehemu ya kujipatia sifa za kuzika watu na kuhudhuria harusi?.. Ndiyo hapa tunapokubaliana kuwa misingi ya utawala bora hakuna bongo..
Hakuna chombo cha sheria kinachoweza kumuwajibisha Rais wa TZ..inasikitisha sana Rais anaweka jiwe la msingi..na mkuu wa mkoa nae afanye nini?..Wenzetu Kenya wameandika katiba mpya inayompunguzia Rais madaraka ya kifalme na atawajibika kwa bunge.. tuige maendeleo tusiombeombe tu... twendeni Kenya tukaangalie katiba yao iwe mfano tukiandika ya kwetu

Anonymous said...

Hayo maneo dear, watu wanaogopa kukosoa na kusema ukweli, kila mtu anaangalia ataitumiaje nchi kufaidika. Hakuna maoni ya watu wanafukiri nini au wanataka nini imfikiayo rais, wabunge wa upinzani tuu ndio wanaopiga makelele lakini watafanya nini? 'mtukufu rais' kila kukicha . Lol mpaka aibu ukisikia vitu vinavyotendeka.

Anonymous said...

Anaangalia mtandao kila siku, hivi haoni Obama anavyowajibishwa? Anafanya vile wananchi wanavyoagiza, wanasikiliza kila kitu, utashangaa RC kafika ikulu kumshukuru rais na rais kavunja shughuli zote kumsubiri na kutumia hela za kila mmoja wetu kwa mapicha. Kuna kina RC wangapi ambao Kama angekuwa mueajibikaji angesaidia kwa safari yake moja tuu ya nje na kuongelea matatizo ya mtu wa kawaida?