ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 5, 2013

Shambulio la Mufti na Padri polisi yaahidi milioni 5

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifuatana na Father Shayo wa Kanisa la Roman Katholic liliopo minara miwili     baada kuwafariji na kutoa mkono wa pole  kwa uongozi wa huo kufuatia kujeruhiwa kwa Paroko wa Parokia ya Mpendae Padre Ambrose Mkenda
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifuatana na Padri Cosmas Shayo wa Kanisa la Roman Katoriki Jimbo la Zanzibar wakati alipokwenda kutoa mkonao wa pole kwa uongozi
Jeshi la Polisi visiwani Zanzibar limetangaza donge  nono  la Sh. milioni tano kwa atakayetoa taarifa za watuhumiwa wa kumwagia tindikali  Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Soraga na kupigwa risasi kwa Padri Ambrose Mkenda.
 
Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa, alisema katika mkutano na waandishi wa habari  uliofanyika jana makao makuu ya jeshi hilo Ziwani mjini hapa.
 
Alisema yeyote atakayetoa taarifa za kusadia kukamatwa kwa watuhumiwa wa hujuma dhidi ya viongozi wa dini atazawadiwa donge nono la Shilingi milioni tano kwa  kila tukio.
 
“Tunaahidi kutoa donge nono la zawadi kwa mtu au kikundi chochote chenye taarifa za mtu ama watu waliohusika na hujuma dhidi ya viongozi wa dini visiwani hapa,” alisema Kamishna Mussa.
 
Aliongeza kuwa watu wawili wanasaidia polisi kufuatia kupigwa risasi kwa Padri Mkenda ambaye anaendelea na matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
 
Katibu wa Mufti Sheikh Soraga, Novemba 6, mwaka jana  alimwagiwa tindikali wakati akifanya mazoezi ya viungo eneo la Magogoni Msumbiji wakati Desemba 25, Padri Mkenda alipigwa risasi nyumbani kwake Tomondio.
 
Aliongeza kuwa polisi inaendelea na msako dhidi ya wafuasi wa kikundi cha  Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiisalam  Zanzibar  (JUMIKI)  waliohusika na vurugu na kusababisha uharibifu wa mali na kifo cha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Oktoba 19, mwaka jana.
 
Alisema hadi jana viongozi 10 wa JUMIKI wamefunguliwa mashitaka ya uharibifu wa mali na kuhatarisha usalama wa taifa.
 
Kamishina Mussa alisema wiki iliyopita jeshi la polisi limekamata mabomu 20 yenye uwezo wa kulipua nyumba au miamba.
 
Hata hivyo, hakufafanua zaidi kuhusu mabomu hayo lakini akasema polisi inaendelea na uchunguzi.
 
Kuhusu tathmini ya uhalifu katika kipindi cha mwaka 2012, Mussa alisema yapo mafanikio na changamato mbali mbali katika kupambana na uhalifu akihusisha na maendeleo ya sayansi na tekinolojia katika kupambana na uhalifu.
 
Alisema polisi Zanzibar imepunguza makosa ya uhalifu mkubwa kama mauaji kwa asilimia 11, ubakaji asilimia 0.6, wizi asilimia 46 dawa za kulevya asilimia 4.0, na makosa ya usalama barabarani asilimia 4.9 pamoja na kuchoma moto nyumbazikiwemo za polisi kuongeza operesheni za kupambana na uhalifu pamoja na biashara haramu ikiwemo dawa za kulevya na gongo.
 
Alitaja miundombinu mibovu ni changamoto kwa jeshi hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: