![]() |
| Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete. |
Mradi huo ungewawezesha wananchi wa mji wa Bunda na vitongaji vyake kupata maji safi na salama.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, hao wakiwamo baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Maji mjini Bunda, walidai kuwa mradi huo wenye thamani ya Sh. bilioni 35, ulitarajiwa kukamilika mwaka 2010.
Hata hivvyo, walisema hadi sasa hakuna juhudi zozote zinazofanywa katika kuwatatulia tatizo kubwa la maji linawakabili.
Walisema mradi huo ambao unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia Benki ya Dunia, ulianza kutekelezwa mwaka 2007 ikiwa ni ahadi ya Rais Kikwete aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Mmoja ya wajumbe hao wa Bodi ya Maji mjini Bunda, aliyetaka jina lake lisitajwe, alisema kampuni ya Nyakirang’ani ilipewa kazi ya kuchimba mtaro, kusambaza mabomba kutoka chanzo cha maji eneo ya Nyabehu hadi katika matangi makubwa mjini Bunda kwa Sh. bilioni 6.7, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika.
“Hapa hata sisi wajumbe tunashindwa kuhoji mradi huu kwanza unatekelezwa kisiasa zaidi...sasa tunashindwa kujua serikali inashindwa kuchukua hatua za kuhakikisha ahadi ya Rais inatekelezwa," alisema.
Mwananchi mwingine, Manyama Elias, mkazi wa Balili, alidai kuwa mradi huo umekuwa ukizungumzwa kwa kasi kubwa kila unapokaribia ujio wa kiongozi yoyote wa kitaifa na wakati wa uchaguzi mkuu, jambo linalonyesha kuwa hakuna dalili za dhati za kuwapatia wananchi wa Bunda maji kama ilivyokusudiwa na Rais Kikwete.
“Wakisikia anakuja waziri, ndiyo utaona juhudi za kuchimba mtaro zikifanyika, lakini akishaondoka tu, kimya…mfano walichimba mtaro mmoja waliposikia Rais anakuja lakini baada ya Rais kupita tu, walifukia mtaro kwa madai eti walikosea eneo la kuchimbwa. Je, hapo kuna dalili za wananchi kupata maji?,” Alihoji Elias.
Licha ya wananchi wa wilaya ya Bunda kuishi takriban kilomita tano tu kutoka Ziwa Victoria, lakini wamekuwa wakikabiliwa na tatizo kubwa la maji.
Hali hiyo huawafanya hata wagonjwa wakiwamo wajawazito kubeba maji yao kwenye ndoo wanapokwenda kupata matibabu ama kujifungua katika Hospitali Teule ya DDH mjini hapa.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mara, Esther Bulaya, akizungumzia tatizo hilo alisema serikali haijawa na nia ya dhati ya kuwaondolea kero ya maji wananchi wa Bunda.
Alisema ingawa amekuwa akilipigia kelele suala hilo kila mara, lakini kelele hizo hutafsiriwa na baadhi ya viongozi kuwa ni mbinu zake za kutafuta ubunge Jimbo la Bunda.
Hata hivyo, alisema kamwe hatakaa kimya wakati wananchi wa Bunda hasa akina mama wakizidi kuteseka kwa kukosa maji.
Mkurugenzi wa kampuni ya Nyakirang’ani, Mahuza Mmangi, anayemiliki kampuni hiyo iliyopewa zabuni ya kuchimba mtaro na kutandika mabomba kutoka chanzo cha maji hadi mjini Bunda, alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu malalamiko hayo ya wananchi, baada ya kuanza kuelezwa, alikata simu.
Hata hivyo, baada ya kutafutwa kwa mara nyingine mara kadhaa, hakupokea simu na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, pia hakujibu.
Mwishoni mwa mwaka jana, Mkurugenzi huyo wa Nyakirangani, alimueleza Naibu Waziri wa Maji, Injinia Benilith Mahenge, mradi huo umekuwa ukikumbwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kutopata fedha kwa wakati, jambo ambalo aliahidi kulifuatilia.
Awamu ya pili ya mradi huo itahusu usambazaji wa maji kwenda kwa wananchi baada ya maji hayo kufikishwa katika matangi yaliyopo mlima Kaswaka mjini hapa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:
Post a Comment