ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 14, 2013

CAG atoa ripoti Mamlaka ya Bandari

BODI ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), imekamilisha kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Sarikali (CAG), iliyochunguza ufisadi ndani ya taasisi hiyo ya umma na imepanga kumkabidhi Waziri wa Uchukuzi ripoti hiyo kwa hatua zaidi dhidi ya waliobainika kuhusika.
Mwishoni mwa mwaka jana, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliwasimamisha kazi vigogo kadhaa wa TPA kwa tuhuma za ufisadi.
Baada ya hatua hiyo, Waziri Mwakyembe alimtaka Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo na kuwasilisha ripoti yake kwa bodi kwa hatua zaidi.
Vigogo waliosimamishwa kazi katika sakata hilo na nyadhifa zao kwenye mabano ni Bakari Kilo (Mkurugenzi Uhandisi), Raymond Swai (Meneja Uhandisi), Frolence Nkya (Mkurugenzi wa Mipango) na Mahebe Machibya (Meneja Ununuzi na Ugavi).
Wengine ni Teophil Kimaro (Meneja Ununuzi), Mary Mhayaya (Ofisa Uhandisi Mkuu), Ayoub Kamti (Mkurugenzi wa Tehama), Mathew Antony (Meneja Kitengo cha Kontena) Maimuna Mrisho (Mkurugenzi wa Mifumo wa Menejimenti).
Pia wamo Fortunatus Sandalia (Askari Kitengo cha Ulinzi), Fadhili Ngolongo (Kitengo cha Marine), Mathew Antony (Meneja Kontena), Mohamed Abdullah (Kitengo cha Mafuta), Kilimba (Idara ya ulinzi) na Owen Rwebu.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Julius Mamiro zilieleza kuwa CAG ameshamaliza kazi yake na kuikabidhi ripoti hiyo kwa bodi ya TPA.
“Ripoti imeshakabidhiwa na bodi ya TPA imeshamaliza kazi ya kuipitia,” kilidokeza chanzo cha habari ndani ya TPA.
Alipoulizwa endapo ripoti hiyo imewatia hatiani baadhi ya vigogo alijibu,” Wapo, lakini siwezi kukueleza kwa undani ni nani na nani. Tusubiri tu, waziri atatangaza.”
Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Julius Mamiro mbali na kukiri ripoti hiyo kuwatia hatiani baadhi ya vigogo, alieleza kuwa bodi ya TPA imemaliza kazi ya kupitia ripoti hiyo, lakini akasema jukumu ya kuiweka hadharani ni ya waziri.
Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Julius Mamiro alilieleza gazeti hili kwa njia ya mtandao kwamba ripoti hizo, zinaonyesha kuwa baadhi ya wafanyakazi TPA wanahusika na ubadhirifu.
“Tumemaliza kupitia tuhuma hizo na sisi hatuna uwezo wa kuitoa taarifa hiyo kwa umma na hivi sasa (juzi) au kesho (jana) tutamkabidhi Waziri (Dk Mwakyembe) kwa hatua zaidi,” alisema Mamiro.
Hatua hiyo imekuja wiki tatu tangu bodi hiyo iahidi kuweka hadharani, hatua itakazochukua dhidi ya wafanyakazi hao, baada ya kuipitia ripoti ya CAG. Hali kadhalika, ripoti ya kamati iliyoundwa Agosti 27, mwaka jana na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe na ile ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Mwananchi

No comments: