Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekosoa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa kwa Taifa kuukaribisha Mwaka Mpya juzi.Chama hicho kimesema hotuba hiyo haikujibu masuala ya msingi kwa ajili ya mwelekeo wa taifa mwaka 2013, ikiwamo yanayohusu usalama wa nchi, kama vile kuundwa kwa tume huru ya kimahakama kuchunguza mauaji ya utatanishi yaliyotokea nchini katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Masuala mengine ambayo Chadema imedai kuwa ni ya muhimu hayakujibiwa na hotuba hiyo, yanahusu mchakato wa Katiba Mpya, haki za kiraia, hususan madai ya kutaka Daftari la Kudumu la Wapigakura (DKWK) liboreshwe ili kuwaingiza na kuwapa wananchi waliotimiza umri wa kupiga kura haki yao ya msingi ya kupiga kura.
Mengine yanahusu Mkutano ujao wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu na sera za kiuchumi.
Chama hicho kimesisitiza kuwa kitaendelea na azma yake ya kuutumia mwaka huu kuhamasisha nguvu ya umma kudai majibu hayo.
Pia kuendelea na msimamo wake wa kuiagiza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutumia njia za kibunge kuhakikisha tume huru ya uchaguzi inapatikana na sheria zinazosimamia uchaguzi zinarekebishwa kabla ya Katiba Mpya haijaundwa mwaka 2014.
Kauli hiyo ya Chadema ilitolewa na Mkurugenzi wake wa Habari na Uenezi, John Mnyika, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Mnyika alisema azma ya kuutumia mwaka huu kuhamasisha nguvu ya umma, ni utekelezaji wa maazimio 10, yaliyofikiwa na Kamati Kuu ya Chadema, katika mkutano wake waDesemba 15-16, 2012.
Alisema hotuba ya Rais Kikwete, mbali ya kugusia masuala tata yaliyoligubika taifa mwaka uliopita ili kuhakikisha kuwa mambo hayo hayajitokezi tena mwaka huu na siku za mbele, kwa kuweka misingi ya haki na uwajibikaji, ilipaswa pia kuwaeleza Watanzania tathmini ya nusu muhula tangu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010.
USALAMA WA NCHI
Mnyika alisema katika hotuba yake, Rais Kikwete ‘amegusia gusia’ na kutoa rai ya jumla juu ya uzingatiwaji wa utawala wa sheria.
Hata hivyo, lisema hakuonyesha serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuguswa na kuchukua hatua katika masuala mahsusi yanayoitia shakani hali ya usalama wa raia na nchi.
“Katika masuala ya usalama, Rais Kikwete amegusia matukio ya mikutano na maandamano pekee, huku akitoa rai ya jumla jumla kuwa utawala wa sheria uzingatiwe, lakini ameshindwa kuzingatia masuala ya msingi kabisa katika hilo,” alisema Mnyika na kuongeza:
“Mathalani, inaonesha Rais hajasoma ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambacho ni chombo cha serikali kilichofanya uchunguzi kwa tukio la (kijiji cha) Nyololo (Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa) la kifo cha (aliyekuwa mwandishi wa habari mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel, mkoani Iringa) Daudi Mwangosi.”
Alisema kama Rais Kikwete angekuwa ameisoma ripoti hiyo angeona jinsi Jeshi la Polisi lilivyovunja Sheria ya Vyama vya Siasa.
Mnyika alisema pia angeona jinsi Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, alivyovunja Sheria ya Sensa.
DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGAKURA
Alisema suala la uboreshwaji wa daftari hilo ili kuwapatia haki ya msingi ya kikatiba ya kupiga kura wananchi, ambao hawamo kwenye orodha hiyo kwa sababu mbalimbali, ni kubwa sana, lakini cha ajabu Rais hakuligusia kabisa.
Badala yake, alisema alichokifanya Rais Kikwete ni kuzungumzia tu kuhusu uandikishwaji wa vitambulisho vya uraia na sensa.
“Lakini hakukugusia kabisa suala la uandikishaji wapiga kura…serikali hii ya CCM haina habari na watu wanaokosa haki zao za msingi za kupiga kura. Kama suala ni ufinyu wa bajeti, rais ndiye mwenye mamlaka ya kupeleka bajeti bungeni, afanye hivyo,” alisema.Hata hivyo, Mnyika alitaka taarifa kuhusu vitambulisho vya taifa itolewe bungeni.
MCHAKATO WA KATIBA MPYA
Kuhusu mchakato wa katiba mpya, hususan marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Mnyika alisema chama hicho kimeshawasilisha mapendekezo yake ya muswada wa sheria hiyo juu ya namna ya uundwaji wa Baraza la Kutunga Katiba na kura za maoni kwa rasimu ya katiba mpya.
Alisema hawakubaliani na sheria hiyo kwa kuwa bado inaitambua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuwa msimamizi wa kura ya maoni ya katiba mpya wakati imegubikwa na malalamiko lukuki na ya muda mrefu.
Mnyika alisema pia kuwa sheria hiyo haikubaliki kutokana na kulitambua Bunge la sasa kuwa chombo cha kutunga Katiba Mpya.
Alisema Kamati Ndogo Maalum ya Kamati Kuu ya Chadema itakutana ndani ya kipindi cha wiki mbili kufanya tathmini zaidi kuhusu mchakato wa katiba mpya na baadaye itatoa taarifa kwa umma kuhusu suala hilo.
Aliwataka Watanzania walio wanachama na wapenzi wa Chadema kutuma maoni yao wanayopenda chama hicho kiyatoe kwenye msimamo wake kitakapokutana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Alisema Chadema inashangazwa na hatua ya Rais Kikwete kuwa msemaji wa tume hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba.
“Rais amesema kuwa tayari Tume imeshamaliza kukusanya maoni kwa mtu mmoja mmoja na ametoa hata ratiba ya tume…ni kama rais amekuwa msemaji wa tume. Tunaitaka sasa tume itoe taarifa kamili kwa umma,” alisema Mnyika.
Alisema tume inapaswa kutoa taarifa hiyo ili ijulikane ni Watanzania wangapi waliifikia na kutoa maoni yao kama ilivyofanya ilipohitimisha awamu ya tatu ya kazi yake ilipotangaza kuwa ilifikiwa na wananchi 900,000.
Alisema jambo hilo ni muhimu kwa tume kwa kuwa hadi inatangazwa kumaliza kukusanya maoni ya mtu mmoja mmoja, kuna Watanzania wengi, ambao hawajapata fursa ya kutoa maoni kwa tume hiyo.
SERA ZA UCHUMI
Akizungumzia gesi na maandamano ya wananchi wa Mtwara, Mnyika alisema Rais katika hotuba yake ameshindwa kujibu hoja za msingi za wananchi wa Mtwara, badala yake anataka kuonyesha kuwa wanasiasa wanaopaza sauti kwa niaba ya wananchi hao, si wazalendo, wakati si sahihi.
Aliitaka serikali kuwaeleza wananchi ni namna gani mapato ya gesi yanayokusanywa na serikali kuu yamewanufaisha Watanzania, kuanzia na wale walioko katika maeneo inakopatikana, tangu ilipoanza kuchimbwa mwaka 2004.
MBATIA
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ameitaka serikali kuunga mkono madai ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara kupinga kusafirishwa kwa gesi kutoka katika mkoa wao. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mbatia alisema madai ya wananchi wa Mtwara ni ya msingi, hivyo ni bora serikali ikayashughulikia badala ya kuyapuuzia.
Alisema serikali inatakiwa kutumia madai hayo kwa kufungua uwanja wa kujadili changamoto mbalimbali za maendeleo ya raslimali za taifa, ili kuangalia namna zinavyoweza kunufaisha wananchi.
“Naomba hili suala la madai ya wananchi wa Mtwara lichukuliwe kama changamoto mojawapo ya kutafakari namna ya kutumia gesi kwa manufaa ya taifa, suala la gesi si la wananchi wa mkoa huo peke yao ni la taifa zima,” alisema na kuongeza:
“Serikali isiwaone kama wahaini, bali ione kama wameibua mjadala, na hivyo itumie fursa hiyo kufungua uwanja wa kujadili maendeleo ya raslimali mbalimbali za nchi na namna zinavyoweza kuwanufaisha wananchi na taifa lao.” Mbatia alisema NCCR-Mageuzi inaunga mkono madai ya wananchi hao na kuitaka serikali kulitafutia ufumbuzi suala hilo kwa manufaa ya wananchi.
Hata hivyo, katika hotuba yake, Rais Kikwete aliwahakikishia wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ambako gesi asilia imegunduliwa au popote itakapogundulika, kuwa watanufaika sawia na katu hawatasahaulika.
Alisema rai yao ya kutaka na wao wanufaike inakubalika na serikali inajiandaa hivyo. “Viongozi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa mfano, wanajua maelekezo niliyotoa kuhusu kuiandaa miji ya Mtwara na Lindi kupokea uchumi wa gesi,” alisema na kuongeza:
“Lakini sharti la kutaka gesi isisafirishwe kwenda kokote na kwamba kila kitu kifanyike kwao halikubaliki. Rasilimali inayopatikana popote katika nchi hii ni mali ya taifa zima na hutumika kwa manufaa ya taifa. Katu siyo mali ya watu wa pale ilipogundulika au pale shughuli hizo zinapofanyika.”
Alisema jumla ya makusanyo ya mapato yatokayo sehemu zote za nchi na kutokana na vyanzo mbalimbali ndiyo yanayotumika kuhudumia watu wote po pote walipo.
Rais Kikwete alisema tangu mwaka 2010 gesi nyingi imegundulika baharini na nchi kavu katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani na kwamba utafutaji bado unaendelea na kuna matumaini kuwa gesi nyingi zaidi huenda ikagundulika. Alisema hivi sasa serikali inaandaa sera na sheria mpya ya gesi ili kuboresha zinazotumika wakati huu. “Nia yetu ni kutaka kuhakikisha kuwa rasilimali hii adhimu inasimamiwa vizuri kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake pamoja na kulinda maslahi ya wawekezaji,” alisema.
VITAMBULISHO
Kuhusu vitambulisho vya Taifa, Rais Kikwete alisema serikali imeanza zoezi la kusajili watu na makazi kwa ajili ya kuandaa kutoa Vitambulisho vya Taifa kuanzia mwaka 2013 na kwamba Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ilifanya zoezi la majaribio katika mkoa wa Dar es Salaam na wilaya ya Kilombero ambalo lilifanikiwa.
Alisema hivi sasa wanaendelea na zoezi hilo Zanzibar na kufafanua kuwa maandalizi kwa ajili ya kutekeleza zoezi la kutoa vitambulisho nchi nzima kuanzia mwaka 2013 yanakwenda vizuri. Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Rais Kikwete alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea vyema na kuwa kwa sasa imekamilisha hatua ya kwanza ya kukusanya maoni ya mtu mmoja mmoja katika Mikoa yote nchini.
Akizungumzia marekebisho ya sheria, Rais Kikwete alisema yalifanyika mazungumzo baina ya serikali, vyama vya siasa na wadau wengine juu ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. “Tulikubaliana tushughulikie marekebisho ya Sheria hiyo hatua kwa hatua. Tulikubaliana kuanza na mambo yanayohusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi ili Tume iundwe na ianze kazi. Baada ya hapo tuangalie vipengele vinavyohusu Bunge Maalum na Kura ya Maoni,” alisema.
Alisema walifanya hivyo kuhusu Tume ya Katiba na sasa wanajiandaa kuanza mazungumzo kuhusu ngwe iliyobaki yaani, Bunge Maalum na Kura ya Maoni.
Kuhusu Kura ya Maoni, alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaelekeza kuwa Kura ya Maoni itatungiwa Sheria yake maalum.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment