ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 2, 2013

Ving'amuzi vyawatesa wakazi Dar

Mkurugenzi wa mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy
NA RICHARD MAKORE
Kuzimwa kwa mitambo ya kurushia matangazo ya televisheni kwa mfumo wa analojia, kumezua utata baada ya wakazi wengi wa Mkoa wa Dar es Salaam kushindwa kupata matangazo.

Mitambo hiyo ilizimwa juzi usiku kwa maelekezo ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Baadhi ya wakazi wa jijini Dar es Salaam, wamesema hawapati matangazo ya televisheni licha ya kununua ving’amuzi.
Aidha, wamesema chaneli tano zilizopewa leseni na serikali kuendelea kurusha matangazo yao, nazo zinaonyesha chenga chenga. Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili jana, walidai kuwa mfumo huo umeleta usumbufu mkubwa kwao.

“Mimi mwenyewe nimekumbwa na tatizo hili tangu jana baada ya mitambo hiyo kuzimwa, sipati tena zile chaneli tano ambazo serikali ilisema ni lazima zionyeshwe ili Watanzania waendelee kuona hata kama vocha zao zitakuwa zimekwisha,” alisema mkazi mmoja wa jijini Dar es Salaam, ambaye hata hivyo, hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Alidai kwamba kituo cha TBC tu ndiyo kilikuwa kinaonyesha na kusema kuwa kama ndiyo hivyo, wananchi wengi watakosa matangazo.

Wakati wananchi hao wakitoa malalamiko yao, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy, aliliambia NIPASHE kwa njia ya simu jana kuwa, kinachowafanya wananchi washindwe kupata matangazo ni wao wenyewe kushindwa kuunganisha ving’amuzi.

Mungy aliwataka wananchi kubadilika na kutumia mafundi wa kampuni zinazouza ving’amuzi badala ya wao wenyewe kujigeuza mafundi.

Mungy alisema huduma ya kufungiwa king’amuzi inatolewa bure na hakuna haja ya mtu kupanda juu ya nyumba yake na kuanza kufunga bila kujua anachokifunga.

“Kila kitu kinaenda vizuri na jana tulizunguka maeneo mbalimbali kuangalia zoezi hili na tumebaini tatizo kuwa ni watu hawajui kufunga hivi ving’amuzi,’’ alisema Mungy.

Juzi, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari, alisema hata kama mitambo hiyo itazimwa, lakini chaneli tano za hapa nchini zitaendelea kurusha matangazo yake kama kawaida.

DAR WAGOMBEA VING'AMUZI

Wakati zoezi la kuhamia dijitali likiendelea, jana mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walifurika katika maduka mbalimbali ya mawakala wa kampuni ya Star Times kuendelea kununua ving’amuzi kwa ajili ya televisheni zao.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi hao walikosoa huduma zilizokuwa zikitolewa na mawakala hao kwa madai kwamba hazikidhi kiwango kinachotakiwa.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, walieleza kwamba baada ya kuweka ving'amuzi kwenye televisheni zao, pamekuwa pakijitokeza tatizo la picha na sauti hasa kwa wale waliolipia chaneli chache.

Mmoja wa wananchi hao, Esther Msigwa, alisema kuwa tangu amenunua king’amuzi chake, hajakitumia kutokana na matatizo kama hayo.

“King'amuzi kinasumbua, sipati picha wala sauti, vile vile tuliambiwa bei yake ni Sh. 39,000, lakini tunauziwa Sh. 48,000," alisema.

Akijibu tuhuma hizo, Afisa Masoko wa kampuni ya Star Times, Erick Cyprian, alisema watu walinukuu vibaya kuhusiana na suala la punguzo la manunuzi kwa kipindi cha kuelekea sikukuu.

“Punguzo la manunuzi ya king'amuzi halihusiani na muda wa hewani, hivyo wengi wao wanadhani wakishanunua king'amuzi kwa bei ya Sh. 39,0000, watapata muda wa maongezi moja kwa moja,” alisema Cyprian.

Hata hivyo, jitihada za NIPASHE za kuwatafuta viongozi wa DSTV kueleza namna walivyojipanga kuonyesha matangazo ya chaneli za ndani zilishindikana.

Simu ya Ofisa Mawasiliano, wake, Barbara Kambogi, ilikuwa inaita bila kupokelewa.

No comments: