Juzi, katika salamu zake za Mwaka Mpya, Rais Kikwete alipinga madai ya wakazi wa Mikoa ya Kusini kutaka gesi hiyo isisafirishwe kwenda Dar es Salaam, akisema madai hayo hayakubaliki popote.“Rasilimali inayopatikana popote katika nchi hii ni mali ya taifa zima na hutumika kwa manufaa ya taifa na katu si mali ya watu wa pale ilipogundulika au pale shughuli inapofanyika,” alisema Rais Kikwete.
Viongozi hao mbali na kuonyesha misimamo ya kuzuia nishati hiyo hata kabla ya kauli hiyo ya Rais Kikwete, jana walisisitiza kwa nyakati tofauti kwamba, wataendelea kuunga mkono jitihada za wananchi kupinga usafirishwaji wake kwa kuwa hiyo ni haki yao.
Murji alisema yupo tayari kuvuliwa ubunge kwa kutetea masilahi ya Wanamtwara wanaopinga gesi hiyo inayovunwa katika Kijiji cha Msimbati, mkoani Mtwara huku Chinkawene akisema msimamo wa chama chake ni kuungana na wananchi kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam.
Alisema Serikali inapaswa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme mkoani Mtwara badala ya Dar es Salaam... “Tulipoona hali inakuwa tete, niliitisha kikao cha Kamati ya Siasa kujadili nini msimamo wa chama katika hili. Kamati ya Siasa wakasema hawawezi kukisemea chama kwa sababu chama ni wanachama, hivyo nikaitisha kikao cha Halmashauri Kuu ambapo pia tuliwaalika mabalozi wa mitaa.”
“Katika kikao hicho, wajumbe walipinga kwa nguvu zote suala la gesi kupelekwa Dar es Salaam. Wakaniambia niseme msimamo wao kuwa hawataki gesi iende Dar es Salaam hadi pale masilahi ya Wanamtwara yatakapowekwa wazi na Serikali.”
Mwenyekiti huyo alisema kwa maana hiyo, msimamo huo si wake binafsi, bali ni maazimio ya vikao halali vya chama hicho vinavyowakilisha wanachama na kwamba historia ya Mikoa ya Kusini jinsi ilivyonyimwa maendeleo ilitumiwa na wajumbe kujenga hoja hiyo.
“Wakati sisi hatuna umeme hakuna aliyefirikia kutuunganisha kwenye gridi ya Taifa… Barabara ya kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam miaka 51 ya Uhuru sasa, haijakamilika. Lakini bomba wanataka kujenga kwa miezi 18. Hivi kuna Watanzania muhimu zaidi ya wengine?” alihoji Chinkawene akinukuu kauli za wajumbe wa kikao hicho na kuongeza:
“Walizungumza mambo mengi, suala la kung’olewa kwa reli, kukatazwa kulima pamba, kuuawa kwa kilimo cha karanga na mkonge. Haya yote wanadai yamesababisha mkoa uendelee kuwa maskini na kwamba tumaini lao limebaki kwenye gesi. Wamesema wapo pamoja na wananchi.”
Murji kwa upande wake, alisema amekutana na umoja wa vyama vya siasa vilivyoratibu maandamano ya kupinga suala hilo na kuwapongeza kwa kazi nzuri akisema wananchi wana haki ya kutetea rasilimali yao.
Alisema yeye si mbunge anayewakilisha mawazo yake bungeni, bali ya wananchi... “Hivyo ni bora niungane na wananchi wangu kutetea masilahi yao; liwalo na liwe.”
“Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa kwa ujasiri na uthubutu wenu wa kutetea rasilimali hii (gesi)… Tusidharau hata kidogo malalamiko ya wananchi…” alisema Murji huku akishangiliwa na wajumbe na kuongeza:
“Nipo pamoja nanyi na hata ikibidi nivue ubunge, nipo tayari kufanya hivyo kwa masilahi ya wananchi….”
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile alisema si sahihi kuwalaumu wananchi wanaopinga kupelekwa kwa gesi hiyo Dar es Salaam kwa kuwa hawajaelimishwa.
“Ni kweli hatuwezi kueleweka kama gesi inakwenda Dar es Salaam wakati hawajui watanufaikaje. Hayo si maswali madogo, lazima yajibiwe,” alisema alipokuwa akifungua Baraza la Majadiliano baina ya uongozi na vyama vya wafanyakazi wa Bandari ya Mtwara mwishoni mwa wiki.
Alipoulizwa jana kama amefuta kauli yake hiyo hata baada ya Rais Kikwete kutoa mwongozo wake alijibu: “Nilisema ni muhimu wananchi waelimishwe, wasilaumiwe tu, kwani wameelimishwa tayari?… Hata Rais (Kikwete) hajakataa kuelimisha.”
Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Uledi Abdallah ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mtwara Mjini, alimpongeza mbunge huyo kwa kuungana na wananchi hao na kuahidi kumpa ushirikiano huku akisisitiza kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kutanguliza masilahi ya wengi.
“Tumefarijika kuona wenzetu wa CCM na wewe mbunge wetu umeungana na sisi…. Tofauti zetu za kisiasa tuziweke kando, tusimamie rasilimali yetu,” alisema Uledi.
Mbunge wa Vunjo (TLP), Agustine Mrema ameunga mkono harakati za wakazi hao wa Mikoa ya Kusini kushinikiza gesi isisafirishwe kwenda Dar es Salaam akisema wana haki ya kudai maendeleo katika maeneo yao kwanza.
“Si kwamba wakazi hao ni wachoyo, hapana wamechoka ni kama Mungu amewaamsha katika usingizi, sasa wanataka haki yao,” alisema Mrema.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema wananchi wa Mtwara na Lindi wana haki ya kuhoji jinsi watakavyonufaika na gesi kwa sababu baadhi ya viongozi wa Tanzania wana tabia ya kutaka kujinufaisha wao kwanza.
“Baada ya wananchi kuibua hoja kuhusu gesi, baadhi ya viongozi wa Serikali wameibuka na kuwaita wahaini, kauli hizi zinaweza kuligawa taifa, kila mwananchi ana haki ya kuhoji juu ya rasilimali za taifa,” alisema.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika ameitaka Serikali kueleza matumizi ya mapato yanayotokana na gesi iliyogundulika katika Mkoa wa Mtwara tangu mwaka 2004 ili wananchi waweze kufahamu wananufaika vipi na rasilimali hiyo.
Mnyika alisema madai ya wakazi wa mikoa hiyo kupinga gesi isisafirishwe kwenda Dar es Salaam ni ya msingi kwani hawaoni faida yake.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema madai hayo ni mwanzo wa kuimega nchi vipandevipande kwa faida ya wachache.
“Hii si gesi yao, ni ya Watanzania wote, hatupaswi kuanza kuimega nchi katika vipande kwani kila eneo lenye maendeleo halijayapata kivyakevyake, bali ni mpangilio na mgawanyo bora wa rasilimali,” alisema.
Mbunge wa Masasi Mjini (CCM), Mariam Kasembe alisema anaungana na Rais Kikwete kupinga madai ya wakazi wa Kusini na kusema kuwa gesi kupelekwa Dar es Salaam si kigezo cha maeneo hayo kukosa maendeleo.
Wiki iliyopita, Umoja wa vyama vya siasa mkoani Mtwara uliitisha maandamano kupinga gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, wakitaka ibaki mkoani humo kwa faida ya wakazi wake. Umoja huo ambao awali ulikuwa ni wa vyama vinane vya Chadema, NCCR-Mageuzi, SAU, TLP, APPT Maendeleo, ADC, VDP na DP, sasa unaungwa mkono na CCM na CUF.
Habari hii imeandikwa na Abdallah Bakari (Mtwara), Florence Majani, Fidelis Butahe na Aidan Mhando (Dar).
No comments:
Post a Comment