ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 10, 2013

DONDOO ZA AFYA: KUTOKWA NA UCHAFU WA KISAMAKI


KUTOKWA na uchafu wa kisamaki ni moja ya magonjwa yanayoshambulia sehemu za siri za mwanamke na kusababisha atokwe na majimaji meupe au uchafu wenye harufu kama ya samaki aliyeoza.
Pia ugonjwa huu huchanganya sana madaktari kwa kuwa unafanana na ugonjwa wa fangasi sehemu za siri za mwanamke pamoja na ugonjwa mwingine unaoitwa kitaalamu kama Tricomonoassis.


NINI MAANA YA UGONJWA HUU?
Ni maambukizi ya vijidudu mbalimbali vinavyoshambulia sehemu za siri za mwanamke, vijidudu hivi kikawaida huishi sehemu za siri za mwanamke bila kumletea ugonjwa.
Kwa kawaida sehemu za siri kuna aina mbili za wadudu, moja ni wadudu wanaolinda wenye madhara wasiingie sehemu za siri, hawa huitwa wadudu wazuri.
Lakini wapo wadudu wanaoingia na kushambulia mwili ambao huitwa ni wadudu wabaya.
Wadudu wanaosababisha ugonjwa huu wa kisamaki huanza taratibu sana bila hata mwanamke kujijua na huendelea kukua na kushambulia sehemu za siri mpaka mama anakuja kugundua harufu baada ya kupita muda mrefu .
Kwa hiyo inatakiwa kuwa na mlingano (balance) kati ya wadudu wabaya na wazuri kama wadudu wabaya watazidi nguvu wadudu wazuri, ugonjwa hujitokeza.
Vifuatazo ni vitu vinavyochangia maambukizi ya vijidudu.
Kuwa na uhusiano wa kimapenzi na zaidi ya mtu mmoja, wavutaji wa sigara kuvuta kupita kiasi na wale wanaojisafisha sehemu za siri kwa kutumia madawa makali kama Strong Ditto.

Dalili kubwa ya ugonjwa huu wa kisamaki ni kutokwa uchafu ambao unaweza kuwa majimaji au uchafu mzito mweupe au wa njano ambao una harufu ya kisamaki na mara nyingi harufu hii huwa kali baada ya kumaliza tendo la ndoa.
Utafiti unaonesha kuwa asilimia 50 ya wanawake huwa wamepata maambukizi lakini hawajitambui.

UCHUNGUZI NA USHAURI
Ugonjwa huu huambatana na magonjwa mengine ya zinaa hivyo, ni vyema kila mwanamke akiona dalili ya uchafu awahi kwenda hospitali na kumuona daktari ili apate tiba ya uhakika baada ya kupimwa.
Ugonjwa hugundulika vizuri hospitali ambapo daktari hupata maelezo mazuri kutoka kwa mgonjwa kisha vipimo huchukuliwa na kugundua ugonjwa au wadudu wa aina gani waliosababisha tatizo hilo.

TIBA
Matibabu ya uhakika hupatikana hospitali na mgonjwa hupona haraka ndani ya siku 3 hadi 6 kwani uchafu wenye harufu ya kisamaki hutoweka.

No comments: