
Jamani! Hakuna anayeweza kubisha kwamba elimu ni ufunguo wa maisha. Mtu yeyote anapokosa elimu ni kama yuko katika usiku wa giza kwani atakuwa hawezi kufanya lolote likaonekana katika maisha yake.
Wazazi wanatakiwa kuhakikisha kwamba wanawapatia elimu bora watoto wao kwa gharama yoyote wakijua kwamba kwa kufanya hivyo ndivyo maisha yao yatakavyokuwa mazuri.
Mipango madhubuti juu ya elimu sahihi kwa watoto inahitajika ili kuwahakikishia usalama na mafanikio katika kipindi ambacho watakuwepo hapa duniani. Tambua kwamba watoto hawana wanachojua kuhusu maisha yao hasa wanapokuwa katika umri mdogo.
Hawajui nini watakumbana nacho katika maisha yao, hawajui wajiandae vipi ili waweze kuja kuishi maisha mazuri kama wanavyoishi wazazi wao ama watu wengine wa karibu yao.
Baadhi yao wanadhani wamekuja hapa duniani kucheza tu. Ni jukumu lako wewe mzazi kumwandaa mwanao vizuri kwa kumpeleka shuleni katika umri unaostahili.
Wapo baadhi ya wazazi ambao kwa kujua kwao umuhimu wa elimu wanadiriki kujinyima kula, kuvaa vizuri na kuishi maisha ya raha mustarehe na kutumia fedha zao wanazozipata kwa uchache kuwapeleka watoto wao shuleni ili wakapate elimu bora.
Lakini kuna ambao wanadhani kutumia pesa zao kuwapeleka watoto wao shuleni ni kuzipoteza. Hao ndiyo wanaona ni heri kuwafanyisha kazi watoto wakiwa na umri mdogo kuliko kuwapeleka shule. Naamini kabisa wanaofanya hivyo hawajui umuhimu wa elimu kwa watoto hivyo si vibaya kama nitawakumbushia juu ya hilo.
Kwa sasa elimu ndiyo silaha madhubuti ya kuweza kuitumia katika kutafuta ajira kama siyo kujiajiri. Katika ulimwengu huu elimu si kujua kuandika na kusoma tu, bali ni zaidi ya hivyo. Ndiyo maana nafasi nyingi za kazi zinazotangazwa kunakuwa na vigezo.
Elimu ni pesa, elimu ni silaha ya mafanikio pia elimu ni ufunguo wa maisha. Tunafahamu kwamba shuleni kunafundisha masomo mengi ambayo yanagusa nyanja mbalimbali za maisha.
Mwanao anapokwenda shule anapata maarifa na upeo mkubwa wa kuelewa mambo na hivyo kumweka pia katika mazingira mazuri ya kutoa mawazo aliyonayo, kufanya maamuzi sahihi na kuitumia elimu yake kuendesha maisha kwa ufanisi wa hali ya juu.Hata kama watakosa ajira lakini naamini kabisa kwa elimu waliyonayo wanaweza kuwa wabunifu kiasi cha kuweza kubuni njia mbadala ya kuweza kuendesha maisha yao. Mwenye elimu hata siku moja hawezi kushindwa maisha na kama atashindwa basi atakuwa hajaelimika.
Ni vyema wazazi wakawa wachunguzi wa kazi gani ambazo watoto wao wanakuwa na mwelekeo nazo ili waweze kuelekeza jitihada zao huko. Kama unaona mwanao anapendelea mambo ya ufundi, mpeleke katika shule za ufundi, kama anaonesha kupendelea mambo ya usanii mpeleke kwenye shule zinazofundisha mambo ya sanaa.
Itaendelea wiki ijayo.
GPL
1 comment:
Beautifully stated. Luv it
Post a Comment