
Umri ambao umewekwa wa kuwaandikisha watoto darasa la kwanza ni kuanzia miaka 7 kwa sasa lakini ni vizuri pia ukampeleka mwanao katika shule za chekechea akiwa na umri mdogo zaidi ya hapo ili kumjengea mazingira mazuri pindi atakapokuja kuanza shule rasmi.
Kwa kuzingatia ubora wa elimu, angalia shule ambayo unaamini wanafunzi wanaotoka hapo wanafanya vizuri. Ndiyo maana wazazi wengine kabla ya kumpeleka mwanaye katika shule fulani huulizia kwanza historia ya shule hiyo. Je, ina rekodi ya kufaulisha?
Wanaofanya hivyo wasionekane wana makuzi, hapana! Naamini wana haki ya kufanya hivyo. Usimpeleke mwanao shule ilimradi umempeleka, angalia na uwezekano wa mwanao kuweza kupata elimu bora.
Hali ya sasa imebadilika, elimu ni fedha, bila kuwa nayo ya kutosha huwezi kufanya maamuzi sahihi juu ya elimu bora kwa mwanao. Hebu jiulize mbona serikali imepitisha gharama nafuu ya elimu kwenye shule zake lakini baadhi ya wazazi wanaamua kuwapeleka watoto wao katika shule za kimataifa ambazo wanalipa mamilioni ya fedha?
Nadhani wanafanya hivyo wakiamini huko wanaweza kupata elimu bora zaidi. Sisemi kwamba wanaokwenda kwenye shule za serikali wanafanya vibaya, hapana! Wapo ambao wanakwenda kwenye shule hizo na wanafanya vizuri zaidi kuliko wale wanaosoma katika shule za kimataifa.
Cha msingi ni kuhakikisha kwamba kwa gharama yoyote mtoto wako anakwenda shule na anapata elimu ambayo unaamini hatakuja kupata matatizo yatakayokana na ukosefu wa elimu katika maisha yake.
Mzazi uwe mfuatiliaji wa karibu sana wa maendeleo ya mwanao shuleni. Unapoona ni mabaya, usife moyo, mkalishe chini na muulize
tatizo hasa ni nini?
Kama utagundua kwamba tatizo siyo yeye bali ni mazingira ya shule anayosoma, fanya jitihada za haraka kumhamisha. Wapo watoto ambao wamekuwa wakifanya vibaya sana wanapokuwa katika shule fulani lakini wanapohamishiwa shule nyingine wanafanya vizuri.
Hivyo ifahamike kwamba wakati mwingine kufanya vibaya kwa mwanao kunatokana na mazingira ya shule aliyopo lakini wanaweza kuwa vichwa kama watakuwa katika shule nyingine.
Sasa hivi zipo shule nyingi zinazoanzishwa. Nyingine zipo uchochoroni ambazo zina walimu wasioweza kutoa elimu inayostahili kwa mwanao. Mwenye macho haambiwi tazama, naamini kabisa unaona jinsi gani waliokosa elimu wanavyopata tabu katika maisha yao hivyo ni uamuzi wako.
Mimi nashauri mzazi kutilia maanami suala la elimu kwa mwanaye kwani elimu ni kila kitu katika maisha ya sasa.
Mwisho kabisa nisisitize kwamba, wazazi watambue elimu haina mwisho hivyo kama mazingira yataruhusu, wasifikie mahali wakasema; ‘mwanangu elimu uliyopata inatosha.’
Mtie moyo ili ikiwezekana aje kuwa na shahada ya Ph.D. Naamini kwa kufikia hatua hiyo kwanza itakuwa ni sifa kwako wewe kama mzazi na pia utamfanya mwanao aheshimike katika jamii huku akiyafurahia maisha yake.
Kwa leo niishie hapa. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.
GPL
No comments:
Post a Comment