ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 19, 2013

HESHIMU MUDA KATIKA MAPENZI, USIUPOTEZE BURE

KAMA ilivyo ada, tumekutana tena, yangu hali namshukuru Mungu, nina imani na wewe mwenzangu u mzima wa afya njema, ndiyo maana leo tupo pamoja.
Leo nataka kuzungumzia umuhimu wa muda katika uhusiano. Kumekuwa na mambo mengi yaliyo wazi, lakini watu wengi wameshindwa kukubaliana nayo kutokana na udhaifu wa moyo na kutegemea huruma ya upande wa pili.

Kuna jambo moja limeleta matatizo sana katika uhusiano na mwisho wake huwa maumivu kwa wapendanao.
Nimekuwa nikipata maswali mengi ambayo kwa upande wangu yameniwia vigumu kutoa majibu kwa vile yapo kifamilia zaidi. Waswahili wanasema mapenzi hayajali dini, rangi wala kabila. Katika haya matatu kuna moja naweza kupingana nalo kama halikufanyiwa matayarisho mapema.
Suala la dini limekuwa kikwazo kwa watu wengi, penzi linapoanza mnajikuta mnapendana lakini tofauti yenu ni dini. Zipo familia ambazo huwa haziingilii uamuzi wa mtoto kwa kitu anachotaka kukifanya,
maadamu amevuka miaka 18.
Familia hizi husaidia kukamilisha ule usemi kuwa mapenzi hayajali rangi, kabila wala dini. Sehemu hii tumeona watoto wa kike wengi ndiyo huwafuata wanaume, japo wapo wanaume wanaowafuata wanawake lakini ni asilimia tano. Lakini kwa upande wa familia zenye msimamo mkali, hapo ndipo tatizo hutokea kwa kila moja kuvutia kwake, kama hawakubaliani ndipo penzi huvunjika.

Nini nia ya makala haya?
Kumekuwa na tatizo la watu kukaa muda mrefu katika uhusiano wakiamini mmoja atakubali kumfuata mwenzake. Lakini mwisho wazazi wanasimama kidete kugomea wazo lao la mmoja kutaka kumfuata mwenzake, kwa kuamini ni makosa kwa mujibu wa dini yao.

Inawezekana hilo umeliona mapema lakini unajipa moyo labda ukibeba ujauzito unaweza kukubaliwa na wazazi wako ubadili dini. Hilo ni wazo la kijinga kwa vile mapenzi mazuri yanataka kufuata taratibu zote na mwisho kupata baraka za wazazi wa pande zote.

Sawa, una mpenzi dini tofauti, kama mmependana kabla ya kuanzisha uhusiano kaeni chini na kukubaliana mtaishi maisha gani kama dini zenu ni tofauti.
Baada ya makubaliano ambayo yatawashirikisha watu wenye busara, muafaka utakapopatikana kupitia pande zote mbili, hapo ruksa kuwa karibu na mwenzako kwa ajili ya maandalizi ya ndoa yenu.
Wengi wamekuwa wakifanya makosa kwa kukaa na mpenzi zaidi ya miaka kumi lakini mwisho wazazi wanagoma katika suala la ndoa kwa vile dini tofauti. Baada ya tatizo kama hilo kutokea, unaniomba ushauri, nikushauri nini? Jambo kama hilo lazima litahusu familia za pande mbili na wala si mtu wa nje.

Kwa nini unacheza patapotea ya mapenzi? Unaufahamu vizuri msimamo wa familia yako, bado unampa mtu matumaini labda watabadilika. Kubadili dini kwa mtu mmoja kumfuata mwenzake si jambo geni, lakini unajua kabisa uwezekano wa kukubaliwa haupo, kwa nini upoteze muda kwa jambo lisilowezekana?
Inawezekana wote mnapendana mapenzi ya dhati, lakini familia zenu hazipo tayari kuhusu suala la kubadili dini. Heshimuni muda katika mapenzi, usipotee bure kwa jambo ambalo unajua kabisa halina mwisho mzuri. Kwa nini msiachane mapema ili kila mmoja amtafute mwingine ambaye atakuwa hana vikwazo, kuliko kukaa muda mrefu mnakuja kuachana baada ya mmoja kulazimishwa kuoa kwa vile muda wa kuoa au kuolewa umefika! 

Matokeo yake unajikuta ukiujutia muda wako wakati jambo hili lilitakiwa kufanyika mapema. Usikubali kucheza patapotea kwa jambo lililo wazi.

Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo.
CHANZO: GPL

No comments: