
Inawezekana kweli ameyafanya maisha yako kuwa na furaha lakini hiyo furaha anaidumisha vipi? Isije ikawa anakufurahisha pale tu anapokuwa na shida zake, pindi unapomtatulia huyo anakwenda zake, akirudi tena ujue ana shida.
Mathalan, mwenzi wako anatimiza kila kitu unachohitaji. Anageuka mtu wa ndiyo na kutekeleza kila ombi lako. Wewe unajiona unatisha kwa kuona kwamba mwenzi wako anakunyenyekea unavyotaka. Kumbe mwenzako ana malengo yake, mkishaingia faragha na kukidhi haja zake, ule unyenyekevu wake wote unaondoka, anarudi kuwa yuleyule.
Mwenzi wako ana asili ya kiburi, mara nyingi ombi lako la kukutana naye faragha hulitolea nje kwa maelezo kwamba eti huwa hajisikii. Lakini anapokuwa na shida ya fedha, anakuwa mpole, kiburi chake chote kinapotea. Hakawii kukwambia ana hamu na wewe. Akili ikae kichwani kwako.
Mfano: Msomaji wangu ambaye naomba nimtaje kwa jina moja la Bryson, aliwahi kunilalamikia kwa njia ya simu kuhusu tabia ya mke wake. Akadai kuwa wakati mwingine hafikirii kama aliyemuoa ni mke wake, ila changudoa anayetaka kuvuna kwake. Akaenda mbali zaidi kwa kusema anahisi mkewe ana kidumu nje ya ndoa yake.
Akaeleza kwamba yeye na mkewe tofauti yao kubwa huwa ni usiku wakati wa kulala. Kila anapomhitaji mkewe hukutana na vizingiti visivyokwisha. Visingizio ni vingi, mara ooh, leo nilifanya kazi nyingi, nimechoka sana, siku nyingine ooh, leo nimezunguka sana, hapa mapaja yote yamechubuka.
Kwa mujibu wa Bryson, visingizio vya mkewe huwa haviishi. Pale ambapo husisitiza, hutokea ugomvi mkubwa kiasi kwamba hata majirani hutambua kwamba kuna kimbembe chumbani kwao. Hii ndiyo inamfanya Bryson ahisi kwamba mkewe ana kidumu pembeni ambacho hutimiza haja zake.
Bryson akaendelea kueleza kuwa inapotokea mkewe ana shida ya fedha, siku hiyo ataanza kumtumia SMS za mapenzi siku nzima. Atamsisitiza awahi kurudi nyumbani kwamba ana hamu naye, wakati mwingine hudanganya analia kwa madai eti, ‘amemmisi’ kupitiliza.
Anaweza kuandika SMS yenye sura hii: “Mume wangu leo uje na shilingi 100,000, kuna nguo nataka ninunue, ukija nayo usiku nitakupa.” Wakati Bryson anatafakari jinsi ya kujibu, mkewe anatuma SMS nyingine: “Yaani tuache utani, ukweli nimekumisi. Leo jiandae kabisa, lazima tukeshe.”
Bryson akichelewa kujibu, mkewe ataandika SMS nyingine: “Nakupenda sana mume wangu. Usichelewe kurudi, leo nina mzuka wa ajabu na wewe, si unajua ni wewe ndiye unayenipatia?” Punde tena, SMS nyingine: “Mbona hunijibu, najisikia vibaya mpaka nalia peke yangu, hiyo tabia gani ya kunichunia?”
Msomaji wangu huyo akaeleza kwamba kimbembe hujiri pale anapofika nyumbani. Hukuta kila kitu kimebadilika.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment