mchezaji Shaaban Kado wa Coastal Union ya Tanga kwa mwaka mmoja.
Klabu za Yanga na Mtibwa Sugar zimeendelea kuzozana kuhusiana na mchezaji Shaaban Kado baada ya kipa huyo kusaini mkataba wa kuichezea Coastal Union ya Tanga kwa mwaka mmoja.
Kipa huyo ambaye aliichezea Mtibwa kwa mkopo katika mzunguko wa kwanza wa msimu akitokea Yanga, amekuwa chanzo cha malumbano baina ya klabu hizo; ambapo ‘Wanajangwani’ wanadai kuwa wana haki ya kumuuza kokote kwavile ni mchezaji wao halali huku ‘wakata miwa’ wa Mtibwa wakisisitiza kuwa anapaswa kuendelea kubaki kwao kwavile walimtwaa kwa mkataba wa kuichezea hadi mwisho wa msimu.
Hata hivyo, akizungumza na NIPASHE jana,
Kado alisema kuwa tayari ameshasaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Coastal iliyowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara mwaka 1988.
“Ni kweli nimesaini mkataba wa mwaka mmoja katika klabu ya Coastal… na nimeshaanza kufanya nao mazoezi,” alisema Kado.
Akieleza zaidi, kipa huyo alisema: “Kulikuwa na mvutano kati ya Yanga na Mtibwa juu yangu, lakini kila kitu kuhusiana na hilo nimewaachia wao. Naamini watamalizana,” alisema Kado.
Mratibu wa Mtibwa, Jamal Bayser, aliambia NIPASHE jana kuwa wameshangazwa na kitendo cha Yanga kumuuza mchezaji huyo il-hali walikubaliana kuichezea timu yao (Mtibwa) hadi mwishoni mwa msimu huu wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Bayser alisema kuwa tayari klabu yake imewasilisha malalamiko katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusiana na suala la kipa huyo ambaye aliwahi kuichezea Mtibwa kabla ya kuuzwa Yanga na baadaye kurejea tena klabuni hapo kwa mkopo.
“Inashangaza sana kuona klabu zinasajili wachezaji kinyume na utaratibu. Kulingana na makubaliano yetu na Yanga, Kado anatakiwa kuitumikia Mtibwa hadi mwishoni mwa msimu huu,” alisema Bayser.
“Tumeshaandika barua TFF, maana tulikubaliana na Yanga, tena tukaweka mkataba kimaandishi. Sasa tunasubiri TFF watoe maamuzi,” aliongeza mratibu huyo.
Alipotafutwa na gazeti hili jana kuzungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema kuwa kwa sasa hawana muda wa kuzungumzia suala hilo kwavile Kado si mali yao tena kwa sasa.
“Kado ni mali ya Coastal Union kwa sasa, siwezi kuzungumzia suala la mchezaji huyo maana siyo mali yetu tena (Yanga),” alisema Mwalusako.
Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa sakata la mchezaji huyo limepelekwa kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF ili lipatiwe ufumbuzi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment