STAA wa filamu za Bongo, Vincent Kigosi ‘Ray’ yamemkuta baada ya ile ishu yake ya kutengeneza filamu inayoitwa Sister Marry ambapo mapadri wamemtaka asiipeleke sokoni milele.
Ishu hiyo ilitokea kwenye kikao kizito cha saa 5 kilichofanyika Jumanne iliyopita katika Ofisi za Utamaduni jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa kikao hicho walikuwa Ray, Mkurugenzi Mtendaji wa Utamaduni aliyetajwa kwa jina moja la Mwansoke, mapadri wanne na mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni wa kutoka Ofisi za Usalama wa Taifa.
Kikao hicho kilikuja baada ya hivi karibuni viongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam kumtaka msanii huyo ajieleze kimaandishi ni kwa nini mtawa Sister Marry (Irene Uwoya pichani) alikuwa akifanya matendo ambayo kiuhalisia, Wakatoliki wenyewe huwa hawayafanyi.
Kabla Ray hajajieleza kwa maandishi ndipo alipoitwa huko na kukubaliana ana kwa ana na jopo hilo huku mashinikizo kadhaa yakielekezwa kwake.
Awali, wajumbe wote wakiwa wamekaa kwenye viti, filamu hiyo yenye saa 3 iliwekwa mwanzo mwisho huku mapadri hao wakiguna kila wakati, hasa wakati Sister Marry akiwa anafanya mambo yake mabaya.
Baada ya kumalizika kwa filamu hiyo, hoja zikaanza. Mwansoke akasema vipande vyote vichafu vinyofolewe na kubaki vile ambavyo wajumbe hawakuvigunia.
Baada ya bosi huyo kusema hayo, mapadri wakasema ‘noooo’. Filamu hiyo isiende mitaani hata kidogo kwani imejaa udhalilishaji wa Wakatoliki.
Inasemekana Paroko wa Kanisa la Mtakatifu Maximilian Kolbe lililopo Mwenge Kijijini (jina halikupatikana mara moja) yeye alipigilia msumari wa mwisho kwa maneno aliyoyatoa.
Alisema kwa kuwa filamu hiyo ilirekodiwa kwenye kanisa lake hilo, anataka vipande vyote vya kanisa hilo vitolewe ndipo iingie mtaani, jambo ambalo lilimtoa machozi Ray.
Ray sasa! Siku ya Alhamisi iliyopita, Ray alizungumza na Amani na kukiri kuwepo kwa kikao hicho. Akasema itakuwa vigumu kuviondoa vipande vya kanisa hilo kwa sababu asilimia 85 ya filamu nzima imerekodiwa Maximilian Kolbe.
“Asilimia 85 ya filamu imerekodiwa Maximilian Kolbe, sasa wanaposema niviondoe ni kuimaliza filamu yote. Filamu ni ya saa 3, ukivitoa vipande vya kanisa si itabaki dakika 5 tu,”alisema Ray.
Alisema kikao kiliisha kwa maamuzi hayo, kwamba mtu wa utamaduni alisema vipande vichafu vinyofolewe huku mapadri wakitaka muvi nzima isiende sokoni na paroko wa Maximilian Kolbe akitaka kanisa lake lisionekane kwenye filamu hiyo.
No comments:
Post a Comment