KILA mwanaume anazo hisia za peke yake kuhusu mapenzi. Jawabu rahisi linaloweza kuja ni kwamba wewe unapenda mwanamke mrefu, mwenzako moyo wake taaban kwa mfupi.
Unaweza kukaa pembeni ukawa unamponda mrembo mwenye matege lakini mwenzako hayo ndiyo ‘maradhi’ yake. Anavyotembea yeye hoi! Wewe unapenda mwanya, jirani yako anaona ni kilema.
Hata hivyo, mada hii haizungumzii mitazamo ya wanaume katika mvuto wa hisia hizo. Kinachoangaliwa hapa ni fikra za wanaume na wanawake ambao wao wanapenda ‘kudeti’ nao au kufanya nao maisha.
Ni mitazamo hiyo ambayo inatengeneza makundi. Wapo wanaume wavivu ambao hupenda kuhudumiwa kila kitu, wao wapo kwenye kundi lao. Kuna mabishoo, wao hutaka warembo masistaduu wanaotazamika.
Kimsingi, kila kundi lina namna yake kwa jinsi ambavyo linayatazama mapenzi na wanawake kama viungo muhimu wa maisha. Ni vizuri kuyaweka wazi ili wanawake nao, wawajue vizuri.
KUNDI LA KWANZA
Wanaounda kundi hili, ni vijana wanaopenda kujipambanua kama watoto wa mjini. Hawa siyo ving’asti au marioo, ukasema kwamba wanapenda kulelewa, la hasha! Wanapenda kumiliki masistaduu.
Mara nyingi wanakuwa ni watu wenye dharau na mitazamo yao kwa wanawake huegemea zaidi katika muonekano. Huhitaji wanawake wenye sura na maumbo ya kuvutia zaidi, wakiamini kuwa inawaongezea ‘ujiko’.
Hata mavazi, wanaume wa kundi hili, hutaka wanawake ambao huvaa kimjinimjini. Nguo fupi na suruali za kubana huhusika zaidi. Kwao hudhani kwamba inawafanya wapenzi wao waonekane ni warembo sana.
Wanaume wa kundi hili, wanaweza hata kukataa kuongozana na wapenzi wao pale wanapovaa nguo ambazo haziwatoi kama wanawake wa mjini kweli. Mitindo ya maisha yao, hujaa maonesho.
Kama ambavyo yeye hawezi kutoka mpaka awe amevaa nguo ambazo zinamfanya aonekane brazameni, vivyo hivyo kwa mpenzi wake kwamba hutaka abebe sura ya kisistaduu kweli. Hutaka watu wakubali kwamba mpenzi wake ni mjanja kama alivyo yeye.
Katika kundi hili, ni rahisi kukuta mwanaume ameangukia kwa mwanamke asiye na malengo yoyote ya maisha. Wao kipaumbele chao siyo mtu wa kutengeneza naye maisha, wanachozingatia ni muonekano, mtindo wa mavazi au umbile.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment