ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 25, 2013

Manyanyaso kila kona yalivyoniacha maskini!

Mjane Odilia Anthony (kushoto),akiwa na mwandishi wa habari hii Suzy Butondo mkoani Shinyanga. 

TATIZO la vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo mengi nchini linazidi kuwa sugu licha ya semina, warsha na makongamano mbalimbali yanayoendeshwa ili kutoa elimu  dhidi ya vitendo hivyo.
Mbali ya semina na makongamano pia kila mwaka hufanyika maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Tanzania ikiwa ni moja ya nchi inayoadhimisha siku hizo ambapo pamoja na mambo mengine madhara ya  vitendo hivyo vya ukatili huelezwa, hali si shwari katika maeneo mbalimbali.
Tafiti zinaonyesha kuwa vitendo hivyo vinaendelea kutokea katika maeneo mbalimbali nchini  ikiwamo Shinyanga, mkoa ambao  unatajwa kuwa moja ya maeneo yaliyokithiri au kuongoza kwa vitendo hivyo.
Hali hiyo inathibitishwa na taarifa za hivi karibuni zilizotolewa na Shirika la Utetezi wa Haki za Wanawake na Watoto Mkoani Shinyanga (PACESHI) zikionyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita lilipokea kesi 4,305 zikiwamo zinazohusu ukatili wa kijinsia.
Akitoa ushuhuda  kuhusu hali hiyo, Odilia Anthony, mjane ambaye anadai amenyanyasika kwa muda mrefu tangu alipokufa mume wake anasema amekumbana na mengi.
Yeye ni mjane mwenye mtoto mmoja ambaye awali aliishi kwa raha mustarehe na mume wake, lakini baada ya kufariki kwa mumewe miaka michache iliyopita, ndugu wa mume, yaani wifi, shemeji zake waliibuka wakimtaka yeye na mtoto wake waondoke katika nyumba ya ndugu yao.
“Nilipofiwa na mume, ndugu zake hawakuwa na subira walikuja wakinitaka niondoke. Walianzia ndani mwangu na kuchukua hati za nyumba mbili wakati nikiwa bado kwenye kilio,” anaeleza.
Anaongeza kuwa baada ya siku tatu akizitafuta hati hizo za nyumba ndipo alipobaini kuwa zilikuwa zimechukuliwa.
Ndani ya nyumba alikuta pia cherehani yake imechukuliwa, mabati 16, pamoja na baiskeli.
Mjane huyo anasema aligundua kuwa ni wanandugu ndiyo waliochukua vitu hivyo, lakini alipofuatilia walimweleza kuwa hiyo ilikuwa mali yao kutoka kwa marehemu kaka yao.
“Waliniambia, mimi sina haki ya kubaki na vitu hivyo ,wameamua kuvichukua kwa sababu mwenye vitu hivyo amekwishafariki na wao kama kaka yao wao ndiyo wenye haki ya kurithi  vitu hivyo kwani mimi nililetwa kwa ndoa, sina haki yoyote,” anaeleza.
Anasema wifi zake na shemeji hao walikuwa wakisema kuwa yeye kama mwanamke hawezi kumiliki nyumba, wakizusha kwa kuwa mume wake alikufa kwa Ukimwi naye (Odilia) asingeweza kuishi kwa muda mrefu na hivyo mali za kaka yao zitapotelea kwa watu wengine. “Walidai pia kwamba mtoto aliyemwacha kaka yao hajafanana naye (kaka yao), hivyo inawezekana siyo wake, lazima vitu hivyo viwe mikononi mwao,” anasimulia.
“Nilihangaika, nililia mchana kutwa kwa yote niliyokuwa nikiyapata nikajiona mie sifai kubaki duniani! Nilitamani nimfuate kaburini mume wangu, sikujua ni nani atanisaidia.
“Baada ya muda niliona niende kwa watu wa Serikali ya mtaa, huko nako nikapewa barua ya kwenda mahakama ya mwanzo.
Anasema kuwa huko alipokewa na kuanza kesi ya madai, lakini alivyokuwa akitarajia kusaidiwa aligonga mwamba na kuambiwa kuwa hana haki ya kumiliki nyumba na badala yake ana haki ya kumiliki samani za ndani pekee.
“Huwezi kuamini, kilio changu kilianza upya, tena nikifikiria nyumba zangu zimechukuliwa na shemeji na wifi zangu,” anasema na kuongeza:
“Nililia upya, nyumba tulizojenga na marehemu mume wangu kwa kuhangaika zinachukuliwa. Nilianza kutoa vitu vya ndani ili niondoke, lakini wakati nafanya hivyo, watu waliokuwa wakinionea huruma walikuja na kuniambia kuwa kuna shirika linalotetea haki za wanawake, wakanielekeza huko.”
Anaeleza kuwa aliamua kwenda ofisi hizo na  alipofika  alisikilizwa  vizuri na baada ya hapo aliambiwa aende mahakama ya mwanzo achukue nakala ya hukumu ya kesi yake ya msingi.
“Kweli, nilienda na nakala hiyo nikapewa na kuipeleka katika ofisi za PACESHI ambao walinielekeza niende mahakama ya wilaya. Huko nako wakanisaidia nikakata rufaa. Shirika hili lilinisimamia mpaka nikashinda kesi, nikarudishiwa hati zangu zote mbili za nyumba na sasa ninaishi kwenye nyumba yangu na nyingine nimeipangisha,” anaeleza.
Anawashukuru PACESHI kwa kumtetea mpaka akapata haki yake  na kueleza kuwa laiti wasingekuwa wao asingepata nyumba zake kwani tayari wifi na shemeji zake walikuwa wamechukua.
Anawashauri kinamama wote ambao wanapata shida kama zake waende ofisi za shirika hilo watasaidiwa.
Kwa upande wake, shirika hilo hivi karibuni limezindua  kituo cha msaada wa kisheria katika Kijiji cha Kolandoto, Manispaa ya Shinyanga ambacho kitasaidia kutoa huduma za msaada wa sheria kwa wanawake.
Mratibu wa shirika hilo,  Perpetua Magoke anasema PACESHI inapigania kukuza uwezo wa uelewa wa haki za msingi za kisheria na haki za binadamu katika masuala yanayogusa masilahi ya kifamilia ili jamii iweze kulinda haki za binadamu na kujenga utawala bora nchini ili kukuza uchumi na kusaidia wanawake kuondokana na manyanyaso ya kijinsia.
“Asasi hii ilianzishwa mwaka 1996 kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria cha Wanawake (WLAC). Kwa miaka mitano  tumepokea kesi 4,305, kati ya hizo migogoro ya ardhi ni 1,500, mirathi 500, matunzo ya watoto 450, talaka 345, kubakwa 197, kutumikishwa watoto 155 jinai 150 na madai mengine 1,008,” anasema mratibu huyo.
Anaeleza kuwa shirika hilo linaisaidia jamii kwa kuwawezesha wengi ambao hawawezi kujisemea na kujitetea pamoja na wale walioachwa nyuma kwa sababu ya uelewa wa haki zao wakiwamo wanawake na watoto. Anaongeza kuwa wanawapa uelewa kwa njia ya huduma za msaada wa sheria, mafunzo, utafiti, uchapishaji na utunzaji nyaraka.
“Vilevile, anasema shirika linashirikiana na mashirika mengine kama vile, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) na mashirika mengine ili kukuza uelewa wa haki za binadamu, uraia , demokrasia na utawala bora,” anasema Magoke.
Anaongeza kuwa PACESHI inatoa msaada wa sheria kuhusu masuala yanayomkabili mwanamke kama ndoa, mirathi, ardhi, mikataba na ukatili wa kijinsia.Wanawasaidia wanawake na watoto ambao wanaendelea kuonewa kutokana na mila na desturi katika jamii.  Anaeleza kuwa wamekuwa wakiendesha semina kwa wanawake na vijana ili waanzishe vikundi mbalimbali kwa madhumuni ya kujikomboa kiuchumi na kufanya utafiti kuhusu sera na sheria zinazowanyima haki wanawake na watoto.
Muundo wa shirika
Magoke anautaja kuwa ni mkutano mkuu ambao ni chombo cha juu chenye wajumbe 17 pamoja na bodi ya wakurugenzi yenye wajumbe 6 wakiongozwa na mwenyekiti, mratibu na wajumbe wanne wafanyakazi wa kuajiriwa na wa kujitolea.
“Tunawakaribisha wanawake na watoto, wazee, watu wengine hata wenye ulemavu, wanaoishi na VVU na maskini wa kipato wenye uhitaji wa msaada wa sheria, ofisi zetu zipo Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga,” anaeleza.
“Kutokana na kuonekana manyanyaso mengi kwa wanawake, PACESHI ikiwa ni taasisi inayojihusisha na utetezi wa haki za binadamu hususan wanawake na watoto ndipo tukabuni mradi huu ambao utafikia kata 32 mkoani  Shinyanga,” anaongeza.
Anazitaja kata hizo zilizopo wilayani Shinyanga, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, kuwa ni, Kolandoto, Kizumbi, Ibadakuli, Chibe, Old Shy na Mwawaza, pamoja naHalmashauri ya wilaya ya Shinyanga katika kata za Mwakitolyo, Salawe, Solwa, Iselamagazi, Pandagichiza, na Lyabusalu.
Katika Wilaya ya Kishapu ni kata za Bubiki, Songwa, Sekebugoro, Mondo, Mwadui Luhumbo, Uchunga, Ukenyenge, Itilima na Talaga, Wilaya ya Kahama ni Kahama, Nyihogo,Mhongolo, Nyasubi, Ulowa, Ushetu, Uyogo, Ukune na Malunge.
“Tunakutana na changamoto nyingi katika jamii kutokana na sera ya sheria kutokufahamika, hivyo imekuwa ni kikwazo kikubwa katika jamii na hasa kwa wanawake na watoto kushindwa kupata haki na baadhi ya jamii kuendeleza kukumbatia mila na desturi ambazo zinakandamiza wanawake na watoto hasa wa kike,” anasema.
Mradi huo umefadhiliwa na The Foundation for Civil Society kwa Sh134, 999,670 ukijishushughulisha na kutoa msaada wa kisheria kwa vituo vya kuhama (mobile legal aid) kwenda maeneo ya vijijini kwa kutumia wasaidizi wa kisheria, pia unatoa elimu kwa njia ya sanaa shirikishi na unanuia kuanzisha vituo vidogo kwenye jamii.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Anselm Tarimo anasema kuwa ukatili bado ni mkubwa katika jamii  na suala hili linatakiwa lielimishwe kwa wanafunzi shuleni ili kuwezesha kutambua haki zao za msingi na kupambana dhidi ya ukatili unaotokea ndani ya jamii
“Nawapongeza PACESHI kwa kazi nzuri  ya kuisaidia jamii iishiyo vijijini ambayo ndiyo inayoathirika zaidi kutokana na ukatili unaotokea ndani ya familia na kuufumbia macho kwa kushindwa kufahamu wataanzia wapi kutokana na kukosa elimu juu ya sheria kandamizi na utetezi wao naamini sasa nao watasikia na watajifunza kupitia shirika hilo,” anasema Tarimo.
Meneja Mradi wa Msaada wa Sheria, John Shija anasema Tanzania imeridhia maazimio mbalimbali kama lile la nchi za Kusini mwa Africa (SADC) la 1977 kuhusu usawa wa jinsia na Ukimwi na hivi mwaka 2008  ilisaini na kuridhia mkataba wa nyongeza wa Maputo Protocal ambao ni mkataba unaoainisha haki za wanawake katika nyanja mbalimbali ikiwemo haki ya kumiliki mali na kutokunyimwa mirathi.
Anatoa mfano kuwa Ibara ya 3 ya mkataba huo kuwa imesisitiza ulinzi wa haki ya asili ya mwanamke kibinadamu na kisheria, kuheshimika kwa wanawake kama binadamu wengine, kutekeleza taratibu za kuzuia udhalilishaji wa matumizi mabaya ya wanawake pamoja na kuwalinda wanawake dhidi ya ukatili, unyanyasaji wa kijinsia na matusi.
“Ibara ya 20 inazungumzia ulinzi kwa wajane ili wapate haki ya kisheria na haki za biashara wasinyanyaswe na kudhalilishwa ili waweze kuwalinda watoto wao  na kuwalea vizuri watoto wao baada ya kufariki, pia mwanamke huyo akipenda kuolewa na mtu ampendaye anaweza kufanya hivyo kwa sababu ni haki yake,” anasema.
Pia, Ibara ya 21 inaeleza kurithi fungu stahili la mume anapofariki, kuendelea kuishi kwenye nyumba ya ndoa, kubaki na mali nyumba baada ya kuolewa tena pamoja na kurithi fungu sawa toka kwa wazazi.
Anaeleza kuwa pamoja na jitihada zote hizo bado kuna ukatili wa kutisha dhidi ya wanawake, wapo wanaofukuzwa kinyama ndani ya nyumba, wanaoteswa na waume zao tumekuwa tukipata wateja wengi wanaokuja na matatizo kuwa wamefukuzwa na waume zao baada ya kuwa na nyumba ndogo, hivyo anamfukuza mke wake ili amlete mke mwingine.
Katika kuzingatia haki za watoto, Shija anasema  Tanzania imepiga hatua za kimkataba, na kuwa na sera na hatimaye kutunga Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo inahakikisha inaweka mazingira bora ya makuzi ya mtoto na kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa iliridhia mkataba wa kimataifa wa haki ya mtoto wa mwaka 1989.
Shija anasema mkataba huo ulianza kutekelezwa mwaka 1990, itifaki ya ziada ya mkataba wa haki ya mtoto juu ya kuhusisha watoto kwenye migogoro ya kivita wa mwaka 2000 unaozuia uuzaji wa watoto na kuwahusisha na ukahaba ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2002.
Akizungumzia  kuainishwa kwa haki na sheria hizo, Shija anasema utekelezaji wake bado unasuasua kwa sababu sehemu kubwa ya jamii hazifahamiki hivyo zinabaki ndani ya vitabu na maonyesho kwa wasomaji wa maandishi na wafuatiliaji wa sera na sheria.
Anasema kutokufahamika kwa sera na sheria na mikataba hiyo kwa jamii ni changamoto nyingine ambayo ni kikwazo kwa jamii na hususan kwa wanawake na watoto kushindwa kupata haki zao na kuendelea kukumbatia mila na desturi ambazo zinakandamiza wanawake na watoto wa kike.
“Mila hizo zinawafanya wanawake kuendelea kunyanyasika zaidi kwani kila jambo wanawake hawana uamuzi katika familia na hata masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa sababu mfumo uliopo unawapendelea wanaume na wanawake kubaki duni na kuachwa nyuma katika mambo mbalimbali,” anasema.
Anaeleza kuwa ijapokuwa yapo matatizo mengi yanayowakabili wanawake, suala la kutokuwa na uwiano sawa katika kupata, kutumia na kumiliki mali changamoto kubwa na ni chanzo cha matatizo mengine ambayo yanazidi kuwafanya kuonekana ni viumbe wasiokuwa na thamani katika jamii.
Hata hivyo, Shija anasema wanawake wengi wanajikuta wakifanya biashara ya ukahaba ili kukabiliana na hali duni ya maisha waliyonayo na matokeo yake wamejikuta katika matatizo mengine ya kuambukizwa Virusi Vya Ukimwi, wanawake wengi wamefiwa na waume zao kutokana na Ukimwi wamebaki na watoto yatima, lakini bado wananyanyaswa na kuporwa mali na ndugu za marehemu.
Mwananchi

No comments: